Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kukushukuru wewe kwa jinsi ambavyo umeendesha mjadala huu vizuri kama kawaida yako. Nimshukuru sana Mheshimiwa Exaud Silaoneka Kigahe kwa kunipa company kwa kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Kigahe tumefanya naye kazi kwa muda mrefu, ni Naibu Waziri mahiri, ni Mbunge mahiri sana na nitumie nafasi hii kwa kweli kuwaambia wananchi wa Mufindi Kaskazini wanalo jembe walishikilie vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia kuendelea kuwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa uchambuzi wao na taarifa yao makini ambayo ilisomwa hapa na mwanamama mahiri sana, Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum. Tunawashukuru sana kwa kuunga mkono hoja na wametoa hoja nyingi, naomba nijibu mbili tu kwa upande wa Kamati.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni suala la Dira ya Maendeleo; walishauri kwamba izingatie mabadiliko yanayoendelea duniani, lakini pia mfumo wa kiutawala. Tumepokea ushauri huo na tutauzingatia. Sasa hivi zoezi ambalo linaendelea katika upande wa dira ni zoezi la kukusanya maoni, kwa hivyo haya maoni ambayo yanatolewa na Kamati na mengine yatazingatiwa na timu ya wataalam.
Mheshimiwa Spika, Kamati vilevile ilishauri na kusisitiza kwamba Serikali ihimize matumizi ya Mfumo wa Miradi (National Project Management Information System). Niseme tu kwamba kwa mujibu wa Waraka Na.5 wa Hazina umesisitiza kwamba miradi yote ya Kitaifa lazima ipitie katika mfumo huu na isipopitia katika mfumo huu Tume ya Mipango haiwezi kuifikiria. Kwa hiyo, niwakumbushe watekelezaji wa miradi yote wakumbuke kuingiza miradi yote kupitia mfumo huu kwa sababu ndiyo utaratibu ambao tumekubaliana na ni utaratibu wa kisheria ambao pia umeidhinishwa na Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba uniruhusu nipitie baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, tumepata michango ya Waheshimiwa Wabunge 17 ambao wamezungumza moja kwa moja na Mheshimiwa Mbunge mmoja amechangia kwa njia ya maandishi. Niseme tu kwamba sisi kama Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji tumewasikia Waheshimiwa Wabunge na tutazingatia maoni na ushauri wao ambao kimsingi ni ushauri wa Watanzania kupitia sauti zao.
Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yamechangiwa ni matatu makubwa. Tunalo eneo la jumla la mipango, tunalo eneo la uwekezaji na uendeshaji wa mashirika ya umma. Nitataka nigusie baadhi ya maeneo haya kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kwanza kwa upande wa mipango hoja zimetolewa nyingi, lakini ni hoja tano. Hoja ya kwanza; mkakati wa kuandaa rasilimali watu ni muhimu sana uzingatie mahitaji yetu na Mheshimiwa Rashid Shangazi alitoa mfano, kwamba vyuo vingi kwa sasa vinatoa mafunzo ya ualimu wakati walimu wamejaa mtaani bila kazi. Ni hoja ya msingi na ndio maana katika mpango niliowasilisha moja ya jukumu na kipaumbele cha Tume ya Mipango kwa mwaka huu unaokuja ni kufanya tathmini ya rasilimali watu ili kubaini mahitaji halisi ya rasilimali watu na ujuzi unaohitajika kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, hilo ni jambo la msingi sana kwa sababu tunapoenda mbele suala la rasilimali watu ni suala ambalo lipo katikati ya mipango. Bila kuwa na rasilimali watu ambayo imepangwa vizuri na ujuzi unaoeleweka na unaohitajika mipango yetu haiwezi kufanikiwa. Kwa hiyo, ukisoma majukumu 20 ya Tume ya Mipango jukumu lao la kwanza ni kufanya tathmini ya rasilimali ikiwemo rasilimali watu na mwaka huu ujao wa fedha hilo jukumu watalifanya ili tupate picha halisi ya mahitaji yetu na hili litazingatiwa vizuri sana katika Dira yetu ya Maendeleo ambayo inakuja. Kwa hiyo, hilo tumelichukua hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni maendeleo vijijini, hili Waheshimiwa Wabunge wamelitolea maoni. Kwa mujibu wa taarifa ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 takwimu muhimu sana zipo nyingi, lakini takwimu mbili za kuzingatia; moja, 65% kama alivyosema Mheshimiwa Kamani, ya Watanzania wanaishi vijijini. Kwa hivyo, huwezi kuzungumzia maendeleo ya nchi hii bila kuwa na focus katika maendeleo vijijini kwa sababu ndiko Watanzania walio wengi wako huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, takwimu ya pili ni ile aliyoisema Mheshimiwa Ngw’asi kwamba 76% ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 35 na kuna mtu mmoja hapa amesema, mimi ni kijana. Nilishapita siku nyingi huko, mimi kwa sasa sipo kwenye ujana, sisi ni wazee wa nchi hii. Kwa hivyo, 76% wapo chini ya miaka 35 na ukienda zaidi 42.8% wapo chini ya miaka 15. Tunasema nini? Tunasema kwamba kimsingi idadi kubwa ya watu wa nchi hii ni watoto na vijana. Kwa hiyo, huwezi kuzungumzia maendeleo yoyote ya maana bila kugusa makundi hayo mawili. Moja, vijijini na pili, vijana na watoto. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mipango yetu iliyopo na mipango ijayo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa tutazingatia sana makundi haya ili kuhakikisha kwamba uchumi wetu unapokua uwe ni uchumi jumuishi, ulenge maeneo ambayo watu wengi wapo. Ndiyo maana kwa kuzingatia hilo, Mheshimiwa Rais ameipa kipaumbele sekta ya kilimo kwa sababu ndiyo ambayo inaajiri watu wengi zaidi ya 65%. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuendelee kusisitiza na kuwekeza sana katika maeneo ambayo yanagusa watu wetu wengi ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi na kadhalika. Pia tuendelee kusisitiza kwamba lazima tu-pay attention ya kipekee kwa watoto na vijana kwa sababu ndiyo usalama wa Taifa kwa sasa na miaka mingi ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wametoa ushauri kwamba kuna haja ya kuanzisha taasisi maalum inayoshughulikia maendeleo vijijini. Ni wazo zuri, lakini niseme tu kwamba tayari tuna taasisi ambazo zipo dedicated kwa maendeleo vijijini. Kwa mfano REA, REA ni taasisi maalum kwa ajili ya maendeleo ya nishati kwa maana ya umeme vijijini na inafanya kazi nzuri na ndiyo maana tangu ianzishwe tunazungumzia hapa karibu 90% ya vijiji vinaunganishwa kwenye umeme.
Mheshimiwa Spika, tunayo TARURA ambayo imekabidhiwa jukumu la kushughulikia barabara za vijijini, tunayo RUWASA ambayo Bunge hili mwaka 2018 ilitunga Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Maendeleo ya Maji Vijijini (RUWASA), tangu ianzishwe Sekta ya Maji Vijijini inakwenda kwa kasi, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge tayari tuna mfumo wa kitaasisi kwa lengo la kushughulikia baadhi ya maeneo kwa maendeleo vijijini.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ina-pay attention kubwa sana kwenye maendeleo vijijini kupitia sekta mbalimbali, ndiyo maana tunatoa ruzuku ya mbolea vijijini ili wakulima wetu waweze kulima bila vikwazo vikubwa. Kwa hiyo, hili ni eneo kubwa ambalo tumeliangalia.
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia umuhimu wa kufungamanisha sekta za maendeleo, wametoa mfano wa matumizi ya rasilimali za maji kwamba mradi wa Lake Victoria kwa mfano, haiwezekani mradi mkubwa kama ule ukaishia kuwa tu mradi wa maji ya kunywa, haiwezekani! Sisi kama Serikali Mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo na tumekubaliana kuwa Mradi wa Maji unaotoka Lake Victoria kuja Dodoma, lazima ndani yake uwe na dedicated lines kwa ajili ya umwagiliaji ili Mikoa ya Shinyanga, Tabora, Singida na Dodoma, ambako mradi huu utapita wananchi wasipate maji ya kunywa tu, bali lakini watumie maji hayo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais na mradi umeshapitishwa, tayari watalaam wanaendelea na upembuzi yakinifu na naamini Mheshimiwa Waziri wa Maji wakati wa bajeti yake ataueleza kwa kina.
Mheshimiwa Spika, tumeshakubaliana tulipoanzisha National Water Grid (Gridi ya Maji ya Taifa), lengo ni kutumia rasilimali za maji kubwa kwa maana ya Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, maji haya ambayo Mungu ametujalia, tuyatumie kwa lengo la uzalishaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo. Kwa hiyo, hili ndilo lengo kubwa ambalo tunakwenda nalo, Waheshimiwa Wabunge maoni yenu yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, mawazo yake mazuri yamezingatiwa, kama alivyosema mate wangu, haya mawazo yake mazuri yamezingatiwa na litafanyiwa kazi jambo hili.
Mheshimiwa Spika, suala la nne lilikuwa ni suala la mipango ya Kitaifa vis-a-vis mipango ya kisekta. Mheshimiwa Kunambi aliongea vizuri kwamba ni lazima tuwe na dira moja, akaeleza kwamba tuna dira nyingi za kisekta, dira ya kitaifa. Kimsingi kwa jina lolote ambalo utaita na wala sihitaji kuwa na wivu unaogawanyika kwa sababu Serikali inafanya kazi kama kitu kimoja, Dira ya Taifa ni moja na mipango yote ya Taifa, sera zote za kisekta lazima ziakisi Dira ya Taifa ya Maendeleo na ndivyo itakavyokuwa.
Mheshimiwa Spika, hii dira ambayo tunaiandaa hatimaye sera zote na hivyo ambavyo Mheshimiwa Kunambi ameviita vi-vision vidogo vidogo itabidi lazima viakisi Dira ya Taifa ya Maendeleo, hili halina shaka kwa sababu hatimaye Dira ya Taifa ya Maendeleo inasimamiwa na Tume ya Mipango.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango kwa muundo wake Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndivyo sheria inavyosema na anao wajumbe wengine wanne pia Mawaziri wanaohusika na Mipango na Fedha ni wajumbe. Kwa hivyo, hii ni Tume kubwa na jambo likitoka pale huwa limepikwa vya kutosha, kwa hiyo msiwe na wasiwasi kwamba kutakuwa na mkanganyiko wa mipango ya kitaifa na mipango ya kisekta. Haiwezekani kwa sababu mipango ya kitaifa inaanzia kwenye mipango ya kisekta ndiyo inafika juu. Ndiyo maana hapa sekta zitawasilisha mipango yake yote na nitakuja kusoma Mpango wa Taifa tarehe 13 Juni, ambao utaunganisha mipango yote hiyo ili kupata mpango wa Kitaifa. Kwa hiyo, hapawezi kuwa na mgongano wa mipango ya kisekta na mpango wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, eneo la tano nimeshalisema, Waheshimiwa Wabunge wamesisitiza na Mheshimiwa Charles Kimei ameongea vizuri kwamba mfumo wa ufuatiliaji wa miradi ya kitaifa, ni muhimu sana tuwe na mfumo. Mheshimiwa Mbunge mfumo upo, tunao na unafanya kazi unaitwa National Project Management Information System (NPMIS) na kwamba sekta zote ambazo zinatekeleza miradi ni lazima zizingatie mfumo huu. Kwa hiyo, hilo lilikuwa ni eneo la kwanza la mipango.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni uwekezaji. Hapa Waheshimiwa Wabunge wametoa maoni mengi katika maeneo matano. Kwanza, ni juu ya Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma. Waheshimiwa Wabunge, waliochangia akiwemo Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya PIC wamesema, Muswada huu uje na ameainisha maeneo pale.
Mheshimiwa Spika, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Muswada huu ulishasomwa kwa mara ya kwanza, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, Serikali iliona kuna maeneo ambayo inahitaji kuyafanyia kazi zaidi na tumeshayafanyia kazi, taratibu zinaendelea kukamilika ili tuweze kumwomba Spika aruhusu ule Muswada usomwe kwa mara ya pili. Niwahakikishie kwamba, Muswada huu bado upo na Serikali haijauondoa.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili lilikuwa ni suala la fursa za uwekezaji hususani uwekezaji kwa wazawa na hasa wawekezaji wadogo. Nitoe tu taarifa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanafahamu, mwaka huu tuliwaagiza TIC na hata nilipoteuliwa mwaka jana, moja ya swali langu kubwa kwa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) ilikuwa ni kwamba, huko nje TIC inaonekana ni chombo cha wawekezaji kutoka nje, lazima mbadilishe mindset ili hiki chombo kionekane kwamba ni chombo cha wawekezaji wa Tanzania primarily na watu wa nje secondarily.
Mheshimiwa Spika, wamefanya hivyo tukaanzisha kampeni kubwa ya kuhamasisha wawekezaji wa ndani, vijana hawa wa TIC wamefanya kazi nzuri wamezunguka nchi nzima kuhamasisha jambo hili, kwa kweli niseme Watanzania wengi ambao wamefikiwa wamefurahi sana.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka kuna mwekezaji mmoja pale Geita ana hoteli kadhaa, alikuwa hajui faida za kujiunga na TIC kusajili mradi wake, tangu asajili anafurahia sana na amekuwa ni ambassador mkubwa sana wa TIC. Kwa hivyo, tutaendelea kuwasukuma vijana hawa wa TIC ili kuhakikisha kwamba wanawafikia Watanzania popote walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili katika hilo, TIC wameanzisha utaratibu mzuri kwamba, kama una eneo, una ardhi yako wanakuunganisha na wawekezaji, kwa sababu kuna Watanzania wengi ambao wana ardhi wamekaa nazo, wangeweza kutengeneza pesa. Kwa hivyo TIC wameanzisha utaratibu mzuri sana kama una ardhi yako unawataarifu TIC na wanakuunganisha na wawekezaji, kisha unaingia ubia na wawekezaji wa nje, wewe una ardhi unapata mtaji na unaanza kutengeneza fedha.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Watanzania wenye ardhi tafadhali wawasilishe ardhi zao kwa TIC, watawaunganisha na wawekezaji mbalimbali ili hiyo ardhi ibadilike kuwa mali waanze kutengeneza fedha na kujenga uchumi wao na uchumi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni suala la miundombinu. Tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge na tutayazingatia. Katika kuzunguka kwangu kote na Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria walijionea tulipozunguka pamoja, changamoto kubwa sana kwa upande wa uwekezaji hasa kwenye viwanda ilikuwa ni suala la nishati, umeme ulikuwa hautoshi, tunashukuru kwa usimamizi mzuri na uongozi wa Mheshimiwa Rais na Waziri wetu wa Nishati ambaye ni Naibu Waziri Mkuu, hatimaye Mradi huu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere umekamilika na umeanza kuzalisha umeme. Kwa hivyo, hii changamoto ya umeme kwa viwanda inaenda kuwa historia na kwa miradi ya umeme ambayo ipo kama ambavyo Waziri wa Nishati ataeleza kwenye hotuba yake, changamoto ya nishati kwa viwanda inaenda kuisha na wawekezaji wengi watakaa vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la maji viwanda vingi kwa kweli wanashukuru kwamba wanapata maji na kuna mfumo mzuri sana wa kuunganisha kwenye maji na suala la miundombinu linaendelea kufanyiwa kazi, hayo yote tumeyapokea.
Mheshimiwa Spika, suala la nne, ilikuwa ni vivutio. Ni kweli tulikuwa na changamoto ya vivutio kwa wawekezaji wanaoitwa wawekezaji wa kimkakati. Wapo wawekezaji 16 ambao walikuwa wameomba vivutio 60 tangu mwaka 2018. Walikuwa wamekwama kwa sababu kulikuwa na mgongano kati ya Sheria yetu ya Uwekezaji na Sheria mbalimbali za Kodi. Sheria ya Uwekezaji inatoa unafuu wa hivyo vivutio, lakini Sheria za Kodi zilikuwa zimekwama.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako, Bunge limefanya marekebisho kadhaa kwenye Sheria yenyewe ya Uwekezaji na kwenye Sheria Mbalimbali za Kodi, tangu mwaka 2022 sasa kupitia NISC (National Investment Steering Committee) ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Waziri Mkuu, vivutio vimeshaanza kutoka. Kati ya vivutio 64 ambavyo vilikuwa vimekwama vivutio 58 vimeshatoka vimebaki sita peke yake na hivi vipo katika taratibu mbalimbali za kupewa GN ili vitoke. Kwa hiyo, hii changamoto nayo inashughulikiwa na tunaamini kwamba inaenda kuisha.
Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho katika hili ilikuwa ni Mradi wa Bagamoyo. Mheshimiwa Muharami Mkenge ameongea kwa uchungu katika eneo hili anafahamu tulishafika, nawataarifu wananchi wa Jimbo la Bagamoyo kwamba, kwanza Mbunge wenu katika jambo ambalo halali nalo ni suala hili la Mradi wa Bagamoyo, anawapigania wananchi wake wapate fidia na pili, wapate maeneo yao ili waweze kuwekeza. Kwa hivyo wananchi wa Bagamoyo wana Mbunge imara sana ambaye kwa kweli analipigania sana suala hili na hoja zake zote tutazizingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekwishakamilisha mpango kabambe wa mradi huu na utaidhinishwa. Mradi huu una maeneo mawili ambayo ni ujenzi wa bandari kubwa na ujenzi wa viwanda. Mradi mzima utagharimu takribani shilingi trilioni 11, ni mradi mkubwa wa kitaifa, ni moja ya miradi 17 ya kielelezo na haki zote za wananchi wa Bagamoyo zitazingatiwa kikamilifu ikiwemo kulipwa fidia zao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge suala hili asiwe na shaka nalo, mimi nimeshafika pale, anafahamu tulikuwa pamoja na wananchi wake, niwahakikishie kwamba, anawapigania vizuri na Serikali yao sikivu ya Chama Cha Mapinduzi imesikia kilio chako na itakizingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu na la mwisho ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelitolea maoni ni eneo la mashirika ya umma. Hoja kubwa hapa ni mbili. Hoja ya kwanza inahusu kufutwa na kuunganishwa kwa mashirika ya umma. Tumepokea maoni ya Mheshimiwa Luhaga Mpina, ameandika vizuri na ametoa hoja za msingi ambazo Serikali tutazifanyia kazi na nyingine nitazijibu hapa.
Mheshimiwa Spika, hoja ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitoa ni mbili, kwanza, vigezo ambavyo vinazingatiwa katika kuunganisha ama kufuta mashirika haya ya umma. Msingi mkubwa wa uamuzi huu ambao Mheshimiwa Rais aliueleza hapa Bungeni na katika hotuba zake mbalimbali na hatimaye akatupatia maelekezo wasaidizi wake, moja ni kuipunguzia Serikali mzigo.
Mheshimiwa Spika, mashirika haya ya umma yanakusanya takribani shilingi trilioni 1.07, lakini mashirikika haya ya umma ukifanya hesabu yanakula fedha za Serikali ikiwemo mishahara na matumizi mengine takribani trilioni tatu. Kwa hiyo, katika hali ya kawaida na kwa kiongozi yeyote makini ni lazima hili eneo aliangalie. Ni lazima alifanyiwe reform ili hatimaye mashirika haya mosi, yaendeshwe kwa ufanisi na pili yachangie kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwa hiyo, ilikuwa ni lazima tufanye tathmini na mapitio ya mashirika ya umma.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Wataalamu ya Kitaifa ikihusisha sekta mbalimbali walifanya utafiti na uchambuzi mpana na hatimaye wakabainisha kuwa mashirika 16 ambayo ilikuwa ni muhimu yaunganishwe na mashirika manne yafutwe. Mchakato huu unaendelea, tutafanya uchambuzi wa mashirika yaliyobaki na tutaendelea nayo.
Mheshimiwa Spika, sasa tunazingatia mambo gani? Moja, tunaangalia yale mashirika ambayo majukumu yao yanaingiliana, yanaunganishwa. Yale mashirika ambayo majukumu yao yamepitwa na wakati, kwa sababu tusisahau kwamba mashirika mengi haya yalianzishwa kipindi ambacho tulikuwa na state-based economy na sasa baadhi ya majukumu hayo yamechukuliwa na private sector. Katika mazingira hayo, majukumu hayo yamepitwa na wakati, yatafutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia yako mashirika ambayo majukumu yao yanashabihiana sana na yenyewe yataunganishwa. Kwa hiyo, huo ndiyo msingi ambao tunazingatia.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo Mheshimiwa Mbunge amehoji ni kwamba, ilipaswa mchakato huu uje Bungeni na Bunge ndilo litoe uamuzi huu. Hata hivyo, kwanza tumezingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukisoma Ibara ya 37 ile Sehemu ya Nane, tumezingatia Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura ya 370, Sheria ya Msajili wa Hazina, pia tumezingatia Sheria iliyounda makampuni ya umma. Yote hii inaeleza mamlaka ya kufuta na kuanzisha shirika la umma yako wapi. Mamlaka haya yako wazi na yametajwa katika sheria mbalimbali. Kwa hiyo nimhakikishie Mbunge kwamba, mchakato huu umezingatia Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na umezingatia kikamilifu sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ambalo limezungumziwa hapa ni kwamba mchakato huu unaua morale ya wafanyakazi, sasa wafanyakazi wako demoralized. Kwanza, of course hoja yenyewe haina ushahidi wa kisayansi, hakuna utafiti ambao umeshafanyika ukaonesha kwamba, kuna wafanyakazi ambao morale imekufa, lakini nimhakikishie Mbunge kwamba, wafanyakazi wote wa mashirika ambayo yameunganishwa na kufutwa wameshirikishwa kikamilifu, lakini wamepewa taarifa sahihi.
Mheshimiwa Spika, mosi, hakuna mfanyakazi ambaye atapoteza kazi, kwa sababu mashirika haya hayafutwi au kuunganishwa kwa sababu ya ubovu wa wafanyakazi, hapana! Ni majukumu tu, hivyo wafanyakazi wote katika mashirika ambayo yanaunganishwa na yanayofutwa wapo salama kikazi na watafanya kazi katika taasisi za umma. Usisahau kwamba tayari kuna maeneo mengi ya utumishi wa umma ambayo yana upungufu wa watumishi, hivyo, zoezi hili litatupatia nafasi ya kupata watumishi wengine ambao watapelekwa katika maeneo mengine ya kazi. Kwa hiyo, suala la morale kwa watumishi wa umma halipo.
Mwisho, mchakato ambao tumeanza nao ni mchakato wa ndani ya Serikali hatimaye sheria husika zitabadilishwa au kuandikwa upya na Bunge hili litahusika. Pale ambapo mabadiliko ya kisheria yatahitajika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litahusika kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, naomba nihitimishe kwa kusema mambo makubwa matatu yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, mosi, katika utekelezaji wa mambo yetu tunazo nyenzo nne kubwa ambazo ni lazima tuendelee kuzishikilia:-
(i) Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 ambayo imetafsiriwa katika mipango yetu ya maendeleo na kwa sasa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 hadi 2025/2026.
(ii) Chombo chetu cha utekelezaji ni Serikali. Serikali imara inahitaji chama imara cha siasa. Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho kimeunda Serikali hii, kipo imara sana kuliko wakati mwingine wowote. (Makofi)
(iii) Tunahitaji nahodha imara. Hakuna shaka juu ya unyenyekevu, ushupavu, uzalendo, weledi na uchapakazi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
(iv) Tunahitaji Bunge imara ambalo linaakisi sauti na hisia za wananchi. Sina shaka na uimara wa Bunge lako, sina shaka na umahiri wa Wabunge wako. Chini ya uongozi wako makini sana, tuna imani kubwa kuwa kwa ushirikiano wa Bunge lako Tukufu, mipango yetu itaendelea kuwa thabiti, endelevu na kwamba fursa za uwekezaji zitaendelea kupanuka na kuimarika kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, nimezungumzia juu ya umuhimu wa nahodha na kwamba tunaye nahodha imara sana na amethibitisha hivyo. Uhodari wa nahodha wa meli haupimwi katika maji yaliyotulia, uhodari wa nahodha wa meli hupimwa wakati wa mawimbi makali baharini. Tangu aingie madarakani Mheshimiwa Rais wetu ameshavuka vikwazo vingi na kumudu kuivusha meli katikati ya mawimbi makali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nimtie moyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba yupo katika mstari sahihi na sisi wasaidizi wake na naamini Bunge lote hili tupo naye pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna wajibu kama Bunge na kama Watanzania katika kuhakikisha kwamba tunatekeleza wajibu wetu katika kuhakikisha kuwa nahodha wetu anatuvusha salama. Nahodha wetu akitikiswa sote tutatikisika. Katika kijitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania, Baba wa Baifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliandika, “Huwezi kumtikisa Rais na nchi ikawa salama.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tusikubali Taasisi ya Urais kutikiswa kwa sababu tukiruhusu hilo tutakuwa tumeruhusu kutikiswa kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo, naomba kutoa hoja na ahsante sana. (Makofi)