Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na kwanza kabisa ninaunga mkono hoja bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu kwa namna anavyofanya kazi kubwa hasa kulinda na kulishughulikia jeshi letu na kuhakikisha kabisa kwamba, nchi yetu inakuwa na amani muda wote saa 24, siku saba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Waziri Mheshimiwa Dkt. Stergomena kwa kazi nzuri anayoifanya, nimpongeze pia Katibu Mkuu ndugu yangu Dkt. Faraji, niwapongeze wote wakiongozwa na CDF Jenerali Mkunda, Mnadhimu Mkuu Luteni Jenerali Salum Othman, Major Generals wote pamoja na ma-CDF wastaafu, nimemwona pale ndugu yangu Jenerali Mstaafu Mabeyo, wote kwa pamoja wanafanya kazi. Jenerali Mabeyo alifanya kazi kubwa sana wakati ule ameliweka jeshi vizuri sana. Vilevile nimpongeze na niendelee kumpa moyo CDF Mkunda, kwa kazi kubwa anayoifanya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza muda wake pale ameongelea masuala mazima ya mpakani. Nchi yetu ina historia kubwa sana kutoka wakati wa Awamu ya Kwanza ya Mheshimiwa Rais wetu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kwa wakati ule nchi yetu ilikuwa katika ile hali ya kukomboa nchi nyingi za Afrika ikiwemo Msumbiji, Zimbabwe na kazi yote hiyo ilifanywa na jeshi letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya vijana wa jeshi by then tulikwenda physically kabisa kuwasaidia nchi hizo kupata uhuru, lakini hali ile imekwenda na sasa hivi nchi zote zimepata uhuru tulizozikusudia zipate uhuru kwa wakati ule Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini operation zinaendelea mpaka sasa hivi? Kwanza kabisa tumshukuru Mungu kwa neema hii ya amani ambayo tunayo sasa hivi. Tunamshukuru sana hii ni zawadi tu kwa Mungu kwamba nchi ya Tanzania iwe ya amani. Nchi za jirani zinapokuwa hazina amani inakuwa ni kimbilio kuja kwetu kwa maana kutaka amani ama kwa mazungumzo au hata kutuma vijana wetu wa jeshi kwenda kulinda amani kama ambavyo inafanya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi vijana wetu wapo kwenye mpaka hapo Mtwara na Msumbiji, vijana wapo Congo, vijana wapo Afrika ya Kati, vijana wapo wanafanya kazi kubwa mno, hii yote ni kwamba, tulinde amani kule tuwasaidie ili chochoko zile zisije zikaleta tashwishi katika nchi yetu hii nzuri ambayo Mungu ametusaidia mpaka hivi sasa kuwa nchi ya amani katika Afrika namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hizi operation zinazofanywa ni kazi kubwa, vijana wanafanya kazi kubwa sana. Mimi nishauri tu kwamba katika bajeti waliyopanga Mheshimiwa Waziri ahakikishe kabisa fedha hizi kwa ajili ya operation zinapatikana kwa wakati muda wowote na kwa uharaka ule ule unaotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya kwamba inaweza ikatokea jambo sasa hivi tu la haraka na la za dharura sasa fedha zinapochelewa ili kwenda kuwahudumia hawa kwa maana ya kununua mitambo, kuwapa maslahi yao waweze kwenda kwa haraka inakuwa siyo jambo zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuhakikishe kabisa kwamba fedha zinakuwa kwa wakati wote, muda wote na nimesoma bajeti yake Mheshimiwa Waziri, kuna asilimia almost 21 fedha hazijakamilika kwa maana kuanzia mwezi Aprili, lakini toka mwezi Aprili mpaka tunapoenda kumaliza bajeti hii mwezi Aprili, ahakikishe basi hii 21% ya bajeti tuliyopitisha mwaka jana wanaipata jeshi hili ili waendelee kufanya majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi majeshi yote duniani yanakwenda kidigitali, tutoke huku tulipo sasa hivi. Mimi naamini kabisa sina mashaka na wanajeshi, sina mashaka na CDF na sina mashaka kabisa na wanajeshi, wapo wataalamu wazuri sana na waliobobea na ni wazalendo kwa muda wowote. Ukiwatuma wakati wowote wanakwenda kufanya kazi nzuri kabisa ya kulinda nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zana ambazo tunazo kama itampendeza na ninafikiri wakikaa kama kikao, tutoke kwenye zana hizi twende kwenye zana za kisasa. Zana za kisasa ni pamoja na zana ambazo sasa hivi utaona wanajeshi wanatumia zana chache tu wanakaa hivi, vitu vinakwenda kule kulinda nchi yetu. Kuliko kutumia zana za zamani ambazo zinakuwa na gharama kubwa au kazi kubwa kabisa ya kufanya mobilization na mitambo ile au zana zile kwenda kwenye eneo ambalo tumekusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona jeshi upande mwingine inapotokea janga lolote au dharura tunakwenda kuomba wanajeshi ili watusaidie. Tumeona pale Manyara, tumeona pale Kusini barabara imekatika na tumeona maeneo mengi tu, lakini kitengo hiki ni muhimu sana kwa maslahi ya Taifa letu. Hiki kitengo tunakisaidiaje? Kwa maana kwamba, tuna fedha gani ya kuwasaidia hawa. Wanahitaji mitambo ya kisasa, wanahitaji zana za kisasa, wanahitaji kufanyiwa training na wanahitaji magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, mnakumbuka wiki mbili tatu mvua iliyonyesha wakati ule imenyesha zaidi ya siku tatu, nne, tano tu au wiki mbili, tatu mafuriko ya nchi nzima. Waliokwenda kutusaidia wale ni akina nani? Ni wanajeshi wenyewe. Ukiona Wanajeshi wanavyokwenda kusaidia pale wanakwenda kizalendo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotakiwa hapa ni kuwasaidia kuwapa zana ili kazi ya kwenda kusaidia kama ni kujenga barabara, kama ni kujenga daraja na kama ni kusaidia wananchi wawe na zana. Kazi ya siku mbili, tatu wanakwenda wiki nzima, why? Hapana. Tuone namna ya kuwasaidia hiki Kitengo cha Uokoaji katika Jeshi letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Nyumbu ni eneo kubwa sana na bado ninaliongelea sana. Hivi tukikaa kabisa tukasema tunatenga bajeti hii hapa tunataka Nyumbu sasa izalishe vifaru. Tunataka Nyumbu sasa izalishe magari ya kijeshi, tunashindwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Wachina wanaanza miaka 30 iliyopita walikuwa wana-copy na ku-paste. Wanachukua magari ya Ulaya, wanachukua magari ya Marekani wanayafumua wanayatengeneza kama hivyo wanaweka jina lao pale. Jeshini kuna watu wapo vizuri mno wamesoma. Mimi ninaamini hivyo na wana uwezo na ni wazalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala tu la kukaa kuona sasa hii Nyumbu tunaiwekea fedha gani shilingi bilioni 200, shilingi bilioni 500, kwa namna ambavyo watakavyofanya visibility study au business plan. Wataona namna ya kuihuisha hii Nyumbu ili iweze sasa kuzalisha magari, kuzalisha vitu pale ambavyo vitakwenda kulisaidia jeshi letu huko mbele ya safari na inawezekana tukauza hata nchi ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kuna nchi ndogo ndogo hapa Vietnam wanaanza kutengeneza vifaa, sijui Bulgaria. Bulgaria miaka 30 iliyopita walikuwa sawa na sisi tu. Wanafyatua risasi, wanatengeneza silaha, wanatengeneza kila kitu. Sisi tunashindwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Nyumbu pale ndio unaona kabisa hili jengo Watanzania waliopo hapa, uzalendo uliopo hapa, wanajeshi waliopo hapa, kilichobaki ni kidogo tu. Kupanga mikakati, kutenga bajeti kusukuma ili mambo yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maslahi ya wanajeshi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ahmed, muda wako umekwisha.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)