Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya wote nimshukuru Mwenyezi Mungu na hatimaye nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ndio Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yetu ya Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampa pongezi Mheshimiwa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu za msingi na sababu hizo si nyingine isipokuwa Mheshimiwa Mama na Amri Jeshi Mkuu, ameendelea kufanya kazi kuisimamia nchi yetu, hata pale nchi ilipopata misukosuko yeye aliweza kusimama imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa misukosuko mikubwa iliyojitokeza hivi karibuni ni pamoja na nchi kupata mvua zisizokuwa za kawaida. Mama amesimama imara na akawaambia Watanzania msiwe na wasiwasi na hata ile hotuba yake katika sherehe za kutimiza miaka 60 ya Muungano aliwaambia Watanzania kaeni, kuweni na subira, kuweni makini, yupo tayari kuhakikisha kwamba, miundombinu yote iliyoharibika tutairejesha na itakuwa salama, wananchi msiwe na wasiwasi. Huyu si mwingine bali ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Amiri Jeshi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyoona na kutambua kwamba Amiri Jeshi Mkuu ndio namba moja, hatimaye, yanafuatia majeshi mengine, yeye akisimama imara hata haya Majeshi yatasimama imara. Tunalipongeza Jeshi kwa kazi kubwa na nzuri inayoifanya na hapo kuna viongozi ambapo wanaongeza majeshi haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jenerali Jacob John Mkunda, tunampongeza sana kwa kazi nzuri, Luteni Jenerali Salim Haji Othman, tunampongeza sana, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele, tunawapongezeni sana kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax kwa kusimamia vizuri Wizara yake. Sambamba na hilo leo hotuba yake ameitoa vizuri sana tena sana, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema ulinzi na usalama; hali ya ulinzi na usalama wa nchi yetu ambayo taarifa imetolewa hapa ya mwaka 2023/2024 mipaka ya nchi yetu ipo shwari kabisa. Urefu wa mipaka ya nchi yetu ni zaidi ya kilometa 5,923.41, tunaambiwa mipaka ipo shwari kabisa. Usivione vinaelea hivi vimeundwa na waundaji si wengine bali ni pamoja na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaambiwa mipaka ya nchi kavu na mipaka ya maji yote ipo shwari, lakini pamoja na ushwari huo ambao unapatikana bado tuna changamoto kadhaa. Nitazitaja changamoto chache tu ambazo zinakabili mipaka ya nchi yetu.

Mheshimiwa NaibU Spika, kama tunavyofahamu bila kuwa na usalama wa nchi, bila mipaka kulindwa vizuri hata haya mafanikio makubwa tuliyoyapata yanaweza yakaharibika. Kwa hiyo, tuna wajibu mkubwa wa kuendelea kulinda mipaka hii ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano Tanzania na Kenya kuna uharibifu wa alama za mipakani, lakini pamoja na uharibifu huo kazi inaendelea na kila kitu kinaendelea vizuri. Mipaka inapoanza kuwa na uharibifu hii ni hatari.

Sasa tukienda Tanzania na Malawi na kule kuna changamoto katika Ziwa letu Nyasa, lakini kazi nayo inaendelea kuhakikisha hali inakuwa shwari. Kuna Tume maalumu ya usuluhishi na hili ni jopo la viongozi wastaafu. Tunawatakia kila la heri na mafanikio ili matatizo haya au changamoto hizi zimalizike haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna Tanzania na Msumbiji. Upande wa kule Kusini Mtwara na Lindi. Msumbiji kule kuna kadhia ambayo kadhia hii inaletwa kutokana na kundi la kigaidi linaloitwa Ansar Al Sunna Wal Jamaah hawa wapo katika eneo la Kaskazini mwa Msumbiji na katika Jimbo la Cabo Delgado. Hili Jimbo ndilo linalopakana na Mkoa wa Mtwara na Lindi yake kwa ujumla. (Makofi)

Sasa tutambue kwamba Mtwara na Lindi kuna miradi ya kimkakati. Kuna gesi asilia ipo Mtwara na Lindi, lakini kuna zao la korosho na zao hili ndilo linalotuingizia…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mama Kikwete hoja hizo zinazungumzwa kwenye Kamati.

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na hayo nataka niwapongeze vilevile hawa Wana-Nyumbu. Nyumbu hawa wametengeneza bomu; na bomu hili ni bomu baridi la kuwafukuza tembo. Tunashukuru sana kwa sababu tembo walikuwa ni shida katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunaomba hii bajeti ambayo mwaka huu imekuja ya shilingi trilioni 3.3 imekuja wakati muafaka na imeongezwa vizuri ukilinganisha na mwaka uliopita. Ahsante sana kwa kuongeza hii bajeti, tunawapongeza sana, tena sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika kutokana na suala la bomu, elimu itolewe yasije yale mabomu yakalia wakafikiria ndiyo wale watu wametoka huko sasa hivi wametuingilia kwenye maeneo yetu kumbe ni suala la bomu lile kuwafukuza hawa wanyama tembo au jina lingine wanaitwaje vile? Wanyama ndovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa 100%. (Makofi