Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu, Mkuu wa Majeshi na timu yote ya Wizara ya Ulinzi kwa bajeti nzuri waliyoileta ndani ya Bunge na naomba Wabunge wote tuipitishe ili jeshi liweze kufanya kazi kwa bidii. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa sababu tunaona anaendelea kuviboresha vyombo vya ulinzi na usalama hasa jeshi letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa mipakani na hasa katika maziwa, mfano Ziwa Tanganyika, upande wa Ziwa Tanganyika ndiyo kuna lango kuu kubwa sana la uhalifu kwa sababu lipo mipakani na nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Rukwa hasa wavuvi mikoa hii mitatu Kigoma, Katavi na Rukwa wana changamoto kubwa sana ya wahalifu wanaotoka nchi jirani, wanapoenda kufanya shughuli zao za uvuvi, wanavamiwa wananyang’anywa nyavu zao na zana za uvuvi na pengine kuvuka kabisa kuja upande wetu na kunyang’anywa mali zao na fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru sana Wizara ya Ulinzi pamoja na Mheshimiwa Waziri na timu yote. Mimi kama Mbunge na mwakilishi wao natokea ukanda wa Ziwa Tanganyika niliandika barua ya maombi kuwaomba ili waweze kuja kujenga Kambi ya Jeshi ukanda wa Ziwa Tanganyika. Hatua hii imechukuliwa kwa haraka, wameshatuma timu ya wataalamu, wamekuja kuainisha eneo la Tarafa ya Wampembe, Kata ya Kizumbi, tayari eneo limeshapatikana. Kwa hiyo, niombe Wizara ipewe fedha ili kambi hii ikishajengwa wavuvi na wananchi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika wamepokea kwa raha sana na wanampongeza Mheshimiwa Rais, kwa sababu hawana hofu tena ya uvamizi (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kambi hii ikijengwa wavuvi wanaofanya shughuli za kiuchumi watafanya kazi bila hofu na maendeleo yatakuwepo, kwa sababu kutakuwa ulinzi ndani ya Ziwa Tanganyika. Kambi ikijengwa itakuwa inafanya kazi ya intelligence gathering ndani ya ziwa na kutoa elimu katika ukanda wa Ziwa Tanganyika hasa kwa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi za JKT; sasa hivi tunaona kuna mwamko na mwitikio mkubwa sana wa vijana wetu kujiunga na Kambi za JKT. Kambi za JKT zilizopo ni chache. Tunaomba Wizara ipewe fedha ili vijana wetu waende wakapewe elimu ya uzalendo ili wawe na mapenzi na nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamechangia kuhusu bomu la kufukuza tembo, niiombe Wizara ya Maliasili na Utalii, sasa iweke ushirikiano na Jeshi letu lililovumbua bomu la tembo, ili pale mara inapotokea changamoto ya tembo kuvamia makazi ya watu, Jeshi la Ulinzi pamoja na Wizara ya Maliasili kwa pamoja waende kwa haraka ili kuweza kutatua changamoto hiyo kwa haraka ili wananchi waendelee kufanya kazi zao kwa amani na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ya jeshi wamesema tunaona kuna changamoto; niiombe Wizara ipewe fedha maeneo yote ili yapate hati kamili ili maeneo ya jeshi yasivamiwe, yawe na hati kamili ili kuondoa migogoro kati ya wananchi na wanajeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)