Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kuwapongeza kwa kazi nzuri hasa kuhakikisha kuwa baada ya muda mrefu watumishi wanapanda madaraja na kulipwa stahiki zao. Pamoja na changamoto za hapa na pale, lakini kwa ujumla kazi nzuri imefanyika, nawapongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nina ushauri mahususi hasa kuhusu nafasi za Watanzania kufanya kazi katika Taasisi na Mashirika ya Kimataifa. Kumekuwepo na manung'uniko kwamba watumishi wanaopata nafasi za kwenda kufanya kazi katika Taasisi na Mashirika ya Kimataifa baada ya kumaliza mikataba wakirejea wanarudi katika ngazi ile ile aliyoondoka nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba, kwa kuwa mtumishi huyu alienda kufanya kazi kwa mfano kwa miaka mitatu, mitano au nane, akapata exposure na uzoefu zaidi, basi akirejea na akakuta wenzake wamepanda ngazi na yeye aendelee katika ngazi ile ambayo wenzake pia wameshapanda. Kwa kufanya hivi, itawamotisha wengi kuomba nafasi hizo katika Taasisi na Mashirika ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, naambiwa kwamba kuna nyakati hata zile nafasi ambazo ni kama share yetu katika baadhi ya taasisi ambazo nchi yetu ni wanachama kama vile SADC na kadhalika zinakosa watu (Watanzania) kwa kuwa tu ama watumishi wetu hawajaomba au kwa kukosa mwamko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa jumla ni kwamba Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje iwe na mkakati maalum wa kuwahamasisha watumishi wetu kuomba nafasi katika taasisi na mashirika ya Kimataifa, na ikibidi hata kuwajengea uwezo wa namna ya kupata nafasi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nina watumishi katika Halmashauri ya Mafinga Mji ambao wamekuwa wakikaimu, mmoja mwanasheria ambaye amekuwa akifanya kazi kama Mkuu wa Kitengo cha Sheria toka Halmashauri inaanzishwa mwaka 2015, kuna wakati aliletwa Mkuu wa Kitengo lakini hakukaa sana akaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kanuni na taratibu za kiutumishi, nashauri watumishi wa aina hii wawe rewarded kwa kuzingatia uwezo wake kikazi na muda ambao amekaimu. Kwa mfano, mwanasheria huyu ametusaidia sana kuokoa mamilioni ya fedha kutokana na kushinda kesi za ardhi na za madai ambazo nyingi tulirithi kutoka Halmashauri mama ya Mufindi DC.

Mheshimiwa Naibu Spika, wa pili ni Kaimu Mweka Hazina wa Mafinga Mji, ambaye kupitia barua yenye Kumb. Na. HM/MAF/CS.20/PF.140/14 ya tarehe 04 Januari, 2024 aliombewa kuthibitishwa/kupandishiwa mshahara. Mtumishi huyu nilipomwuliza shida ni nini, alinifahamisha ana CPA, lakini hana masters.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufahamu wangu, akiwa na CPA kwa mhasibu ni sifa muhimu kuliko hata masters. Ushauri wangu, naomba watumishi wa aina hii Serikali iwatazame kwa macho mawili hasa kwa kuzingatia kwamba baadhi ya wenzao wenye sifa kama wao wanakuwa wamethibitishwa katika nafasi kama hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni suala la recategorization. Ushauri wangu wa kila mwaka kwenu ni kwamba mtumishi akifanyiwa recategorization, basi walau abakie na mshahara wake. Kwa mfano, mwalimu ambaye yuko kwenye TGTS F, akasoma na akafanyiwa recategorization akawa HR, ni wazi lazima aanzie HR Daraja la Pili, lakini mshahara wake abakie nao ule ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuongea na Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete akafafanua kwamba mwajiri anaweza kumwombea mtumishi aliyefanyiwa recategorization mshahara binafsi, lakini mimi naliona gumu kiutekelezaji. Hivyo ni vyema ikawekwa openly kuwa mtumishi akifanyiwa recategorization automatically mshahara wake utabakia ule ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza tena maana katika lolote linalofanyika hapa nchini, engine ni utumishi wa umma. Mmebeba dhamana kubwa na Mwenyezi Mungu awasimamie katika utendaji wenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha