Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Ofisi hii ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Nafahamu kabisa kwamba Serikali imefanya vizuri sana kurudisha Ofisi hii baada ya kutolewa kwa muda fulani. Kama wenzangu walivyosema, tunaamini sana vijana ndio watakaolisaidia Taifa hili na Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kitila ni kijana, hivyo naamini katika ujana wake atasimamia na kuhakikisha anasaidia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda niseme kwamba, katika mambo ya uwekezaji kumekuwa na shida kidogo katika maeneo ya kuboresha mazingira ya uwekezaji. Ninapozungumzia maeneo ya mazingira ya uwekezaji namaanisha uwekezaji wa nje na wa ndani pia. Tukienda kwa wawekezaji wa nje, tuliomba hapa siku za nyuma kuwepo na one stop centre. Tukimaanisha one stop centre siyo majengo, kwamba ataiona TRA hapa au ataiona OSHA hapa, bali tunataka huduma na utendaji wa haraka. Hicho ndicho tunachokitaka na si majengo na kuwa na ofisi tu peke yake. Kwa hiyo, inawezekana ndugu yangu Mheshimiwa Waziri anaenda kwa speed lakini akawa amewaacha wenziwe nyuma, wale watendaji wake. Kwa hiyo, naomba sasa performance appraisal aisimamie vizuri kwenye Wizara yake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo wawekezaji wengi wanalalamika, anaweza akafuatilia kitu kwa mwaka mmoja au hata zaidi. Sasa siyo vizuri Mheshimiwa Waziri na ikumbukwe kwamba Tanzania hatujajitenga, kuna majirani zetu wanaweza wakawaalika hao wawekezaji. Kwa hiyo tusipofanya kazi kwa bidii na kwa u-smart tutaendelea kulalamika na kuwa watazamaji wa maendeleo yakienda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu wawekezaji wa ndani, kuna watu wanawekeza; tumesema viwanda vya kati ni viwanda muhimu sana katika kukuza uchumi wa Taifa hili. Kwa mfano mtu anafungua kiwanda cha kusaga unga na ni mzawa, anapata shida kubwa sana kupata documents. Anapata shida sana kila siku kuripoti nenda hapa rudi hapa. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kama nilivyosema, atumie elimu yake na ujana wake ili kuhakikisha kwamba Taifa lake linasonga mbele. Tunaomba uwekezaji huu uwe wa makini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati imetoa maoni hapa kuhusiana na kutenga ardhi ya wawekezaji. Ni vyema kujua ni eneo gani wawekezaji watakuwepo. Ni kweli wakijazana sehemu moja pia pana madhara na hatimaye isiwe mtu anapotaka kuwekeza kitu tunaanza kuhangaika tunamweka wapi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kuna wawekezaji hasa kwenye sekta ya madini wamechukua maeneo makubwa kabisa. Ikumbukwe kwamba watu wetu wamezaliwa katika maeneo haya. Unaenda kwenye maeneo kama Nyamongo unakutana na watu waliozaliwa pale, maisha yao yote wako pale; lakini anakuja mwekezaji anachukua eneo kubwa na halitumii kwa wakati na wale watu ambao ni wazawa, wanakosa sehemu ya kufanya ule uchimbaji mdogo mdogo. Kwa hiyo nafikiri ili uchumi uendelee ni lazima kwanza kila mtu kuanzia ngazi ya chini awe anashika hela kiasi. Kwa hiyo tunaomba waweke mazingira mazuri kwa vijana wetu, lakini na ardhi yetu pia itunzwe na mtu anapopewa ile ardhi aiendeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mashamba makubwa kama vile ya Mbarali yamekaa kwa miaka na miaka na wananchi wanaozunguka maeneo yale wanapata shida ya kulima; mwisho wa siku wanaenda kukodisha na kumpatia mwekezaji faida na kumwacha Mtanzania katika hali isiyofaa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri asimamie maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu uwekezaji wa vijana. Tumemaliza sensa juzi hapa, leo hii tuna asilimia kubwa sana ya vijana. Vijana hawa tusipowawekea msingi wa kujua ni namna gani wanaweza kutoka katika maisha yao tutakwama kama Taifa. Naomba sana tuhakikishe vijana hawa wanajengewa uwezo wa kuwekeza kwa level zote; level ya chini, ya kati na ya juu. Tuhakikishe, kama ni vijana tunawasimamia. Kwa mfano Soko la Kariakoo, pale utakuta kuna wawekezaji wenye rangi nyeupe, naomba nisitaje mataifa yao kwa sababu unajua hili ni Bunge, siwezi kuwataja. Naomba wawepo wazawa zaidi na kwa upande wa wageni, kutokana na mitaji waliyonayo wapewe uwekezaji mkubwa ili uwekezaji huu mdogo mdogo waachie watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii huwezi kwenda kwenye nchi jirani ukasema kijana wa Kitanzania anakwenda kuwekeza eneo ambalo jirani yetu Mkenya, Mganda na mtu yeyote akaacha watu wake akawapa watu wako; siyo sawa, naomba msimamie hilo. Mtazame hata hao wanaokuja kuwekeza kwenye madini pia, ni lazima tuhakikishe watoto wetu wanafaidika.
Mheshimiwa Spika, kuna ujanja unaotumika, mtu anakuja kuwekeza anatafuta bosheni, anamtafuta Mtanzania, anachukua document zake halafu inaonekana kama na yule Mtanzania ni mwekezaji, lakini baada ya muda mfupi wanamwacha kwenye mataa na watu wetu elimu hiyo hawana. Naomba kama Serikali wasimamie hilo ili kuhakikisha Watanzania hawa hawadhulumiwi na wanapata haki, fifty-fifty ile ambayo imeandikwa BRELA au sehemu nyingine yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali iongeze mitaji kwenye mashirika ya umma ambayo tunafikiri yalianzishwa kwa ajili ya kuongeza uchumi wa Taifa letu. Tunaomba wapewe mitaji. Kuna wakati unaweza ukalaumu, ukasema watu wetu hawafanyi kazi lakini bajeti inapitishwa katika Bunge lako, 40% ndiyo inawafikia; wanawezaje kuendelea. Tunaomba sana, Bunge ni taasisi kubwa, inapopitisha fedha halafu 40% au 35% tu ndiyo inatoka, nafikiri hatuwatendei haki wataalam ambao wamesoma kwa kodi za Watanzania, naomba Serikali iwekeze fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, viongozi waliotutangulia kama Mwalimu Nyerere walifanya mambo makubwa, alipoanzisha ZZK - Mbeya alijua kwamba Nyanda za Juu Kusini kunahitaji dhana za kilimo, leo hii yamekuwa magodauni ya pombe. Alipoanzisha viwanda mbalimbali vingine vikubwa, wao wamesoma wanaelewa na ndiyo maana walienda shuleni wengine walikimbia, tukakimbia wao wakaenda, basi wachangamke, kuangalia, kuchanganua vizuri na kujua ni namna gani tunaweza tukalisaidia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani bado tuna nafasi ya kutengeneza. Madini yetu yatatuongezea sana fedha. Leo Mwadui wamechimba miaka 84 kama siyo 86, lakini still mzigo bado uko chini, mikataba kama ilikuwa mibovu basi tutafute namna ya kuweka mikataba vizuri ili madini yatuokoe. Pia tuna kilimo, kwenye kilimo tunayo nafasi ya kusaidia Taifa hili. Tuwekeze kwenye kilimo, tuongeze bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nitaunga hoja pale ambapo Mheshimiwa Waziri atakuja na majibu mazuri na mpango unaoweza kumsaidia Mtanzania, nitamuunga mkono kama atasema vizuri, ahsante. (Makofi)