Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba kila uwekezaji mpya huchochea uchumi mpya kukua, lakini vilevile inakwenda kuchagiza ongezeko la kodi ambalo linaenda kuchangia katika maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia uwekezaji, tunaangalia mambo matatu. Tunaangalia miradi inayosajiliwa, ajira zinazotokana na miradi hiyo iliyosajiliwa pamoja na mtaji.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ukurasa wa 10, ameonesha mwenendo wa uwekezaji nchini kuanzia mwaka 2020 – 2023. Nasema kweli, kwa mwenendo ule nina kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuweza kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika miradi iliyosajiliwa na TIC kati ya mwaka 2020 – 2023, mwaka 2020 miradi ilikuwa 207 na ikapanda mpaka 2023 ikafikia miradi 526. Natambua kwamba mwaka 2019/2020 kulikuwa na shida ya COVID ndiyo maana hii miradi ilikuwa siyo mingi, lakini tangu kuapishwa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwezi Machi, 2021 amefanya kazi kubwa sana ya kuongeza miradi iliyosajiliwa TIC kati ya mwaka huo 2020 – 2023. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa miradi hiyo imeweza kuchagiza mitaji kutoka mwaka 2023 dola za Kimarekani 1,092.7 hadi kufikia dola za Kimarekani 5,704. Vilevile idadi ya ajira ziliendelea kuongezeka kutoka 17,385 mwaka 2020 hadi kufikia 137,010. Naweza kusema kwamba kwa takwimu hizi Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba ameendelea kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Wizara, kitu cha kwanza napenda kuishauri Wizara iendelee kufanya ufuatiliaji katika miradi ambayo imesajiliwa. Kwa hiyo, muimarishe suala zima la ufuatiliaji wa miradi hiyo ambayo imepatikana. Vilevile mfanye kazi kwa kushirikiana na sekta pamoja na Wizara nyingine kama vile Wizara ya Madini, Wizara Kilimo, Wizara TAMISEMI, Wizara Utalii, Wizara Viwanda na Biashara pamoja na Wizara Nishati.
Mheshimiwa Spika, natambua kabisa kwamba kulikuwa na changamoto ya kutokupatikana kwa umeme, lakini na sehemu nyingine ambazo umeme ulikuwepo, ulikuwa unakatikakatika. Kipekee, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kukamilisha miradi ya umeme ambayo itawezesha kutatua changamoto hii. Nampongeza kwa kukamilisha mradi mkubwa wa umeme kama wa Julius Nyerere.
Mheshimiwa Spika, sisi Watanzania tunaamini kwamba kwa kukamilika mradi huu, kutachochea uwekezaji na pia itaondoa kabisa zile changamoto ambazo zilikuwa zinatokea kwenye viwanda ambavyo vimeshaanzishwa na vitakavyoanzishwa. Hivyo basi, tutaenda kuchagiza uchumi wetu na vilevile kuvutia wawekezaji kwa kuwa na nishati ya umeme ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, narudi kwenye mikoa na halmashauri zetu. Kule kwenye mikoa yetu na halmashauri zetu kuna idara za uwekezaji, viwanda na biashara; na ziliwekwa kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji pamoja na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo katika maeneo yetu nchini kwetu. Kule mikoani kuna Wakuu wa Mikoa, kuna Wakuu wa Wilaya, na kwenye Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri kote huko kuna hizi idara za uwekezaji wa viwanda na biashara.
Mheshimiwa Spika, kuna fursa nyingi ambazo zinatoka kwenye wilaya na mikoa yetu ambazo zingeweza kusaidia kuchagiza katika uwekezaji. Hivyo basi, nilikuwa nawashauri Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wasimamie vizuri fursa ambazo ziko kwenye maeneo tunayotoka kule wilayani na mikoani ili kuweza kuisaidia Serikali katika kufungua mwanya mkubwa wa uwekezaji katika nchi yetu. Hii ni kwa sababu wao ndio wanaziona moja kwa moja fursa ambazo ziko katika wilaya zetu kwenye maeneo ya utalii, kilimo na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa kila Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba anaisaidia Serikali katika kutambua fursa hizo za uwekezaji sambamba na kuboresha miundombinu ambayo itasaidia kurahisisha uwekezaji wa haraka. Kwa mfano, kuangalia barabara zetu, kuangalia viwanja vya ndege ambavyo sehemu husika vinahitajika viwepo ili kuvutia wawekezaji waweze kuja kuwekeza na kuweza kukuza uchumi wetu. Vilevile tupate kodi ambayo itasaidia katika kutatua kero na katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)