Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Shamsi Vuai Nahodha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, mwaka 1987 Marehemu Baba wa Taifa alipokuwa akihutubia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama chake Cha Mapinduzi alisema; “Tatizo kubwa la Afrika si ukosefu wa rasilimali bali tatizo kubwa la nchi za Kiafrika ni matumizi sahihi ya rasilimali walizopewa na Mwenyezi Mungu.” Maneno haya ya Mwalimu yananifanya nitafakari sana juu ya namna tunavyosimamia uchumi wa gesi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimeanza kusikia mipango ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya gesi asilia tangu nilipoingia kwenye Bunge hili Tukufu mwaka 2010. Ni kama miaka 14 hivi na kwa bahati mbaya hatujaweza kutekeleza kikamilifu mipango hiyo ya kutekeleza uchumi wa gesi kama tulivyodhamiria. Nitaeleza jinsi tunavyopoteza fursa mbalimbali za kiuchumi kadiri tunavyoendelea kuchukua muda mrefu kutekeleza mipango hiyo ya uchumi wa gesi na nitatoa mifano kwenye maeneo manne.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza, nchi yetu inatumia takribani 50% ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nchi za nje. Kama tungefanya maamuzi kwa wakati mwafaka tukatekeleza miradi ya kuanzisha nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya magari na mitambo bila shaka tungepunguza sana matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nje. Jambo hili lingekuwa na maslahi mapana sana kwa ajili ya uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, hivi sasa vitendo vya ukataji miti vinaendelea kwa kasi sana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, hata katika ripoti ya Waziri Mkuu amelisema jambo hili. Naamini kama tungetekeleza miradi hii na mipango ya uchumi wa gesi kwa wakati bila shaka tungeweza kusambaza gesi katika majumba mbalimbali ya wananchi. Sasa badala ya wananchi kuendelea kukata miti wangetumia gesi kupikia na hatimaye tungeweza kuokoa miti na kuimarisha mazingira ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, hivi sasa tunatumia 40% ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mbolea kutoka nje na kwa bahati nzuri Mwenyezi Mungu ametubariki hazina kubwa ya gesi asilia hapa nchini. Tungeitumia gesi asilia kikamilifu tungeweza kuanzisha viwanda vya kutengeneza mbolea na tungeweza kuleta mapinduzi makubwa sana ya kilimo hapa nchini. Kwa isivyo bahati hatujalifanya jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne na la mwisho, hivi sasa tuna upungufu mkubwa sana wa fedha za kigeni, ningetarajia huu ungekuwa ni wakati mwafaka wa kutekeleza mradi wa muda mrefu wa kusindika gesi asilia ili tuweze kuuza nje kimiminika cha gesi ili tupate fedha za kigeni. Kwa isivyo bahati mradi huu haujatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, kwa maoni yangu mradi huu umechukua muda mrefu sana na moja ya sifa kuu ya viongozi ni kufanya maamuzi kwa wakati mwafaka na kutumia fursa zilizopo. Natambua kuna haja ya kufanya majadiliano kwa umakini, lakini nina wasiwasi, kadri tunavyoendelea kuchukua muda mrefu ndivyo tunavyoendelea kupoteza fursa za kiuchumi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tuzingatie mambo matatu, laiti tungeutekeleza mradi wa kusindika gesi kwa 100%, miaka mitatu iliyopita tungeweza kuitumia fursa ya vita inayoendelea kati ya Ukraine na Russia kwa ajili ya kuuza kimiminika cha gesi Nchi za Ulaya na kupata pesa za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili la tafakari, kadiri tunavyoendelea kutafakari namna tutakavyoitumia nishati ya gesi katika kuendesha mitambo na magari, wenzetu kwa mfano Elon Musk ameshaanza kuzalisha magari yanayotumia betri za umeme.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu la kutafakari ni kwamba, hivi sasa kuna utafiti mkubwa sana unaoendelea katika Nchi za Ulaya wa kutumia hewa ya nitrogen kama chanzo kikuu cha nishati na bila shaka jambo hili likifanikiwa basi hapana shaka matumizi ya gesi asilia duniani yatapungua sana. Kwa maana hiyo Tanzania kama Taifa tutakuwa tumepoteza fursa kubwa sana ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba nimalize mchango wangu kwa kunukuu maneno aliyoyasema Hayati Baba wa Taifa; “Inawezekana, timiza wajibu wako.”

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)