Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa afya na uzima wa kuendelea kulitumikia Bunge letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaanza kwa kusema kwamba, katika historia ya nchi yetu tulijitambulisha kote duniani kwa sera na mielekeo yetu kwamba hii ni nchi ya wakulima na wafanyakazi. Katika kujitambulisha hivyo, tulisimamia kazi zote za wakulima na wafanyakazi kwa kiwango cha juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hapa kwamba bahati nzuri tunaye Rais ambaye ni msikivu, tena ambaye anajali. Unaposikia tunazungumza habari ya 4R za Rais, haziendi katika jambo moja tu. 4R za Rais zinaenda kwenye kila jambo, maana kuna watu wengine wanafikiri hizi 4R zipo kwa ajili ya siasa tu, Tume Huru ya Uchaguzi sijui na nini, Hapana. Ni katika kila jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza suala la haki za watumishi, haki za wafanyakazi waliopo kazini na wanaostaafu, tunazungumza jambo kubwa kwa mustakabali wa nchi. Kwa maana hawa wafanyakazi ndio wanaotafsiri kwa vitendo maamuzi ya Bunge hili, maamuzi ya Serikali, na maamuzi ya Rais. Ni hawa hawa mpaka maamuzi ya Mahakama ikihukumu mtu kwenda jela, ni hawa hawa wanaotafsiri maamuzi hayo. Kwa hiyo, ni lazima tuendelee kujenga mazingira mazuri kwa wafanyakazi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo malalamiko mnaendelea kuyafanyia kazi kama Serikali, lakini bado hamjafikisha sehemu nzuri malalamiko hayo. Ni haki za watumishi kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hivi kuna haja gani ya kumhamisha mtu kama hamna fedha? Sioni haja kama hamna fedha msimhamishe mtu, maana mkimhamisha mnatengeneza deni ambalo halina sababu isipokuwa tu kwa mtu mwenyewe ambaye kaamua kwamba mimi niko tayari kujihamisha mwenyewe, basi ahame na kwamba halipwi. Mtumishi unamhamisha kwa mamlaka yenyewe ya Serikali kuamua halafu humlipi. Kwa hiyo, jambo hili nilitaka niseme kwamba katika kipindi hiki kinachoendelea, mjaribu kuendelea kuliweka sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, mmefanya kazi nzuri katika suala la upandishaji madaraja watumishi, lakini bado wapo Maafisa Utumishi kwa makusudi anakwambia, jina la mtumishi fulani nililisahau. Ni lazima Wizara ichukue hatua kali kwa Maafisa Utumishi wa namna hii ambao wanafika mahali hawatendi haki kwa watumishi wengine. Mwingine anafanya kwa makusudi tu kwa sababu hawaelewani na mtumishi huyo, anasema jina lake lilisahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, heshima hii na hadhi ya mtumishi iende mpaka anapostaafu. Ni kweli tulikaa hapa tukaamua kwamba tukitazame kikokotoo tukakitazama, baada ya kuamua tumerudi kwa wananchi, tumerudi kupitia maamuzi yetu, tunaona kabisa kwamba maamuzi yetu haya kwa ujumla yana kasoro katika ustawi wa jamii ya wastaafu. Tumeliona hilo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais huyu ni msikivu na Serikali hii ni Sikivu. Zaidi ya hilo, sera zenyewe za Chama cha Mapinduzi zinataka kuwaangalia watumishi na wastaafu. Turudi tuyatazame yale maamuzi na kurekebisha. Najua Serikali hii haishindwi, tumeamua na kurekebisha mambo makubwa kama Azimio la Arusha, tumeamua na kurekebisha mambo makubwa kama sera yetu ya Serikali kumiliki njia kuu za uchumi, mpaka tukafika mahali tukasema Serikali sasa inabaki kuwa mhimili wa shughuli za uchumi, lakini njia kuu za uchumi zisimamiwe na sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeamua mambo hayo makubwa ya kisera, hatushindwi kurudi kutazama tena kikokotoo ili tukirudishe katika nafasi yake ya ustawi wa maisha ya wataafu. Jambo hili siyo jambo la kufumbia macho ni lazima tulichukulie hatua haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali kwa hatua iliyoichukua kuhusu TASAF. Kwa maana leo tunapozungumzia TASAF, ukimfufua mtu aliyekufa miaka 10 au 20 iliyopita, haijui TASAF. Ni Serikali hii imeona umuhimu wa kuwasaidia watu wa familia zenye kipato cha chini ndiyo ikaleta TASAF. Kwa hiyo, lazima tuishukuru kwanza Serikali kwa kuileta. Hata hivyo, katika utekelezaji wa TASAF, tunakutana na changamoto ambazo lazima tukae kujadiliana na kuzirekebisha, lakini Serikali yenyewe kuleta jambo la TASAF ilifanya jambo kubwa na zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna matatizo kwenye TASAF kwa upande wa ulipaji kwa wakati, vilevile ulipaji katika masuala ya usimamizi. Mwenyekiti wa Mtaa anasimamia kazi kubwa kwenye TASAF, lakini anazidiwa na mtu aliyeitwa kuja kusimamia kazi siku moja ya kuelekeza barabara. Kwa hiyo, lazima tuangalie katika ulipaji wa TASAF, namna gani tunawalipa hawa wasimamizi na namna gani tunalipa kwa wakati hawa ambao wanahusika na TASAF yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie, najua kwamba majeshi yetu kwa ujumla yanao utaratibu wake, lakini wanajeshi vilevile ni watumishi wa umma. Naomba Wizara hii ya Utumishi hebu jaribuni kukaa na Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara nyingine, muangalie hii kitu kinaiutwa PGO. PGO ipo tangu ukoloni, Police General Order kuna vitu mle vimepitwa na wakati kabisa. Askari wa cheo cha chini, nafasi yake katika kulitumikia Jeshi la Polisi kwa raha, ni ndogo sana. Anaambiwa kwenye PGO kwamba anapotaka kwenda likizo akabidhi nyumba. Sasa unakabidhije nyumba wakati familia yako ipo humo? Hayo yote bado yamo kwenye PGO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Askari anaambiwa, akiajiriwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu asizae. Maana yake hata akipata mtu wa kumuoa leo hawezi kumuoa maana hatakiwi kuzaa ndani ya kipindi cha miaka mitatu. Haya mambo yote tuyatazame. Hivi yana ustawi katika utumishi wa sasa wa Jeshi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Wizara ya Utumishi, ninyi ndio mnaobeba dhima kubwa ya masuala ya utumishi nchini, angalieni hizi Kanuni zote za Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja za majeshi, kwa sababu wanajeshi kwa nidhamu yao hawana mahali pa kulalamika, wasemaji wao ndio sisi. Mimi hapa hata nikisema sichukuliwi hatua na afande yeyote, niko huru. Kwa hiyo, tunawasemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni haki zao za uhamisho. Askari anakwenda uhamisho au likizo, anarudi, halipwi mwaka unaisha, mwingine unakuja. Hapa katikati tuliweka utaratibu mzuri kwamba Askari wawe na posho kila katikati ya mwezi ili kuwafanya wasipate dhiki, wakafikiria namna ya kuombaomba hela kwa wananchi. Nasikia ile posho mmeiondoa, mmeipeleka mwisho wa mwezi. Irudisheni katikati ya mwezi. Posho ile nia yake ilikuwa ni kumfanya Askari muda wote awe na pesa za matumizi ili asishawishike kuomba hela ndogo ndogo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilitaka Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara zinazohusika, watusaidie kurekebisha mambo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)