Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kurudia pongezi zilizotolewa na wengi. Shukurani kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume ya Mipango na kuunda hii Wizara ya Mipango na Uwekezaji ambavyo vyote ni taasisi, ameviweka chini ya ofisi yake. Tunaamini kwamba taasisi hizi zimeweza kuanza kutekeleza majukumu yake kwa kasi ya juu sana kutokana na usimamizi shupavu wa Mheshimiwa Rais mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo pamoja na timu yake, Dkt. Kida, Lawrance Mafuru pamoja na Mchechu na wafanyakazi wote wa pale kwenye Wizara hii mpya.

Mheshimiwa Spika, kama ungeniambia niseme majumuku ya hii Tume ya Mipango ni nini? Yameorodheshwa 20, lakini naweza kusema ni coordination ya Mipango ya Serikali; ni coordination ya Sera za Serikali kwenye sekta mbalimbali. Kila sekta inakuwa na interest zake. Kwa hiyo, kila sekta inataka ipate zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu ambaye ni neutral, au taasisi ambayo ni neutral ambayo Wabunge walisisitiza iundwe, ni Tume ile, kwa sababu haina sekta. Kazi yake ni kuhakikisha kwamba resources zinakuwa allocated in a balance manner ili uchumi ukue in a balance way. Kuwe na both, social and economy balance. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta za jamii zisipokee too much zikasahau kwamba ili sekta za jamii ziweze kuzalisha huduma zile ambazo zinahitajika za afya, elimu na kadhalika, ni lazima zipate fedha kutokana na sekta za uzalishaji, sekta za kilimo, viwanda na huduma mbalimbali kwa jamii, pamoja na sekta nyingine. Kwa hiyo, naamini kwamba sasa tumepata chombo ambacho kitatuwezesha kututengenezea mipango ambayo ina tija kwenye maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchangiaji wa mwanzo alisema tusianze tena kuongeza walimu na kadhalika, lakini kazi ya mipango ndiyo hiyo, kuona kwamba ni wapi ambapo sasa tulenge rasilimali yetu ili iweze kuchaji maeneo yale ambayo yamekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna dhana moja kwamba ili uweze kwenda sawasawa, ni lazima uweze kusema nalenga kitu gani? Inavyoonekana, mwelekeo wa Tume so far, au wa Wizara, zaidi unalenga wawekezaji wakubwa kutoka nje, na wawekezaji wa ndani wakubwa.

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kwamba nchi hii haiwezi kutoboa bila kulenga SMEs na wawekezaji wadogo wadogo, ambao ndiyo kule chini tuliko, ndiyo kule kwenye halmashauri zetu tuliko, wawekezaji wadogo; kuona ile mikopo ya wanawake, vijana na walemavu isimamiwe namna gani ili iweze kuleta tija? Iendelee kutolewa kwa mbinu zipi? Ni kitu gani cha ziada kifanyike ili mikopo inayotolewa kwa kupitia empowerment funds zote na kwa namna nyingine ambayo mabenki yanatoa ili iweze kuleta tija kwenye uchumi wetu na fedha yetu iwe na thamani na kadhalika?

Mheshimiwa Spika, naomba katika vitengo vyote, na sijaona kama kuna kitengo kwenye hii Wizara ya Mipango kinachoshughulika na wawekezaji wadogo wadogo na SME. Ukishakuwa nacho na kikatumia sasa wale Maafisa Mipango na Maafisa Uwekezaji kwenye halmashauri, tutaweza kuhamasisha uwekezaji mdogo mdogo na kufanya incubations ili watu waweze kutekeleza miradi midogo midogo ambayo itakuwa ina-hide kwenye mnyororo kwa thamani (value chain) wa hawa wakubwa wakubwa ambao Mheshimiwa Rais amefanikiwa kupata.

Mheshimiwa Spika, ninaamini pia kwamba hawa wawekezaji wanaosajiliwa kwenye TIC, pia hiyo orodha ingekuwa inachapishwa ili tujue ni wapi wanaenda kuwekeza, ili nasi tuanze kujipanga, wanapokuja kuwekeza tuweze ku-supply vile vitu ambavyo wanahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri hilo ni la msingi sana na ninaamini pia kwamba suala zima la PPP liwekewe mkazo kwenye Wizara hii ambayo ndiyo inaenda kusaidia kuona kwamba wakubwa na wadogo wanapata msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, pia niseme kwamba kuna ile investments forums ambazo zilikuwa zinafanyika, zilikuwa zimeanza kwenye mikoa na kwenye wilaya mbalimbali na naona zimefanyiwa tathmini na Tume. Naamini kwamba hizo nazo sasa zianze kuhimizwa ili ziweze kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango ni think tank, kwa sababu ina-coordinate vitu vingi na inatakiwa iwe na utaalamu, iwe na watu ambao inawasaidia katika kufanya utafiti. Wasifanye utafiti wenyewe, wawe na Taasisi za Utafiti. Sasa kuna Taasisi za Utafiti kama REPOA. Na-declare conflict of interests, mimi ni Board Member wa REPOA.

Mheshimiwa Spika, ESRF, REPOA na Taasisi nyingine hata Vyuo Vikuu kama Sokoine wana taasisi na Idara za Tafiti. Sasa watenge fedha kwa ajili ya utafiti. Kwa mfano taasisi hizi ninazotaja, hiyo sarafu, wanapata kidogo, lakini wanapata fedha za nje, ni wafadhili ndiyo wanafadhili utafiti ambao unaenda kusaidia Serikali hii kutengeneza sera za kiuchumi na kutengeneza mipango ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani, kwa nini hawajatenga fedha kwa ajili ya taasisi za utafiti? Naomba sana, sijawahi kushika shilingi ya Waziri, lakini nitashika shilingi kama hatasema kwamba ametenga kiasi gani cha fedha ambazo zitaenda kugawa kwa hizi taasisi za utafiti ili zimsaidie yeye na zitusaidie sisi Wabunge pia.

Mheshimiwa Spika, watu wanakuja kutusaidia kutupa percentage kwenye Kamati ambazo hata wazungu hawawezi kutengeneza. Wale wanakujanazo wanatuelewesha namna gani mapato yanaweza kukua, kwa nini hatuwapi fedha? Naomba sana jamani, naomba sana Mheshimiwa Waziri na Profesa Kitila uende ukaangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilishangaa kidogo, huwezi kuwa na mpango ambao hauna bajeti, yaani bajeti na mpango zinaenda sambamba, zile process zinaenda sawia. Ukiniambia kwamba msimamizi wa Tume ya Wizara hii ya Uwekezaji na Mipango na Tume yuko kwenye; sijui namna gani unapita kwenye Kamati ya Bajeti. Kwa sababu mimi niko kwenye Kamati ya Bajeti na sijaona chochote na nilikuwa nasita hata kuchangia, lakini nimeona nichangie tu kwa sababu ni vizuri kuchangia.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nafikiri kutafutwe namna yaku-link hapo ili Kamati ya Bajeti iweze pia kupata nafasi ya kuona mipango hii na ndiyo watu wanaweza pia wakajua bajeti inaweza kuwa ya namna gani? Siyo tu ya Wizara, lakini bajeti kwa ujumla na mipango ya kutekeleza mipango hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimefurahi sana kuona kwamba blue print inatekelezwa kwa ujumla na inatekelezwa vizuri, na inawasilishwa kwenye wasilisho. Hata hivyo, nafikiri ni wakati sasa wa kusema kwamba hii blue print tui-review tena, tuone kwamba ni kitu gani bado kimebaki? Ni kitu gani kimefanyika, lakini kimefanyika kinyume ya namna tulivyotarajia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupunguza tozo siyo kusaidia uwekezaji. Unaweza ukatoa tozo zote na usipate hata mwekezaji. Kuna vitu vingine ambavyo vinahitajika ili uwekezaji uweze kuonekana katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri anayehusika aone namna gani pia ya kurahisisha na kuelimisha umma ni kitu gani kimefanikisha kwenye hili la kurahisisha uwekezaji na kuhamasisha au kupunguza gharama za uwekezaji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafurahi pia kuona kwamba Tume chini ya Mheshimiwa Mafuru imeanza sasa kufikiria upya namna ya ufuatiliaji, kwa sababu ufuatiliaji na tathmini ndiyo jambo kubwa pia katika kuhakikisha kwamba fedha inapata thamani. Sasa kama kweli Tume inafikiria namna hii, maono yake ni kwamba tutengeneze mifumo ya ufuatiliaji. Mradi ukiingia tu kutekelezwa kunakuwa na dashboard ambayo hata Mheshimiwa Rais mwenyewe anaweza akaona dashboard kwamba mradi huu sasa umefikia hapa na hapa na hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliona juzi Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alituonesha pale. Unaenda pale unaangalia Bwawa la Nyerere, huna haja ya kwenda kule, unaliona linavyotiririsha maji na linavyozalisha umeme. Ni mambo ya namna hiyo tunataka kuona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaweza ukafungamanisha ule mfumo wake wa mradi na mifumo mingine, ukafungamanisha, na kila mtu anaweza akajiaonea, hata Spika akikaa ofisini kwake akaweza kuona akiingia kwenye websites. Siyo lazima atengenezewe mfumo wa ajabu, ni web base system ambao mtu ukiingia ukitaka kuona huo Mradi wa SGR umefika wapi? Unaingia, unaona. Mradi huu umezalisha kiasi gani au umekufa au ni kitu gani? Unaona. Naomba tuendelee kwa mawaidha hayo ili tuweze kurahisisha shughuli nzima ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kwamba mawanda ya ufuatiliaji ya Tume yako limited kwa sababu ya resource ya watu pia. Sasa kuna miradi hii ya Pension Funds, miradi ya Pension Funds inafadhiliwa na nani? Kwa sababu ile miradi katika zile sijui shilingi trilioni 76 au 78 alizosema Mheshimiwa mwenzangu ni kwamba, nyingi pengine ni miradi ya pension.

Mheshimiwa Spika, sasa tunachouliza, inafadhiliwa na nani? Return kwenye Assets ya miradi ya Pensions ni zero point something percent. Mimi nashukuru kwamba sasa hivi Registrar Mheshimiwa Mchechu ameanza ku-recruit wasimamizi na Bodi kwa njia ya ushindanishi na ameanza kuwapa mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa huyu kwa sababu anajua mambo, naomba katika mafunzo anayotoa, achukue top business schools, Harvard Business School kuna wahadhiri wazuri, waletwe wawafundishe hawa watu namna ya kusimamia, wanatoa case studies ambazo ni nzuri. Mkienda kule tutatoboa, seventy six trillion is a lot of money. Kwa hiyo, mimi naamini kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga…

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nilifikiri nitazungumza kidogo sana, lakini naona muda umeenda.

SPIKA: Mheshimiwa, nakupa dakika moja, malizia.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba basi tuangalie namna ya kutumia wahadhini kutoka kwenye top business school, kwa sababu ni njia pekee ya kuweza ku-sharpen skills za management katika nchi yetu na katika Mashirika ya Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)