Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kunipa nafasi hii ya kipekee ili niweze kuchangia katika Ofisi hii muhimu ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo ameanza kuifanya vizuri, nampa hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi ambazo amezifanya katika kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano, ameutekeleza vizuri sana. Tuna kila sababu ya kumpongeza, kwa sababu, tunaona kabisa kwa mfano sasa hivi Bwawa la Nyerere limeshaanza uzalishaji na tumepata faraja sana juzi tuliposikia sasa Tanzania umeme tunaozalisha ni mwingi kuliko mahitaji. Kwa kweli hiyo ni pongezi kubwa sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, mradi mwingine wa kielelezo, tulianza ujenzi wa SGR ambayo tumetumia muda mrefu kuujenga, lakini kipande cha Dar es Salaam mpaka Dodoma kimekamilika, ni faraja kubwa na ni pongezi kwa Mheshimiwa Rais. Jana treni hiyo imefanyiwa majaribio, imetumia masaa manne kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, ni faraja kubwa sana na ni maendeleo makubwa. Wale waliokuwemo kwenye hiyo treni jana wakikusimulia unatamani hata leo na wewe angalau uende, kwa kweli ni maendeleo makubwa ambayo tumeyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona mafanikio makubwa Rais amenunua ndege ya mizigo, tumenunua ndege za abiria ili kuchochea uchumi, hayo ni mafanikio makubwa. Zaidi ya hapo tumeona ujenzi wa majengo ya Ofisi hapa Makao Makuu Dodoma katika eneo la Mtumba, tunaona majengo yanaota kama uyoga kwa sababu ya kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais. Majengo yanapendeza, Mji wa Magufuli unapendeza, Dodoma imebadilika, ni kwa sababu ya kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, tumeona jinsi alivyofanya kwenye upande wa elimu, karibu majimbo yote madarasa yamejengwa ya shule za msingi, shule za sekondari na vyuo vinajengwa. Kwenye afya, hospitali zinajengwa, vituo vya afya na zahanati. Kwenye maji sijui tutumie maneno gani ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi, wakulima amewawekea ruzuku, ambayo imewasaidia sana wakulima kuweza kupata pembejeo. Pembejeo za kilimo ambazo zimesaidia sana upatikanaji wa chakula na malighafi kwenye viwanda vyetu. Kwa kweli, ni kazi nzuri ambayo tumeiona na wakulima wa nchi hii kama hawatatoa kura watakuwa watu wa ajabu, lakini, imani yangu watatoa kura kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu wamepata ruzuku na imewasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, tumeona jinsi alivyojenga meli na vivuko ambavyo vinajengwa. Tulienda kule Ziwa Victoria tukaona meli kubwa ambayo imeundwa hapa Tanzania, imezinduliwa na imeanza kufanyiwa majaribo. Meli ambayo huwezi kuamini kama kweli imeundwa hapa Tanzania, ni kazi kubwa ambayo wameifanya, tumeona vivuko mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo viwanja vya ndege vinajengwa kila mahali, tumeona kwenye Mhimili wa Mahakama kumejengwa jengo zuri na la kisasa hapa Dodoma ambalo linapendeza sana. Sidhani majengo kama yale kama yapo mahali pengine kama ambavyo linaonekana japo sijaingia ndani kwa nje tu kunaonesha jengo la Mahakama lilivyopendeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais hajaishia hapo na sisi hapa Bungeni amesema tupanue eneo, nimesikia kuna fununu tunaanza kutoa fidia kwa majirani hawa ili tupate eneo kubwa la Bunge na tuweze kufanya mambo mengine mengi. Kwa kweli, hiyo ni kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya, kwa hiyo, amefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mipango yetu na bajeti ya Mheshimiwa Waziri lazima itupelekee katika kukamilisha Dira yetu ya Miaka Mitano. Dira yetu ya mwaka 2025 ambayo inaenda kukamilika na tunakuja na dira nyingine mpya. Dira yetu inasema; “Tunahitaji maisha bora kwa kila Mtanzania,” kwa hiyo, hii Bajeti ya Mipango itupelekee namna ya kuboresha maisha ya Mtanzania. Sasa hivi maisha katika maeneo mengi wananchi wanalalamika lalamika, maisha hayajawa mazuri. Kwa hiyo, lazima kwa kweli Ofisi hii sasa ituambie namna maisha yatakavyoboreka, yatakavyokuwa mazuri, Watanzania watakavyoweza kufurahi. Vilevile tunataka Ofisi hii itupeleke mahali pa kutuambia namna tutakavyoweza kupambana na umaskini mkubwa katika maeneo mbalimbali. Umaskini tulionao huu ndiyo unaoifanya nchi yetu ambayo ni tajiri sana ionekane kama bado haina maendeleo, kwa hiyo, lazima itupeleke hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa tuko katika kipato cha kati cha chini, lazima twende kwenye kipato cha kati cha juu na hatimaye ndoto yetu itupeleke kuwa kwenye nchi za kipato cha kwanza au cha juu kabisa, kwa hiyo, lazima twende hivyo. Mipango yetu lazima pia ituambie tunaendaje kulinda amani na utulivu na umoja wa nchi yetu, lazima mipango itupeleke hapo na mipango hii itupeleke katika namna tutakavyoimarisha utawala bora kwa Watanzania, tutakavyojenga jamii iliyoelimika na tutakavyojenga uchumi wa ushindani. Haya yote kwa kweli nina imani kwa heshima kubwa, Profesa ataitendea kazi nchi hii na atayazingatia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kazi kubwa iliyofanyika kuna mambo tulipendekeza kama Bunge yamefanyiwa kazi na kuna mambo bado hayajafanyiwa kazi sawasawa. Tunaamini tunaendelea kupendekeza, kwa mfano, sasa hivi tija ni ndogo sana katika maeneo mengi, tija kwenye biashara, viwanda, kilimo na uzalishaji iko chini. Hii inatokana na kwamba hatuna taasisi inayosimamia tija katika nchi hii. Mheshimiwa Waziri, ifike mahali sasa waangalie uwezekano wa kuanzisha Shirika la Kuongeza Tija, Shirika la Tija lilikuwepo kule nyuma, lakini tulilifuta. Naamini tulikosea kulifuta kwa sababu tija ni muhimu sana ili nchi iweze kupiga hatua, kwa hiyo, nashauri kwamba hili ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, yapo mambo ambayo yanachukua fedha nyingi sana za nchi yetu, kwa mfano, ununuzi wa magari, magari yote tunayoyaona Tanzania yanatoka nje na yote tunatumia fedha za kigeni kutoka nje. Siamini kabisa kwamba toka tumepata uhuru mpaka leo Watanzania hatuwezi kutengeneza gari au hatuwezi kuunda magari au tukawa na viwanda vya kuunganisha magari. Kwa hiyo, mipango hii lazima itusababishie sasa ufike wakati kama tumeweza kuunda meli ya kisasa kule Mwanza, tumeweza kuunda vivuko vya kisasa, basi tuna uwezo wa kutengeneza magari hata madogo, magari ni muhimu. Kwa hiyo, nashauri Serikali waangalie uwezekano wa kuanzisha Kiwanda cha Kutengeneza Magari hapa Tanzania. Tumechoka sasa kuendesha magari ya mitumba, tunataka tuendeshe mapya yaliyotengenezwa hapa nchini na naamini tukiwa na dhamira ya kweli tutaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tulipendekeza kule Tunduma mizigo karibu 70% inapita pale, tukaomba kwamba paanzishwe Bandari Kavu ili mizigo isafirishwe na treni ya TAZARA kutoka Bandari ya Dar es Salaam mpaka pale, ikifika pale tukiwa na Bandari Kavu, wananchi wa kutoka Zimbabwe, kutoka Malawi, kutoka Kongo, kutoka Zambia waje wachukue mizigo pale. Tutakuwa tumerahisisha shughuli za biashara na tutaweza kupata mapato makubwa, lakini pia hata nchi itaweza kupata mapato zaidi.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, Songwe ni Mkoa wa mwisho, tunaita ni mkoa kitinda mimba kwa kuanzishwa hapa nchini. Sasa Mheshimiwa Waziri ifike mahali kwa sababu, tunataka kujenga jamii iliyoelimika, basi mipango hii itupeleke kuanzisha vyuo, matawi ya vyuo iwe vyuo vya kati au vyuo vikuu, tunahitaji vijengwe Songwe ili wananchi wa Mkoa wa Songwe waweze kupata elimu katika maeneo hayo, lakini si wananchi wa Songwe tu, tunataka na nchi jirani watuletee dola kwa kuja kusoma hapa. Vyuo vyote vilivyoko hapa tukivijenga vizuri, tukatoa elimu iliyo bora, wale watakuja kusoma hapa, tutapata dola. Tunaona Uingereza wanapata hela nyingi sana, Malaysia…

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, Malaysia na maeneo mengine wanapata hela nyingi sana.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Hasunga kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Condester Sichalwe.

TAARIFA

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naomba kumwongezea Taarifa Mheshimiwa Hasunga kwamba, kwa Mkoa wa Songwe, tunaomba waanze na kupandisha Chuo cha DIT kukifanya kiwe Chuo Kikuu ili kiwe chuo cha kwanza kwenye Mkoa wa Songwe.

SPIKA: Hebu nikuelewe kwanza mimi kabla sijamwuliza unayempa Taarifa?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, kule Mkoa wa Songwe kuna Chuo cha Dar es Salaam Institute of Technology ambacho kinatoa masomo kuanzia Certificate mpaka Diploma. Kwa kuwa, tunatamani Mkoa wa Songwe upate vyuo vikuu na hakuna chuo hata kimoja, tunaomba tuanze na hicho kipandishwe hadhi kiweze kutoa degree ili tuweze kupata hizo dola nyingi ambazo Mheshimiwa Hasunga anasema.

SPIKA: Naona huyu alipaswa apewe nafasi yake achangie kwa sababu, nadhani kitu anachoongea ni kitu tofauti. Kama kinaitwa Dar es Salaam Institute of Technology maana yake ndiyo tawi la Dar es Salaam Institute of Technology, sasa kama inabidi kiwe chuo kikuu maana yake kianzie kule ambapo ni chuo mama.

Mheshimiwa Hasunga.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa mchango wake, Mheshimiwa Mbunge wa Momba, ni mzuri na kweli tunahitaji tuwe na matawi ya vyuo vikuu katika eneo lile.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kupendekeza, kama muda utaruhusu, ni lazima katika mipango yetu twende tukaangalie namna taasisi zetu na mashirika ya umma yanavyofanya kazi. Sasa hivi zipo taasisi ambazo hazina faida, zimekuwa ni mzigo kwenye Serikali Kuu. Tufike mahali wafanye uchambuzi wa kina kuangalia kila shirika na umuhimu wake, faida zake na kwa nini liendelee kupata fedha kutoka Serikali Kuu. Hilo ni muhimu na litaipunguzia Serikali matumizi ambayo sio ya lazima. Sasa hivi kila mtu anapata hela kutoka Hazina, hafanyi kazi sawasawa, kwa hiyo, baadhi ya taasisi zirekebishwe, naamini hilo litatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni kwa nusu dakika, naomba mipango yetu ituoneshe namna tunavyoenda kuimarisha sekta binafsi. Bila kuimarisha sekta binafsi, bila kuiwezesha, bila kuchochea uwekezaji kwenye sekta binafsi, bado mzigo utakuwa kwenye Serikali Kuu katika kubeba majukumu mbalimbali. Haya majukumu yanaweza kufanywa na sekta binafsi vizuri iwapo Serikali itahamasisha na itailinda na kuchochea sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)