Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Hotuba hii muhimu ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji katika mwaka huu wa fedha 2024/2025. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametujalia kukutana siku ya leo kujadili bajeti hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye hasa analifanya Taifa hili kuwa kipaumbele katika uwekezaji na kwa mipango mizuri ambayo inaliletea Taifa uchumi unaokua kwa kasi zaidi. Pia, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa sababu, ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo yote haya yanafanyika kwa umoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana vilevile Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango, Makamu wa Rais, Waziri wetu Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko. Nachukua nafasi hii pia, kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Kitila Mkumbo, ambaye kwa kweli anafanya kazi kubwa sana na ndiyo leo tunajadili bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe Spika wetu pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge lako Tukufu kwa jinsi ambavyo ameendelea kutuongoza vizuri katika kujadili Bajeti za Serikali na leo hii katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Pia naipongeza Kamati kwa kazi kubwa iliyofanya pamoja na Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika maeneo mengi kwenye bajeti hii. (Makofi)

Maheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapa pole Watanzania wenzangu katika maeneo mbalimbali ambako kumetokea changamoto ya mafuriko kutokana na mvua hii ya El-Nino, lakini pia najua kuna changamoto kubwa katika miundombinu. Nachukua nafasi hii pia, kuwashukuru wananchi wenzangu wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa vile ambavyo wanaendelea kuniunga mkono na kuhakikisha natimiza wajibu wangu kama Naibu Waziri katika Wizara ya Viwanda na Biashara katika Serikali hii ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua changamoto zilizopo maeneo mengi Tanzania, pamoja na kule jimboni kwangu, zipo barabara nyingi zimeharibika katika kata zote 11. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, niishukuru Serikali yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana na kule kwangu kuna fedha ambazo zimeenda kwa ajili ya kutengeneza maeneo haya ambayo yana changamoto ya dharura kwenye miundombinu ya barabara. Sisi kama Wanamufindi Kaskazini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie kidogo katika bajeti hii muhimu. Moja ya maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana ni namna ambavyo Serikali imejipanga kuhakikisha Sekta ya Biashara Ndogo na Viwanda Vidogo (SMEs) inapewa kipaumbele katika mipango ya Serikali kwenye uwekezaji na kuwapa vivutio maalum.

Mheshimiwa Spika, takwimu zinasema kwamba zaidi ya 95% ya biashara zote hapa Tanzania ziko kwenye sekta hii ndogo na ndogo sana. Pia 35% ya GDP ya Tanzania inatokana na sekta hii ndogo na ndogo sana na ya kati. Zaidi, katika sekta hii kwa maana ya SME zaidi ya 54.3% imeajiri wanawake. Kwa hiyo, maana yake ndio wanaofanya kazi kubwa sana katika mchango huu kwenye pato la Taifa na shughuli nyingi ambazo wanawake wanafanya zinahusisha shughuli za kilimo na uongezaji thamani katika mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimesema haya ili tuone umuhimu wake kwamba Serikali tunachukulia sana umuhimu wa SMEs, tukianza sisi Wizara ya Viwanda na Biashara tunayo sera mahususi inayoangalia SMEs. Kwa sababu ya umuhimu wa sera hii ya mwaka 2003, kwa hiyo tunaenda kuihuisha ili iweze kuchukua uhalisia wa sasa na mahitaji kamili ya SMEs kulingana na wakati huu. Pia ndiyo maana SMEs iko katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambao nao wanaangalia wajasiriamali kwa namna ya pekee ili kuhakikisha wanafaidika na vivutio vyote ambavyo vinatolewa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hivyo tu, lakini Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu pia wamechukua sera hii na wanaifanyia kazi na ndiyo maana huko kuna peer startups ambayo tunaangalia wale wajasiriamali wadogo (SMEs wadogo) wanaoanza biashara basi wanaweza kupewa mitaji na elimu. Katika eneo hili tumeangalia zaidi kwenye value addition, kuongeza thamani na hasa mazao yanayotokana na sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya uratibu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji tumeona ni lazima tuhakikishe tunaendelea kuweka vipaumbele. Moja, kuendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali kupitia NEDF, Mfuko huu ambao unasimamiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO), ambapo huko kuna wajasiriamali wadogo wanaatamiwa (incubation) ili waweze kukua katika kujenga viwanda vidogo vidogo lakini pia kufanya biashara.

Mheshimiwa Spika, kupitia Chuo chetu cha Elimu cha Biashara (CBE), nako pia kuna uatamizi wa uanzishaji biashara mbalimbali ili kuhakikisha tunawasaidia SMEs. Katika maeneo haya Wizara imeweka mpango mahsusi wa kuanza kujenga mitaa ya viwanda (Industrial Parks) katika halmashauri. Pia tutaenda mpaka ngazi za kata ili kuhakikisha kunakuwa na maeneo mahususi ya uzalishaji, kwa sababu changamoto mojawapo tuliyonayo kama ambavyo wachangiaji wengine (Wabunge) kwamba tunazalisha bidhaa ambazo sasa tunaenda kushindana katika Eneo Huru la Biashara la Africa (AfCFTA). Maana yake ni lazima tuzalishe bidhaa zenye ubora ili tushindane katika soko hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi kama Wizara kwanza tunaandaa maeneo hayo, lakini pia kujenga majengo ambapo humo tutaweka mitambo mbalimbali. Moja ya mitambo ambayo tunaibuni sasa hivi ni sugar min plant kwa maana ya viwanda vidogo vya kuchakata miwa ili kuzalisha sukari kwa ajili ya matumizi ya ndani, lakini kwa ajili ya kuuza katika masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na michango kwenye eneo la viwanda vilivyobinafsishwa. Serikali chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imeendelea kuratibu; na sisi kama Wizara ya Viwanda tumeendelea kuhakikisha kwamba viwanda vyote ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa na wale waliouziwa wameshindwa kuviendeleza hatua mbalimbali tayari zinakwenda kuchukuliwa, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema katika hotuba yake.

Mheshimiwa Spika, wale ambao walishindwa katika viwanda ambavyo vimerudishwa Serikalini; moja, tumesema tunaendelea kujadiliana nao ili wale ambao wana uwezo au wanataka kuviendeleza na tayari kuna kampuni kama nne ambazo viwanda vyao vimerudishwa Serikali, lakini wamesema wako tayari kuviendeleza, tunajadiliana nao ili tukiingia mikataba waweze kutekeleza kama ambavyo tutakuwa tumekubaliana ili viwanda hivyo vifufuliwe.

Mheshimiwa Spika, pili, tunaendelea kuwasaidia wale ambao hatujafikia muafaka wa kuvirudisha Serikalini tuwape elimu na ujuzi wa namna ya kuviendeleza viwanda hivyo. Mheshimiwa Ulenge ametoa mfano Kiwanda cha Unga wa Ngano cha Pembe pale Tanga, ni moja kati ya viwanda ambavyo tunashauriana na wawekezaji. Moja, kuwapa namna ya kuendeleza biashara zao, lakini pia kama kuna changamoto ya mitaji Serikali iweze kuona namna ya kuwasaidia ili waendelee kuzalisha ili viwanda hivi vyote viweze kufanya kazi kama ambavyo vilikuwa vimekusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na maeneo mengi ya namna gani tunaendelea kusaidia wawekezaji wa ndani ili waweze kufanya vizuri na kusiwe na ile hisia kwamba tunapendelea au tunatoa vivutio kwa wawekezaji wa nje. Moja, katika Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 2022 ambayo Bunge lako Tukufu liliipitisha, imeangalia viwango ambavyo mwekezaji wa ndani akikidhi anapata vivutio na hii tulipunguza mtaji kutoka Dola za Kimarekani 100,000 mpaka 50,000. Hii ina maana sasa Mtanzania anaweza kuwekeza kwa mtaji huo na akapata vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ili aendelee kuzalisha kwa tija.

Mheshimiwa Spika, pili, pia tunaendelea kutekeleza mpango ule wa MKUMBI (Blueprint) ambao nao umetekeleza mambo mengi ikiwemo kuondoa tozo na kodi kero ambazo wafanyabiashara wengi na wawekezaji walikuwa wanakumbana nazo. Kwa hiyo, tunaendelea kuboresha hilo.

Mheshimiwa Spika, katika Mpango Mkakati wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, tumeshaanza kuweka lile dirisha la pamoja la kuhudumia wawekezaji ili kurahisisha kupunguza ule ukiritimba au urasimu usio wa lazima kwa wawekezaji; kuhakikisha kwamba wanapata huduma kwa haraka katika sehemu moja.

Mheshimiwa Spika, taarifa tu, katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024, jumla ya miradi 295 kati ya miradi hiyo 509 yote ilisajiliwa na Kituo chetu cha Uwekezaji na miradi hii inamilikiwa na Watanzania. Kwa hiyo, utaona kwamba Watanzania tayari wanafaidika na vivutio hivi ambavyo Serikali inavitoa kwa wawekezaji bila kuangalia kwamba ni wa ndani au wa nje ambao ni zaidi ya 58% ya Watanzania ambao wamesajiliwa katika miradi hii.

Mheshimiwa Spika, usajili wa miradi katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika Mamlaka yetu ya Uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha kwa mauzo nje; EPZA imeweza kusajili jumla ya miradi ya viwanda 25. Aidha, jumla ya miradi 206 ambayo imesajiliwa kupitia EPZA tangu mwaka 2006 ilipoanzishwa miradi hii imelenga zaidi katika viwanda vya kuongeza thamani na hasa kwenye sekta ya pamba, nguo na mavazi, lakini pia kwenye kuchenjua madini.

Mheshimiwa Spika, kati ya miradi 509 iliyosajiliwa na TIC sekta zilizoongoza kwa usajili wa miradi hiyo ni uzalishaji wa miradi viwandani kwa maana ya miradi 221 ambayo ni sawa na 43% ambayo inatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 28,445 na wameweza kuwekeza zaidi ya mtaji wa Dola za Kimarekani milioni 1,501. Kwa hiyo, hii ni mikakati ambayo inatekelezwa kwa uratibu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kupitia Wizara ya Viwanda na Wizara nyingine.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuchangia katika maeneo machache ambayo pia yaliongelewa kuhusiana na miradi ya kimkakati, imeongelewa kuhusiana na Mradi wa Magadi Soda Engaruka pia Mradi wa ule wa Liganga na Mchuchuma. Serikali inafanya jitihada za makusudi na hasa Awamu hii ya Sita kuhakikisha miradi hii ya kimkakati na kihistoria inaenda kukwamuka na ndiyo maana tayari fidia imeshaanza kulipwa katika maeneo haya. Tukianza kule Liganga na Mchuchuma lakini baadaye sasa tunaenda kulipa fidia katika eneo la Magadi Soda ili miradi hii yote iweze kutekelezwa kadri ambavyo Watanzania wengi wangependa.

Mheshimiwa Spika, kuliongelewa kuhusiana na Sekta ya Madini hasa kwenye chumvi na Mheshimiwa Dkt. Chaya pale Manyoni Mashariki; tunalifanyia kazi na Serikali imeshasema makusudi, chumvi ni bidhaa muhimu. Kwa hiyo, tutaangalia maeneo yote ambayo yana uzalishaji wa chumvi ili tuhakikishe chumvi hiyo inazalishwa hapa Tanzania, tutumie sisi Watanzania pia tuweze kuuza nje ya nchi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba tutahakikisha miradi ya kimkakati kwenye bidhaa muhimu ambazo kama Watanzania lakini pia soko linahitaji tutazalisha kwa weledi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niseme naunga mkono hoja bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Ahsante sana. (Makofi)