Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Pili, nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai. Leo kama siku nyingine nilizopata kuchangia namshukuru kwa fursa hii. Pia, niwashukuru familia yangu kwa kunivumilia kwa muda mrefu nikifanya kazi hii ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo langu lakini na wananchi wa nchi hii kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, binafsi nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya kutengeneza ustawi wa nchi hii. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa kama nilivyosema hapo mwanzo kwa sababu kila tunachojaribu kukiongelea kuhusiana na jitihada zake alizozifanya zipo wazi.
Mheshimiwa Spika, mimi binafsi nawaasa wasaidizi wake kwenda na kasi yake. Mheshimiwa Rais amekuwa akienda kwa kasi kubwa kiasi cha kuwaacha baadhi ya watendaji wengine wakiwa wanatambaa. Sasa kama nilivyosema ni muhimu sana watendaji na wasaidizi wake kwa ujumla tukajitahidi kutaka kuangalia na kufahamu kwamba Mheshimiwa Rais ana maono gani na anatarajia nini kutoka kwao, hali kadhalika matokeo ya kile anachokitarajia huko mbeleni ni nini?
Mheshimiwa Spika, ukiangalia ni kama vile sehemu hizi mbili kuna nyimbo hizi mbili tofauti zinaimbwa. Upande huu huku inachezwa nyimbo hii lakini upande mwingine unacheza wimbo mwingine; hakuna correlation. Natofautiana kidogo na wenzangu kuhusiana na suala la Tume hii ya Mipango kwamba labda inaweza ikatutoa sana katika mazingira yetu tuliyokuwa nayo kama sisi hatutabadili mind set zetu; kwa sababu gani?
Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwamba mipango ilikuwepo muda wote, hakuna hata mwaka mmoja ambapo mipango ilisimama. Kilichobadilika ni kwamba mipango hii imebadilishwa katika utekelezaji kwamba nani anaisimamia. Kuna wakati mipango hii ilisimamiwa na Wizara ya Fedha, kwa hiyo Idara ikawa ndani ya Wizara. Kuna wakati pia mipango hii ilikuwa imesimamiwa yenyewe ikiwa na Wizara maalum kabisa ikijitegemea kufanya mipango.
Mheshimiwa Spika, muda huo wote tumeona kwa kadiri mambo yalivyokuwa. Hali kadhalika hivi sasa toka mwaka 2023 Tume ya Mipango pia imerudi ikijitegemea na kuwa ni Wizara kamili kabisa ambayo inashughulika na mipango hii. Kwa hiyo nyakati hizi zote mbili tumepitia, kipindi ambacho Wizara imeshughulika na mipango, lakini kipindi ambacho Tume imeshughulika na mipango. Bado kumekuwa na mapungufu kwa nyakati hizo tofauti, licha ya kama nilivyosema viongozi wetu wakubwa kwa maana ya Marais kwa muda tofauti tofauti, kujitahidi sana kuhakikisha kwamba ustawi wa nchi hii unakuja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo jitihada zao binafsi zilikuwa zikionekana, lakini mipango ile ilikuwa inashindwa kuunganika kutoka kwa wenzetu, watekelezaji. Kwa hiyo kama nilivyosema nafikiri mind set ni muhimu sana katika kuhakikisha tunavuka hapa tulipo. Kusema peke yake kwamba Tume ya Mipango imekuja, kwa hiyo tutakuwa na hali nzuri, huko ni kujidanganya. Tunahitaji ku-change mind set completely kutoka kwa watendaji na wale wanaopanga hii mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikisema kwamba ni kwa nini, ni jitihada binafsi? Ukiangalia kutoka mwaka 1996 mpaka kufikia hivi leo, TIC ilivyoanza kusajili wawekezaji ilisajili takribani watu au kampuni 12,381 zilizokuwa na nia ya kuja kuwekeza katika nchi hii. Tafsiri yake ni nini? Kampuni hizi au watu hawa kama wangekuwa wamekuja wote wangetuletea pesa za Kimarekani takribani bilioni 117. Hizi ukizibadilisha ni pesa nyingi sana. Ni kama shilingi trilioni mia mbili hivi na kitu, ni pesa nyingi mno.
Mheshimiwa Spika, sasa pesa hizi kama zingekuja maana yake nini? Zingeleta mtaji kutoka pesa ya kigeni kuja hapa kwa kiasi cha pesa nilichokitaja hapo. Impact ya hii ingekuwa ni nini? Kungekuwa na vitu mbalimbali vingejitokeza. Kwanza hawa wawekezaji wanakuja na pesa ya kigeni kama nilivyosema kwa maana kungekuwa na pesa ya kutosha kwenye reserve kwa maana ya dola ya kutosha kwenye reserve. Hii ingeimarisha Uchumi, kwa sababu gani? Kwa sababu pesa yetu ya Kitanzania ingeimarika, kwa maana mahitaji ya dola yangekuwa yanaenda proportional kabisa na uwepo wa pesa hiyo.
Mheshimiwa Spika, si kama hali iliyopo sasa hivi kwamba tunatamani kuwa na matumizi ya dola kwa ajili ya kununua au kuingiza kutoka nje, lakini dola hizo hatuna tunalazimika sasa kuzinunua dola zile kwa kutumia pesa ya Kitanzania, pesa nyingi sana. Wakati ambapo ungeweza ukanunua kikombe kwa shillingi mbili unalazimika kununua kikombe hicho hicho kwa shillingi 100 na sababu ni tofauti ya dola (exchange) iliyotokea pale.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona kwa kiasi gani athari inajitokeza kwa kuja na kiasi hicho kikubwa cha fedha. Maana yake tungekuwa na fedha nyingi kwenye uchumi na uchumi ungekua. Pamoja na hiyo hali jinsi ilivyo, kungekuwa na wawekezaji wengi, kiasi hicho kingi cha fedha kingeingia. Hatuoni na hiyo fedha haionekani wala wawekezaji hawajaja kwa kiwango hicho. Hii inaonekana kwa uhalisia wa hali ya malalamiko yaliyopo sasa hivi ya dola na ni tafsiri ya wazi kabisa kwamba hizi fedha za kigeni ambazo kupitia kwenye investors hawa, ambazo wangezileta kama miradi hazipo au kama zimekuja basi ni kiwango kidogo.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalozungumzia kwamba hakuna correlation ya mipango ni pale ambapo tunatamani kabisa miradi mikubwa ya kimkakati, ambayo tungetamani tufahamu kama imeshaanza kufanya kazi, ni kama vile Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mradi huu umezungumzwa tangu wengine sisi hatujazaliwa, lakini mpaka sasa hivi bado umebaki kuwa kwenye karatasi. Kila wakati wa mipango, iwe ni mipango ya kutoka kwenye Wizara au kutoka kwenye Tume yenyewe, bado mpango huu ulikuwepo na umeendelea kuwa kwenye mchakato.
Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie kwamba, hili neno la mchakato ndilo neno gumu sana na tena linaleta ukakasi mkubwa, kwa sababu mara nyingi sana kila kinachoshindikana kufanyika kwa kifupi tu utapewa taarifa kwamba, bwana hili jambo liko kwenye mchakato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mradi mkubwa, kwa mfano Mradi wa Gesi Mtwara. Huu ni kati ya mradi ambao tungetegemea kwamba nchi hii isingekuwa hivi ilivyo. Tulipewa matarajio makubwa sana wakati ule mradi unaanza na kila mtu alielewa hivyo kwa sababu uhalisia ndivyo ulivyo. Nchi kubwa zilizoendelea zenye vyanzo vya gesi zimekuwa zikiendelea kwa kasi kubwa, lakini ule mradi bado umebakia kwenye mchakato. Ukiuliza utaambiwa kwamba hili jambo liko kwenye mchakato na kama kuna kiwango kimetumika au kimetusaidia ni kiwango kidogo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halikadhalika Mradi wa Gesi ya LNG, ndugu zangu wa Likong’o pale kuna wakati nalazimika kuwakimbia, nikipita pale hata kusimama sisimami kwa sababu nikipita pale swali la kwanza kuulizwa ni kuhusiana na mradi huu, kwamba unakuwaje na utaanza lini.
Mheshimiwa Spika, kuna project pia ambazo tumeshawahi kuzizungumza hapa; mimi mwenyewe nilishawahi kuzizungumzia kama vile Mradi wa Magadi Soda, Engaruka. Mradi huu umeendelea kuwa kwenye karatasi kama miradi mingine. Kwa hiyo ukiangalia hapa ninachoweza kuzungumza ni kwamba Waziri aliye kwenye nafasi hii sasa achukue reference kwenye miradi ile yote ambayo iko kule nyuma na failures ambazo tumekutana nazo kusudi...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa, dakika moja malizia.
MHE. ISSA ALLY MCHUNGAHELA: ... tuweze kujirekebisha, twende katika hali ile inayotarajiwa na watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)