Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja ya Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere moja ya vitu ambavyo alituachia na akilihutubiia Taifa miaka ile, maadui wetu wakubwa walikuwa ni watatu ambao sisi watoto wake na wajukuu zetu tunatamani nao wajue kwamba maadui hawa tunaenda nao namna gani? Alituambia maadui hao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Mheshimiwa Spika, leo nijadili jambo moja tu la umaskini wa Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Duniani nchi hutegemea rasilimali zake ili kujikwamua na kujitoa katika umaskini. Afrika ilikuwa ina-host sana wageni kutoka Bara la Asia miaka ya nyuma kwa sababu gani? Bara la Asia walikuwa na hali ngumu ya uchumi. Kwao mvua zilikuwa hazinyeshi na ndiyo utamaduni wao na ndiyo tabia ya nchi za kwao. Sisi mvua zilikuwa zikinyesha na tunapata chakula na walikuwa wanakuja kuhemea katika nchi hizi, tukawa hadi na ukoloni ambao umetokana na Nchi za Kiarabu katika Pwani ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa maana gani? Kwa maana kwamba, sisi uchumi wetu tunazo rasilimali, kama wale ambao walikuwa wanakuja hapa kuhemea chakula, leo wana rasilimali ya mafuta na gesi, sasa tunaenda kuhemea kwao vitu vya viwandani kwa sababu tumeshindwa kuheshimu rasilimali yetu ambayo tunayo na kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Tanzania kama Jamhuri ya Muungano, tunayo gesi asili, leo toka tumeanza mchakato wa kufanya gesi hii iwe kimiminika kuwa LNG mchakato huu ni miaka 12 sasa bado upo juu ya meza na hatujamaliza, shida yetu nini? Nadhani wale tunaowateua kuwa katika meza ya mazungumzo inawezekana nao wana shida, kwa sababu wanapokaa vikao wanapewa posho, sasa hawawezi kumaliza mchakato kama zile posho zitakatika. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, huwezi kuchakata jambo kwa miaka 12, toka 2012 mpaka leo bado LNG ipo kwenye mchakato. tunategemea nchi hii kweli tutakwenda? Hebu tuone mifano michache ya nchi ambazo zimenufaika na gesi asilia, Qatar juzi walikuwa ni host wa World Cup, hawana rasilimali nyingine zaidi ya gesi. Wenye uchumi mkubwa duniani, wanaoshindana na Marekani, Warusi uchumi wao mkubwa unategemea gesi na mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati tunapigana vita vya Uganda na nchi jirani hapa, mtu aliyetusaidia mafuta ilikuwa ni Nchi ya Algeria lakini Algeria uchumi wake mkubwa haubebwi na mafuta umebebwa na gesi. Leo sisi tuna gesi kwa miaka 12 tumekaa tunazungumza juu ya meza ni namna gani twende, namna gani tufanye, tunashindana wapi? Wapi tunakwama? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, natamani kuiona Tanzania kwa macho yangu angalau pamoja na umri huu mkubwa, lakini natamani kuiona nchi hii inanufaika na rasilimali zake. Leo pale Dar es Salaam kuna vituo vichache vya CNG. Ukikuta foleni ni kama hapa na kule CBE, magari yanasubiri kujaza gesi. Hivi kweli Watanzania tupo hapo? Namwomba Profesa na timu yake na Tume hii ya Mipango, watupe mipango endelevu juu ya hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tunaagiza LPG (Liquid Petroleum Gas) kwa ajili ya kupikia, lakini sisi tuna natural gas hapa ambayo tunatakiwa tusambaze tu mabomba, watu wapikie gesi. Tulishindwa kutengeneza biogas hata vijijini tu kwa uwekezaji wa Serikali, leo ni msamiati, mtu ukimwambia biogas ni nini hapa Tanzania, hajui. Namwomba Mheshimiwa Kitila Mkumbo Profesa wa Uchumi atusaidie kwenye mambo haya, waje na mipango ambayo itawezesha kama nchi tutoke hapa kwenye mchakato tufike mahali sasa uchumi wetu ubebwe na gesi asilia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unajua gesi asilia ikishachakatwa kuwa kimiminika itabebwa na meli kwenda nchi nyingine. Leo lazima utengeneze pipe ili gesi ifike Dodoma, sasa tunashindwa hapo lakini hata kuchakata? Kuzungumza na mtu kuzungumza na mabenki, trilioni 100 ni nini? Wakati tunakwenda kuokoa bajeti ya miaka na miaka!
Mheshimiwa Spika, leo Bunge hili tunaidhinisha bajeti ambayo ina utegemezi wa zaidi 38%, kwa nini tusitoke huko? Tuna vitu vya kutosha, tuna rasilimali ya gesi asilia ya kwetu ipo ndani ya ardhi. Hata kama huyo anayetuchimbia anachukua kiasi chake kuna ubaya gani? Wewe una shamba huwezi kulilima akaja mtu akalima na wewe ukapata chakula shida ipo wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninalo jambo lingine ambalo natamani kulichangia leo, tuna mipango mingi ya Serikali katika kilimo, katika nishati, katika barabara, katika maji, katika afya, katika maliasili na maeneo mengine lakini hatuna mipango ya maendeleo vijijini. Nchi yetu 80% ya wananchi wetu wanaishi vijijini. Leo tuna dude kubwa TAMISEMI linasimamia maeneo yote Majiji, Manispaa, Miji, Miji Midogo na Vijiji, hivi kweli tutafika?
Mheshimiwa Spika, natamani kuona waje na mipango ambayo itafanya tuje na mpango ambapo aidha kuwe na Mamlaka au Taasisi, aidha chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo itashughulika na maendeleo vijijini peke yake. Leo TAMISEMI wanashughulika na elimu msingi hadi sekondari kidato cha sita, TAMISEMI hao hao wanashughulika na afya kuanzia zahanati mpaka hospitali za wilaya. TAMISEMI wanashughulika na maeneo mengi yanayohusu maendeleo ya jamii kule kwetu kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa waje na mipango ambayo itatupa Taasisi nyingine ambayo aidha ni Wizara au ni Idara au ni namna gani watatusaidia wataalamu, tuje na kitu ambacho kitasimama kwa ajili ya maendeleo vijijini peke yake ili nchi nayo iweze kwenda. Huwezi kuchanganya vijiji na majiji kama Dar es Salaam, Mwanza au Dodoma halafu wakawaweka katika level moja, hatuwezi kufika. Natamani kuona haya yatokane na mipango ambayo tutakwenda nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie jambo la Msajili wa Hazina, ametuonesha dhamira njema. Juzi tulipokuwa na maonesho ya nishati hapa kuna vitu nimevibaini naomba nivizungumze. Tuna TGDC hawa watu wa joto ardhi, tunao TPDC, tunao TIPA na tunao EWURA wote ni wamoja. Kwa nini tusije na Taasisi moja nzito yenye nguvu yenye kusimamia haya mambo? Huyu anayechakata utafiti wa gesi na mafuta kule baharini na huku maeneo mengine ni mwingine, akitaka kuzalisha anakuja mwingine, hizi taasisi kwa nini haziendi pamoja? Pia, mifumo ya Serikali haisomani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huyu anayefanya exploration akishatoa taarifa yake haisomwi na mwingine inabaki kwake na mwingine mpaka akaiombe. Kwa nini tusiwe na uwazi na tujenge mifumo? Nataka niombe pia ikiwezekana eGA waingie hapa waweze kuona mifumo ya Serikali kama kuna exploration, basi taarifa zake ziwe wazi kila mahali ili hata kama kuna mwekezaji mwingine atataka kwenda mbele zaidi ya huyu alipoishia aweze kuona.
Mheshimiwa Spika, natamani kuona nchi yangu inakwenda lakini haiwezi kwenda ila kwa mipango ambayo imeundwa na Wizara hii ya Uwekezaji na Tume ya Mipango, watu wa Mipango wa Wizara ndiyo watatusaidia zaidi kwa sababu Tume wao wataangalia namna gani, kwa sababu Mwenyekiti wa Tume hatuwezi kumgusa, tunamgusa huyu ambaye ni wa kwetu.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimeona nitoe maoni haya na naunga mkono hoja hii ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji. Ahsante sana. (Makofi)