Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii nami kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uhai nami niweze kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo mengi ambayo anaifanyia nchi yetu hata kwa kutangaza nafasi za ajira kwa vijana wetu ambayo itapunguza kwa kiwango fulani changamoto ya ajira kwa vijana wetu wengi waliopo kwenye maeneo tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nawashukuru Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii. Hawa ni miongoni mwa wachache sana waliowahi kutembelea Kilolo tangu nimekuwa Mbunge kwa nyakati tofauti. Jimbo la Kilolo halipokei Mawaziri wengi wala Naibu Mawaziri, lakini hawa wawili wote wameshafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe Mheshimiwa Naibu Waziri, alipokuja alikuwa na ahadi yake kwa kupitia TASAF kukamilisha ujenzi wa zahanati mbili ambazo wananchi wameziibua. Zahanati ya Winome na Zahanati ya Kijiji cha Mkalanga. Nimkumbushe ndugu yangu kwamba wale wananchi wanakumbuka ziara yake na wanajua akitoa ahadi huwa anazitekeleza; na kwa hiyo, na hiyo nayo ataitekeleza kama alivyokuwa ameahidi. Mimi nitaendelea kumkumbusha kila tunapoonana mpaka hapo atakapotimiza ahadi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie dhana ya kujitolea na jinsi inavyofanywa hapa Tanzania na athari zake kwa vijana wetu ambao wanajitolea. Tanzania ina baadhi ya kada ambazo zina mfumo wa internship kama udaktari, na lengo lake huwa ni kupata uzoefu, ina mwongozo, ina namna ya kupata posho na kwa kweli imeundwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba Tanzania hatuna uzoefu wa jinsi ya kufanya internship, tunao na tungeweza kujifunza kupitia madaktari. Kwa bahati mbaya mfumo huo Serikali haijataka kuuchukua kwa kada nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tumekuwa kwenye Kamati ya USEMI tuliomba kwamba mwongozo utakaotengenezwa utoe fursa ya internship iliyokuwa organized vizuri, tangu upatikanaji wa watu kwenda kwenye internship, kwamba wanapatikanaje ili kuondoa uwezekano wa watoto wa walimu wakuu wa shule na watoto wa wenyeviti peke yao kupata nafasi za internship. Ili kuondoa upendeleo lazima kuwe na namna bora ya kupata watoto wa kujitolea kwenye hayo maeneo kwa sababu hata kujitolea huwa ni fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ukishapata mwongozo huo lazima kuwe na muda maalumu wa kujitolea na namna ya kuwapa motisha wale wanaojitolea. Sasa kama kwa mfano, Tanzania tungeweza kufanya kila halmashauri iwe na vijana angalau 100 wanaojitolea, maana yake kila mwaka tungekuwa na vijana 18,400 kwenye maeneo mbalimbali wanajitolea. Hao ni wengi na kwa hiyo, ingetosheleza kwa angalau kuwapa nafasi ya kupata uzoefu. Jambo hili tumelizungumza muda mrefu, lakini utekelezaji wake umekuwa kwa kuchelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mkiwa na data base nzuri ya kujitolea, faida yake ni kwamba, inapokuja wakati wa ajira tusingekuwa na kizungumkuti cha kusema kwamba hatuwezi kutumia hii nafasi ya vijana kujitolea kwa sababu hatufahamu. Kwa sababu siku za nyuma imesemwa kwamba haitumiki nafasi ya vijana wanaojitolea kwa sababu inaogopwa kwamba vijana wanaweza ku- forge au wanaweza wakafanyaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi madaktari wanapofanya internship, daktari anaweza aka-forge? Kwa nini kwa mfumo ule ule isitumike kwa watumishi wengine kama vile walimu, sekta za afya za chini? Ili tuwe na uhakika kwamba huyo amejitolea, assessment zimefanyika na kwa hiyo, inapofika wakati tunasema huyu aingie kwenye ajira kwa sababu amejitolea, inakuwa inajulikana kabisa kwamba kweli huyu amejitolea na tathmini zake zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mwongozo huo upo, azingatie haya mambo, wanapatikanaje? Wanasimamiwa na nani? Assessment inafanywa na nani? Wanalipwaje? Baadaye, uwezekano wa acceleration ya wao kuajiriwa unakuwaje ili tuweze kuondoa changamoto hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kuzungumza ni kuhusu watendaji wa kata na watendaji wa vijiji. Hawa ndio ambao wanaonwa kwenye vijiji. Serikali za Mitaa kwa kiwango kikubwa ndio wanaotegemewa kuwahudumia hawa wananchi kila siku. Hata hivyo, kwenye maeneo mengi kuna upungufu mkubwa sana wa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Mitaa na badala yake wanaokaimu ni baadhi ya viongozi kama Wenyeviti wa Vitongoji au wananchi wanaojitolea ambao uelewa wao dhidi ya kazi hiyo siyo mkubwa. Tukumbuke kuwa hawa wanakuwa na mihuri, wanakuwa wanaweza kukusanya baadhi ya mapato, na kwa hiyo, wanapopata mafunzo kwenye hivi vyuo vyetu huwa wanapata uelewa wa jinsi ya kufanya haya mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja pale Iringa mjini na ninajua aliona upungufu ule ulivyokuwa, lakini afikirie, je, kwenye zile kata zote, ni nani alikuwa anakaimu wakati wale watu hawapo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii namna ya kukaimu hata hakuna mwongozo wa jinsi ya kukaimu, kwamba kama kijiji hakina mtendaji awepo nani? Kwa hiyo, ni mtu yeyote yule ambaye Mwenyekiti wa Kijiji ataona anafaa, basi huyo huyo ndiye atakaimu. Kwa hiyo, ilitakiwa kwanza kuwe na maelekezo maalum kwamba kijiji kama hakina mtu ni nani anakaimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kufanya haraka kuhakikisha kwamba vijiji vyote vina watendaji kwa sababu wanafanya kazi kubwa na muhimu sana kwenye hayo maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, hawa watu wanatoka kwenye vyuo, na siku hizi angalau unakuta mzazi amejitahidi, amejichanga changa amepata shilingi 350,000 kamnunulia laptop ili afanyie kazi. Wanapofika sasa kwenye ofisi zenyewe za kata na za vijiji hakuna laptop, hakuna printer, barua zinaandikwa kwa mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala ni kwamba je, tumeshindwa kweli kutengeneza mfumo mzuri wa angalau kuhakikisha kwamba kuna vitendea kazi na teknolojia inayofaa? Umefika wakati kwamba hata wao wenyewe jinsi ya kufanya vitu kwenye halmashauri wanatakiwa wafanye kwenye mfumo. Sasa, unafanyaje kazi kwenye mfumo wakati kitendea kazi hauna? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kuna haja ya Wizara hii na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuzungumza ili kuhakikisha kwamba angalau hawa watumishi, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, wanapata laptop. Kama Serikali ikiona kwamba zile mpya ni gharama, zipo used tutawaonesha, tutaenda tutanunua wapewe maana hata wakiwa kwenye vyuo walitumia hizo. Kwa hiyo, sasa anaporudi huku hawezi kuchukua ya nyumbani kwake aje atumie huku, hilo litakuwa limeboresha sana utendaji wao wa kazi, wataandika hizo barua kwa kutumia hivyo, wataweza kufanya hivyo vitu kwenye mfumo, lakini pia tutakuwa tumeboresha mazingira yao ya utendaji kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo nataka nizungumzie ni hili suala la wastaafu na mafao yao, hasa wakati wanapokwenda kudai na kukuta kwamba Serikali haikupeleka michango na hii inaweza ikawa ni halmashauri au idara nyingine yoyote ya Serikali. Halafu yule mtumishi anaambiwa yeye atoe hela zake ili mishahara itimie ndipo alipwe mafao. Hili linafanyika na ushahidi upo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninachofikiri ni kwamba, na yule mzee unakuta anastaafu, anazunguka, anaenda anarudi, ataenda NSSF sasa hivi mifuko imeunganishwa, ataenda na kwingine. Mimi nafikiri ni wajibu wa yule ambaye kwenye lile eneo analostaafu yule anayemstaafisha kuhakikisha kwamba huyu mzee mstaafu mafao yake yanapatikana na michango yake yote inapatikana badala ya kuwaacha hawa wazee ambao wamelitumikia Taifa, wanateseka kwa muda mrefu wakitafuta namna bora ya kupata mafao. Jambo hili kwa kweli linawaumiza sana wazee wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sidhani kama Serikali imeshindwa, pengine ni vizuri kufanya tathmini ni wastaafu wangapi sasa hivi michango yao haijapelekwa na ni nani alizembea? Kwa hiyo, aliyezembea apeleke, na wastaafu wanapostaafu waweze kupata mafao yao bila shida. Pengine ni vizuri, ni kweli kuna namna ya kusema mtumishi awe anakwenda kwenye mfuko kuangalia mwenendo wa mafao yake kila wakati, lakini pia ni wajibu wa mwajiri kuhakikisha kwamba anapeleka ile michango yake kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila upande utimize wajibu wake, lakini inapotokea Serikali haikupeleka michango, basi mara yule mtumishi anapostaafu pengine kutengenezwe mfuko maalum utakaolipa yale mafao ili huyu mtumishi alipwe halafu ninyi mwendelee kumtafuta yule ambaye alikuwa hakupeleka hayo mafao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia ni wakati ambapo inatokea watumishi wanaomba kuhama hasa wale wanaotaka kuhama kwa sababu ya ndoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kweli wapo watu ambao unakuta anataka kutoka kwenye mojawapo ya Wilaya za Kigoma kule Buhigwe kuja Kilolo, tena vijijini, kwa sababu anamfuata tu mke wake au mume wake. Sasa zipo nyingi ambazo ni halisi, nadhani kumetokea dhana kwamba ndoa inatumika kama kisingizio cha kuhama. Kwa hiyo, hata wale halali hawahudumiwi na hawapewi umuhimu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri sisi sote tunafahamu umuhimu wa familia na tunafahamu umuhimu wa kuhakikisha kwamba hawa watumishi wanakuwa eneo moja, hasa pale ambapo hizo sehemu zote zina upungufu, kwa sababu anayehama kutoka kwenye kijijiā€¦(Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Justin, ahsante sana.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)