Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwanza kabisa, napenda kushukuru kwa kupata nafasi hii ya kutoa mchango wangu kwa hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ambayo imewasilishwa hii leo. Pili, napenda kuchukua nafasi hii kutoa pole kwa wananchi wenzangu wa Bagamoyo kutokana na mvua kubwa iliyonesha leo na kusababisha nyumba nyingi kuingia maji na watu wengi kupata karaha kidogo ya hapa na pale, nawapa pole sana.

Mheshimiwa Spika, nataka pia nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, bingwa number moja wa kufukuzia na kufuatilia uwekezaji katika nchi mbalimbali duniani na kuuleta hapa katika nchi yake. Tunampa pongezi sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kumpa pongezi Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo pamoja na Katibu Mkuu wake Bi. Tausi Kida na viongozi wote wa Wizara pamoja na Taasisi ambazo zipo chini ya Wizara yao kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Spika, niipongeze tena Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Uwekezaji wa viwanda Tanzania umekuwa mkubwa sana. Leo hii nashukuru katika Mkoa wetu wa Pwani kuna viwanda vingi sana, nafikiri ndiyo Mkoa ambao unaongoza kwa viwanda katika nchi hii. Ukianzia Kibaha – Mkuranga mpaka ukija Bagamoyo, kuna viwanda vingi vya kutosha, hii ni juhudi ya makusudi inayofanywa na Serikali pamoja na viongozi wetu wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nataka kuzungumzia masuala machache tu. Suala kubwa ambalo nataka kulizungumzia ni suala la EPZA. Mnakumbuka mnamo tarehe 13 Septemba, 2023 Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji baada tu ya kuchaguliwa siku siyo nyingi sana kwa makusudi kabisa alifunga safari kuja Bagamoyo. Alipokuja tulifanya kazi kubwa mbili:-

(i) Tulitembelea miundombinu iliyokuwa ikijengwa katika eneo ambalo linakusudiwa kujengwa viwanda; na

(ii) Tukaenda kufanya kazi moja ya kuzindua masterplan ya EPZA (Kongani ya Viwanda) ambayo kwa kipindi kile ilivyowasilishwa ilisema kwamba itagharimu shilingi trilioni 11, namshukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, katika ile kazi ambayo tulikwenda kuitembelea ya kukagua miundombinu ya Mradi wa EPZA, napenda kuchukua nafasi hii kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba, bado ile kazi inasuasua. Nimepitia hotuba yake na nimesoma hapa kwamba kilometa tatu za lami mpaka sasa hivi zimekwisha kwa 70% tu, 30% bado haijaisha. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri ile sehemu ni muhimu sana, wawekezaji hawawezi kuja wanapoona sehemu yoyote ambayo haina miundombinu. Tujitahidi, Ofisi yake ihakikishe kwamba ile miundombinu inamaliziwa ili wawekezaji waweze kuja na kuwekeza katika sekta hii ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nimetumwa na Wanabagamoyo ambalo hilo ni masikitiko yao makubwa sana na changamoto kubwa sana kwao na hasa wananchi wa Kata ya Zinga, ni kuhusu suala la fidia. Toka EPZA wachukue lile eneo sasa hivi ni mwaka wa 14 wananchi wanahangaika hawajui lini watalipwa fidia zao. Hata hivyo, nimepata faraja kidogo katika hotuba ya bajeti ya Waziri upande wa vipaumbele na kazi zitakazotekelezwa amelizungumzia kidogo suala la fidia. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, muda umekwenda sana miaka ni mingi, hawa watu wanateseka, maeneo yao yamepigwa pini, leo hii mtu hata akienda ardhi akitaka kuuza hata hekari moja, hawezi anaambiwa hili ni eneo la EPZA wakati yeye mpaka sasa hivi hajafaidika chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi hawa wa vitongoji mbalimbali, kuna Kitongoji cha Kibuba, Gongoni, Mikungalungo, Kokoto, Mkusangalakichwa, Mkunguni, Dagaza, Gwazo, Kondo, Gongoni, Chaponda, Bondeni na Changuruwe wana masikitiko makubwa, wanahitaji Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma, ikiwezekana bajeti ya mwaka huu wawafikirie angalau kupata chochote kwa sababu ni miaka 14 sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine katika huu mpango wa EPZA, kuna maeneo ambayo wenzetu wa EPZA wameyatoa katika mpango wao. Nafahamu ikiwemo Kijiji cha Mlingotini wamekiondoa katika mpango wao wa EPZA, kwa hiyo yale maeneo yatabakia. Naomba maeneo yote yale ambayo yatabakia, basi kwa wananchi wale iende ikaondolewe GN, ilimradi wananchi wale waweze kuyamiliki maeneo yao ili wafanye maendeleo yao wanayoyataka, kwa kweli hii itawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nigusie pia mpango wa Bandari ya Bagamoyo, kwa kweli hakuna kitu ambacho Serikali inakipoteza au inakwenda kukipoteza kama kutoharakisha ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Kwa kweli, bandari ile ikijengwa itasaidia sana kuondoa msongamano wa meli ambazo zinarundikana katika Bandari ya Dar es Salaam na kuiingizia faida nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, leo hii, kama unasafiri unakwenda Zanzibar meli zimejaa, zinakaa mwezi mzima hazijashusha mzigo, kwa nini, basi mpango wa kujenga Bandari ya Bagamoyo usiwasilishwe mapema sana. Tunamtegemea sana Mheshimiwa Waziri, yeye ni Profesa wa Mipango, ni Profesa wa Uchumi, ajaribu kuangalia mpango gani wa haraka ambao anaweza kuufanya kuhakikisha Bandari hii ya Bagamoyo inajengwa kwa haraka zaidi ili kupunguza msongamano wa meli pale Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kuchukua nafasi hii tena kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuisaidia nchi yetu katika mpango mzima wa uwekezaji. Mheshimiwa Rais, amejipambanua wazi katika kila sekta, katika Sekta ya Utalii, ameleta Royal Tour, katika sekta za viwanda anasafiri kila siku na wawekezaji wanakuja kwa hiyo, nimpe pongezi zake za pekee kabisa kwa kazi hiyo kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumwambia tena na tena Mheshimiwa Waziri kuhusu suala la fidia kwa Wanazinga. Ingekuwa ni kipindi ambacho Ofisi hii ameishika kwa muda mrefu ningeshika shilingi, miaka 14 ni mingi sana, lakini, kwa sababu Ofisi hii ameichukua juzi, hakuna sababu ya kufanya hivyo. Tutaenda mwakani kama Wanazinga, Wanamlingotini pamoja na hivi vitongoji nilivyovitaja, kama hakuna chochote kitakachofanyika basi kwa kweli itakapofika bajeti ya mwakani ataniona mbaya, nitakuja kukamata shilingi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)