Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia bajeti hii ya Uwekezaji, lakini kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa za kutengeneza ustawi wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaase wasaidizi wake kwenda na kasi yake, ni vyema wakajibidisha kumwelewa, kufahamu matamanio yake, maono yake na matokeo anayoyatarajia. Kwa jitihada zake binafsi amepandisha idadi ya watu/makampuni yenye nia ya kuwekeza na hivyo kufanya TIC kusajili wenye nia ya kuwekeza kufikia 1,282 kwa muda wa miaka mitatu pekee. Kama wenye nia hawa hawa wote wangefanikiwa kuwekeza wangeingiza kiasi cha mitaji cha Dola za Marekani bilioni 15, sawa na shilingi trilioni 36 za Kitanzania.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kwa miaka 23 toka mwaka 1996 hadi sasa TIC iliweza kusajili jumla ya wawekezaji 12,381 ambao wangeweza kuingizia mtaji wa dola bilioni 117 sawa na shilingi trilioni 281. Kama angalau nusu ya wawekezaji hao wangewekeza, wangeweza kuchangia mitaji ya dola bilioni 59, sawa na shilingi trilioni 140 za Kitanzania.
Mheshimiwa Spika, hapa naeleweka ninakoelekea, maana yangu ni kwamba wawekezaji wanakuja na dola, hivyo tungekuwa na dollar reserve ya kutosha na haya malalamiko ya dola yasingekuwepo; shillingi yetu ingeimarika sana dhidi ya dola na pia multiplier effects ya mitaji hii mikubwa ingeonekana kila pahali (sekta) na kuwa na uchumi imara, kwa mfano kila shilingi moja inaongeza shilingi tano kwenye mzunguko wa matumizi (one shilling creates five shillings spending) hivyo uwekezaji wa mitaji ya shilingi trilioni 140 ingetengeneza shilingi trilioni 700 kwenye mzunguko wa matumizi.
Mheshimiwa Spika, kwa uoni wangu jitihada hizi kubwa za Mheshimiwa Rais zimekuwa zikikwamishwa na watendaji wasioelewa tafsiri sahihi ya maono ya Mheshimiwa Rais kisha kutafsiri maono hayo kwa vitendo na mara nyingi ni zao la uvivu, uzembe wa kutowajibika.
Mheshimiwa Spika, ubora wa mambo utaonekana kwenye matokeo, mipango yetu ya mwaka, miaka mitano, kumi na kadhalika haioneshi matokeo chanya na tafsiri yake ni kwamba watekelezaji hawaimbi wimbo mmoja na wapangaji.
Mheshimiwa Spika, naomba ieleweke kwamba mipango imekuwepo muda wote, either ikisimamiwa na Wizara ama ikisimamiwa na Tume, hivyo Tume ya Mipango sio jambo jipya kwani kuwa na matarajio mazuri kwa kigezo tu cha kubadilisha utaratibu wa nani asimamie mipango bila kubadilisha mindsets zetu huko ni kujidanganya, yatubidi sote wapangaji na watekelezaji tubadilishe mitazamo yetu ya jinsi ya kuwajibika. Kama tabia yetu ya kutofuatilia mipango yetu itaendelea, basi hakuna kitakachobadilika.