Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia katika Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Awali ya yote naomba nimshukuru tena Mwenyezi Mungu kila siku kwa kutuamsha salama na tukiwa na afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa muda wake anaoutumia angeweza kuwa na familia yake, lakini muda mwingi anafanya kazi kwa ajili ya Watanzania na sote tunaona na tuna-appreciate sana, atambue hilo. Kwa nafasi yake tunamheshimu sana na tunasema tena tunasimama na Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nishukuru Mhimili wa Bunge; Mheshimiwa Spika na wewe Naibu Spika, nawashukuru sana kwa sababu mnaendesha Bunge letu vizuri, mnatupa nafasi na fursa vijana leo hii ni mara ya tatu nachangia. Ahsanteni sana na Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwenye Ofisi hii ya Utumishi na Utawala Bora au Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora nataka nichangie mambo kadhaa. Naomba kwanza niwapongeze sana, mmefanya kazi nzuri sana. Mimi nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, mna mipango mizuri sana kiasi kwamba natamani sana tupate pesa za kutosha. Tupate pesa za kutosha vipi? Tupate pesa za kutosha kwa ajili ya kutimiza yale ambayo tumeyapanga katika mipango yetu endelevu tunayoenda kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano tu TAKUKURU kwa mwaka 2023/2024 wameweza kujenga ofisi tatu za mikoa. TAKUKURU hao pia wameweza kujenga ofisi saba za wilaya katika kipindi cha Mama Samia. Ni kipindi cha mwaka mmoja tu, TAKUKURU hawa hawa wameweza kuajiri watu 350. Ni hatua kubwa sana hiyo ambayo Serikali inafanya na tunawashukuru sana kwa sababu hizi ajira ni za watu wetu, ni za wananchi wetu. Sisi kama Wabunge tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachana na TAKUKURU kwa mambo ambayo imefanya, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeweza kusimamia promotions mwaka 2021/2022 watumishi 91,841 wamepata promotions. Mwaka 2022/2023 promotions 120,210. Mwaka 2023/2024 promotions watumishi 81,515 lakini mwaka 2024/2025 tunakadiria tutaweza kuwapandisha watumishi 219,000. Hizi zote gharama yake ni shilingi 789,615,000 na kuendelea. Hii ni hatua kubwa sana ambayo mmeifanya naomba niwapongeze sana Utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, mmeweza kuajiri katika hiyo miaka, mwaka wa kwanza ule 2021/2022 mmeajiri watu 32,000, mmeajiri tena watu 30,000 kwa mwaka unaofuatia, mmeajiri watu 47,000 na mmekadiria kuajiri watu katika mwaka huu wa bajeti 2024/2025 watu 45,000. Mwenyezi Mungu awatangulie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana mwanzo nilianza kusema kwamba hizi pesa tunazopitisha hapa Bungeni zifike kwenye hii ofisi, kwa sababu tunaenda kuhakikisha ajira za Watanzania zinaenda kupatikana. Tumsaidie Mheshimiwa Rais, tuhakikishe vipaumbele vya ajira vinakuwepo kwa sababu nchi yetu hii changamoto kubwa iliyopo ni ya ajira. Ndiyo maana sasa hivi Serikali imekuja na utaratibu mzuri wa kuanzisha vyuo vya mafunzo ili watu waweze kujisimamia na kujiajiri ambayo ni hatua nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu ambao wamesoma maeneo mbalimbali na wameshatumia muda mrefu sana kusoma lakini ajira hakuna. Kwa hiyo, ajira hizi bado tunazihitaji pamoja na vile vyuo ambavyo vipo, tunavihitaji pia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nigusie naomba zile rufaa zinazotolewa na watumishi mzifanyie kazi kwa haraka sana. Jambo lingine naomba Ofisi hii au Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora, hakikisheni mnafanya tathmini ya kujua ofisi gani kuna wafanyakazi kiasi gani na kuna uhaba wa kiasi gani? Kwa sababu kuna ofisi ambazo wafanyakazi ni wengi zaidi ya ofisi nyingine ili iwe rahisi ninyi ku-reallocate wafanyakazi waende kwenye maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja hayo, nataka pia nigusie suala la uhamisho ambalo kila mtu hapa ameligusia na amelizungumzia. Kusema ukweli mimi kwenye hili nitakuwa tofauti na wenzangu, mnisamehe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mhubiri wa kutokuhamisha watu. Kwa sababu gani? Kwa sababu watu wanakosa ajira kwa muda mrefu, wanapopata ajira wanapangiwa maeneo ambayo kule kuna wananchi na hao wananchi wanahitaji huduma yetu. Hao wananchi wanahitaji huduma yetu jamani. Hivyo basi, kama wananchi wanahitaji huduma yetu, tunahitaji kuwatendea kazi, tunahitaji kuwatumikia, isipokuwa tu pale ambapo mtu atakuwa na sababu za msingi zinazomfanya ahame kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani nitakuwa nimeeleweka kwamba, mimi siyo muumini wa kutaka watu wahamishwe maeneo kwa sababu ya matakwa yao, ila wahamishwe maeneo kwa sababu za msingi zinazowahitaji wao wahame. Kuna sababu za ugonjwa ambazo zinahitaji hospitali kubwa, basi mtu ahamishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri jambo kwamba katika zile ajira ambazo mnatangaza, kwa nini msiainishe kwamba ajira hizi ni za mikoa hii ili wale watu wanaoenda kuomba wajue kabisa wanaomba kwenda kwenye hiyo mikoa, wasiombe kwa ajili ya kutaka kuingia ili wahame? Waombe katika Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata wale wenye matatizo, wanaotaka kuhama, kwa mfano juzi kati kulitokea kesi moja kuna mtu anataka kuhamia Manyara na mwingine anataka kuhamia Dar es Salaam, hawa watu wawili waliweza kuwasiliana wakabadilishana. Ikitokea fursa kama hiyo Utumishi, pitisheni tu kwa sababu hawahitaji gharama zenu, wanahitaji kuhama kwa matakwa yao basi, msiingie gharama kama Serikali ya kuwahamisha mtu kama huyo ambaye anataka kuhama kwenda sehemu nyingine ambayo yeye anaona kwamba inafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo, naomba pia niwashukuru sana Ofisi ya Utumishi na Utawala Bora kwa kuwa mmeweza kutengeneza utaratibu mzuri ambao unaenda kusaidia watu wenye ulemavu kwenye usahili kwa urahisi zaidi. Namaanisha nini? Pale mnapowaita watu wengi sehemu moja, mnatakiwa mtambue mahitaji ya watu wenye ulemavu. Tayari mmeweza kuainisha katika Kamati yetu kwamba mtaweka utaratibu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kwanza wawe ni first priority kwenye interviews, pia kuwawekea maeneo maalum kwa wao kupumzika ili wasipate ile pressure kutokana na hali zao na ugumu wa mazingira kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwapongeze sana kwa kujali hilo, na kwa sababu hii ni Serikali ya Mama Samia, Serikali ya Mwanamke inatambua, inathamini watu wenye ulemavu, pia utu wa binadamu. Kwa hiyo, hongereni sana kwa hilo. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Simbachawene kwa ushirikiano wako, umefanya kazi nzuri sana na unashirikiana vizuri na Kamati yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)