Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimshukuru sana na jirani yangu Mheshimiwa Kiswaga kwa ukarimu wake kwa kunipa dakika tano hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo pamoja na Naibu wake Dkt. Kalemani kwa kazi kubwa wanayoifanya. Lakini nianze kwa kupeleka salamu maalum za shukrani kuungana na watanzania wengine kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna alivyosimamia uamuzi wa kushirikiana na Uganda kujenga lile bomba la mafuta kutoka Uganda kuja kupitia Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba ujenzi wa bomba lile ulikuwa na ushindani mkubwa, ni hitajio la kila nchi inayopatikana ndani ya mipaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wae ule, pia umebadilisha siasa za nchi za Afrika Mashariki, kwa hivi tunampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo tunakupongeza sana kwa namna ambavyo ulisimamia utekelezaji ule ukiongoza kikosi cha wataalam hongera sana pamoja na timu nzima ya Serikali. Dkt. Kalemani miezi miwili iliiyopita ulikuwa Sengerema, tunakupongeza sana kwa ziara iliyoifanya, mafanikio yake tumeshayaona, lakini kuna moja nilitaka nikukumbushe Mheshimiwa Kalemani, tulivyokuwa pale katika ule Mgodi wa Nyanzaga ulisema uliwapa siku 14 wale wachimbaji wenye leseni ile ambayo wamepewa ambayo ni ya Acacia, ulisema utawaandikia barua uwape notice ya siku 14, waeleze kama wana nia ya kuendeleza ule mgodi ama laa, na kama hawatakuwa na nia Serikali ichukue uamuzi mwingine kwa kutoa leseni ile kwa watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatarajia kwamba Mheshimiwa Waziri, utakapokuwa unafanya hitimisho/majumuisho yako ya jioni ya leo basi utatoa hatima na mwelekeo wa Mgodi wa Nyanzaga ambao unapatikana katika Jimbo la Sengerema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 30 wa hotuba ya Mheshimiwa Profesa Muhongo ambayo kwa kweli imebeba mambo mazito na mazuri, mojawapo ya mambo yanayozungumziwa pale ni kufikisha umeme katika baadhi ya maeneo ambayo hayafikiki kirahisi, hayafikiwi na umeme wa Gridi ya Taifa. Na mazingira ya maeneo hayo yanayozungumziwa ni pamoja na visiwa, Jimbo la Sengerema ambavyo msemaji ndio anaiwakilisha ina maeneo ambayo hayafikiki kirahisi, nina visiwa kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alivyokuwa anachangia jana Mheshimiwa Dkt. Tizeba alisema hapa, lakini mimi nataka niungane naye kwamba katika yale aliyozungumza ni pamoja na visiwa vya Juma Kisiwani, Chitandele, tuna kisiwa cha Chikomelo kule pamoja na Lyakanyasi. Nilikuwa naomba mtakapokuwa mnatafakari kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kirahisi msije mkasahau visiwa vinavyopatikana katika Jimbo la Sengerema na Wilaya ya Sengerema kwa ujumla ikiwemo Jimbo la Buchosa kwa ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba na maeneo mengine ambayo tunakumbwa na hilo jambo ambalo tuko katika maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri inatukumbusha kwamba malengo ya Serikali kufikia mwaka 2020 katika eneo la uzalishaji umeme tunakusudia tuwe tumefikia uzalishaji wa umeme kiasi cha megawati 4,915 kutoka kwenye 1,500 tulipo sasa. Nilichotaka kusema nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kufafanua, kuna miradi mingi imetajwa hapa, lakini kwa mahitaji haya na mkakati wa Serikali sasa hivi wa nchi ya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, tunaamini demand itaongezeka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka atusaidie katika mipango tuliyonayo, je,ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya Hydro, inayotokana na nguvu ya maji ama vinginevyo kwa sababu tuna potentials kama Stiegler’s Gorge lakini tuna Mpanga, Ruhuji, Mnyera, Rukose, tuna kule Kilombero, tuna maeneo mengi ambayo yanaweza kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji. Tunataka kujua tu kama katika mpango wetu wa kulitoa Taifa hili, kufika hapo mblele tunakususia kujumlisha hii miradi mikubwa ambayo inaweza kuzalisha umeme kutokana na nguvu ya maji/
Mheshimiwa Mwenyekiti,la mwisho, kwa sababu ni dakika tano tu, tarehe 21 Aprili, Shirikisho la Wachimbaji na Watafutaji wa Madini walitoa taarifa wakifafanua ushiriki na uwezesho na namna ambavyo wao wamechangia katika uendelezaji wa uchumi wa Tanzania. Katika baadhi ya mambo waliyoyazungumzia walitoa hisia zao na taarifa zilitoka kwenye vyombo vya habari vingi tu kwamba mpaka sasa hivi wameshachangia kiasi kikubwa. Lakini hoja ninayoizungumzia hapa ni kwamba tunaiomba Serikali itoe ufafanuzi itakapokuwa inafanya majumuisho, kwa sababu mchango wa kwenye Pato la Taifa wa sekta ya madini sasa hivi ni asilimia tatu pointi kadhaa. Lakini sisi tuna dira ya Taifa hapa inasema katika sekta ya madini tunakusudia mchangowa Taifa uwe umeshafikia asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema kwa sababu maandalizi ni sasa, miaka tisa, kumi iliyobaki sio mingi sana, pengine katika hatua hii Mheshimiwa Waziri, pamoja na Serikali nzima inaweza kukusaidia kutoa mwelekeo kwamba mikakati iliyopo kutoka kwenye asilimia tatu na ukizingatia changamoto zinazopatikana katika sekta ya madini duniani sasa hivi, ni mikakati ipi tuliyonayo ya kutoka hapa kusogea mbele kufikia hiyo asilimia 10 ifikapo mwaka 2025?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naungana na Watanzania wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa tunayoifanya katika kuendeleza sekta. Lakini pia nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, wameanza vizuri sana wamefanya kazi kubwa sana, tunakushukuru sana na tunawatakia kila la heri.