Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipa nafasi hii. Nami nianze kwanza kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumbua wote wabadhirifu na mabaradhuli wote wanaoharibu uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa namna ya pekee niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri wote na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa wanazofanya hasa za kuhakikisha kwamba uchumi wan chi hii unakua. Lakini nimpongeze pia Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Muhongo na Naibu wake Waziri kwa kazi kubwa wanayofanya kwa kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha na hatimaye tuweze kuwa na viwanda vya kutosha na shughuli nyingine za uchumi ziweze kuboreshwa kupitia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nimpongeze tena Mheshimiwa Waziri, nirudie, kwa kuhakikisha kwamba Jimbo langu la Lupembe pia linapata umeme. Nashukuru katika wiki hii vijiji viwili vimeweza navyo kupata mwanga wa umeme kwa mara ya kwanza kati ya vijiji 45; kwa hiyo, bado vijiji 33 havina umeme kati ya vijiji 45. Niombe Mheshimiwa Waziri na vile vijiji 33 vilivyobakia tuendelee kuvipigania ili viwe na umeme nao wajisikie wapo nchini Tanzania kama Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba maendeleo ni umeme. Uwepo wa umeme kwa maana ya nishati ya kutosha ya umeme na nishati yenye uhakika, lakini pia yenye bei nafuu ndipo tutaweza kuwa na maendeleo, lakini kama nishati itakuwa bado bei yake ipo juu wananchi wengi hawawezi ku-afford kuipata bado hatutaweza kuhakikisha kwamba tunaenda kwenye uchumi ambao tunauhitaji.
Niseme kwanza nipongeze kwa kupunguza bei, na umeme toka 1.5% mpaka 2.4%, lakini pia nipongeze kwa kutoa tozo la maombi ya uunganishaji wa umeme ambayo ni application fee shilingi 5,000; lakini pia nipongeze kwa kutoa service charge, hii ilikuwa inawakwaza wananchi wengi sana. Na nipongeze kwa niaba ya wananchi wangu wa Lupembe kwa kupunguza hii kodi maana wananchi kipato cha chini, wataweza kuingiza umeme kwa kutumia tu angalau shilingi 5,000 wanaweza wakapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia kuhusu mradi wa REA. Katika eneo langu na katika Jimbo langu mradi wa REA Phase I hatukupata, lakini tukapata mradi wa REA Phase II, lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kupata umeme hata kijiji kimoja katika REA II. Basi tunaomba vijiji vyote hivi viingizwe kwenye REA III kwa maana ya vijiji vyote 33, tunaomba mtusaidie kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kuna Shirika ambalo linafanya kazi kule kwa ushirikiano wa Serikali, Shirika la CEFA ambalo limeingiza vijiji viwili, sasa tatizo bado ni kadri ya mkataba ile asilimia ambayo Serikali ilitakiwa ichangie naomba tujitahidi tuweze kuwapatia lile Shirika ili liweze kuendelea na kuhakikisha kwamba linasambaza umeme kwenye vijiji vingine ambavyo tayari nguzo zimechomekwa lakini bado nyaya hazijafungwa na hawajazambaza umeme, kwa hiyo niombe hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niombe kupitia ile mradi ambao wa kwanza ulikuwa TANESCO, ile Gridi ya Taifa iliyowenda mpaka vijiji vile vya Lupembe na Igombora, basi kuna baadhi ya vijiji vilirukwa haukushushwa umeme, umeme umekatiza tu umepita katikati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mara nyingi wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba umeme umepita kwenye vijiji vyao, lakini vijiji hivyo havina umeme au vitongoji mbalimbali ambavyo umeme umepita juu haujashushwa. Tuombe tunapopeleka umeme kwenye maeneo hayo au kwenye maeneo mengine tuhakikishe kwamba yale maeneo ambako umeme unapita basi wananufaika na nishati ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia bei ya umeme ilivyo sasa hivi pamoja na kwamba tumepunguza kutoka kwenye asilimia 1.5 mpaka 2.4 bado bei hizi ziko juu. Kuna baadhi ya wananchi wengi wanashindwa kulipia gharama hizi, tuangalie uwezekano wa kupunguza gharama za umeme angalau zishuke kabisa kutoka kwenye ile asilimia ziende chini kidogo ili wananchi wengi wa kipato cha chini waweze kununua na kutumia umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi, tunasema mazingira yanaharibika kwa kutafuta mkaa, wananchi wanatumia mkaa walio wengi lakini pia wanatumia kuni katika kupata nishati. Tukishusha bei ya umeme ukawa wa gharama ndogo au ukawa gharama ambayo wananchi wa kipato cha chini wanaweza wakaununua basi yale madhara ya misitu kwa maana ya kutafuta nishati ya mkaa na kupata kuni yatapungua. Wengi wao watahamia kwenye umeme kwa kuwa umeme utakuwa una bei ndogo, utakuwa wa bei rahisi na wataweza kununua umeme na kwa upande mwingine tutakauwa tunapunguza madhara ya kupotea kwa misitu, tutakuwa tunapunguza uharibifu wa mazingira kupitia kutumia hizi nishati za mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba tujitahidi tuweze kuhakikisha kwamba umeme unapungua uwe na bei ndogo ili tuweze kuokoa mazingira yetu na misitu yetu ambayo kila siku tani za miti zinakatwa kwa ajili ya kupata nishati hii ya kupikia kwa maana ya mkaa na kuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kwamba huduma ya umeme hii lazima tufikirie kuisambaza hasa kwenye maeneo yenye taasisi kama vile shule, maeneo ya Hospitali,na maeneo ya huduma muhimu za binadamu. Kwa hiyo lazima tufikire hilo pia tunasema kwamba tunataka shule zetu ziwe na E-schools, tuwe na E-learning ni lazima tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na umeme ili mipango ya kuwa na E-learning, E-schools kwenye shule zetu uweze kukamilika. Kwa hiyo, tunaomba tupeleke pia kwenye huduma hizi za kielimu na huduma nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naona kuna Waheshimiwa Wabunge wengi wamelalamika sana juu ya kuweka vinasaba kwenye nishati ya mafuta. Kwanza lazima tujiulize sababu zipi zilizosababisha Serikali iweze kuhakikisha kwamba inaweka vinasaba. Ni kutokana na kwamba kulikuwa na uchakachuaji wa mafuta kwa kiasi kikubwa, magari yamekuwa yakiharibika, pampu za magari zikiharibika mara kwa mara na baada ya sisi wananchi kulalamika na Wabunge tukaja tukaa na tukajadili, tukaamua kwamba tupitishe sheria ya vinasaba. Kwa hiyo, vinasaba hivi ni muhimu, naomba Waziri na Baraza zima la Mawaziri viendelee, kama kuna matatizo madogo madogo basi yafanyiwe uchunguzi tuweze kuyatatua lakini sio kusimamisha hili suala la vinasaba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeona faida zake, udhibiti wa uchakachuzi wa mafuta umepungua lakini pia Serikali imekuwa inapoteza mapato mengi sana hasa kwenye mafuta yale yaliyopo on transit kama walivyosema wenzangu. Kwa hiyo, kwa kuweka vinasaba tunaweza tukabaini kwamba haya mafuta yamepitiwa na vinasaba, watu wanaokagua vinasaba na haya mafuta hayajapitiwa. Kwa hiyo, kwa kwa kufanya hivyo tutadhibiti upotevu wa kipato cha Serikali na hivyo Serikali itaweza kupata pato lake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hasara kubwa kama nilivyosema ya haya mafuta kulikuwa na wizi mkubwa sana wa mafuta ambayo yanakuwa kwenye on transit, kulikuwa na wizi mkubwa sana wa mafuta yaliyopo kwenye migodi. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo maana yake tutapunguza madhara ya wizi wa mafuta ambao ulikuwa unapelekea hasara kubwa hasa wenye migodi wenyewe, lakini kwa upande mwingine ulikuwa unapelekea hasara Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana kwa nafasi.