Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, kutokana na muda naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na namna anavyotuongoza, lakini nitoe pongezi za jumla kwa Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara kwa kazi nzuri inayofanywa katika Wizara hii. Mungu azidi kuwabariki kwa sababu tumeona juhudi walizonazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuwa na machache tu kwa sababu ya muda, kwanza niishukuru na kuipongeza Serikali kwa kutangaza tender kwa ajili ya kuweka umeme katika visiwa. Nchi yetu ina visiwa 289 na katika visiwa 289 ni visiwa 229 vina shughuli za kibinadamu na kati ya hivyo visiwa 16 vina uwekezaji. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba umeme ulioko kule pengine ni wawekezaji wenyewe wameweka. Kwa hiyo, katika tender ile inaonekana ni visiwa 120 ambavyo vimetangazwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Serikali kwa sababu nimekuwa nikiomba katika suala zima la kuweka umeme kwenye Kisiwa cha Bezi kilichopo Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ilemela ambacho kina wakazi takribani 3,742. Wamekuwa na umeme wa solar kutoka kwa mwekezaji anayeitwa PowerGen Renewable Energy lakini alikuwa anatoza pesa shilingi elfu moja kwa saa na umeme unawaka saa 11, mwisho saa tatu usiku, lakini wakati mwingine hauji ila kesho yake inabidi utoe tena 1,000. Kwa hiyo, niishukuru sana Serikali kwa sababu itakwenda kuokoa uchumi wa wale wavuvi ambao wamekuwa wakikusanya pesa zao kwa ajili ya maendeleo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, napenda kuishukuru Serikali na kuipongeza sana katika suala zima la uzalishaji wa umeme. Umeme unaozalishwa, uwezo wa mitambo yetu au vyanzo vya maji ni megawatts 2,138 lakini mpaka sasa inazalisha megawatts 1,756, lakini mahitaji ambayo tuko nayo ni 1,590. Maana yake kuna extra lakini katika extra inaonekana kabisa pengine kunakuwa na changamoto za hapa na pale kulingana na mitambo na uchakavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niiombe tu Wizara, kwa sababu juhudi zinaonekana na ongezeko la uzalishaji kuingiza umeme kwenye Grid ya Taifa unakwenda kuwa mzuri baada ya Bwawa la Mwalimu Nyerere kuanza kuingiza umeme wa megawatts 235 kupitia mtambo namba tisa. Nadhani tutajikuta tuna umeme wa ziada ambao tutakwenda kuhudumia nchi za jirani. Tuna imani kazi hii ikikamilika Tanzania inakwenda kuuza umeme katika nchi jirani jambo ambalo litatuletea fedha za kigeni na kufanya mambo mengine yaende vizuri. Niishukuru sana Serikali kwa hiyo kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu nataka kuzungumzia umeme wa gesi asilia. Tuipongeze Serikali kwa wazo zuri hasa la kufanya magari yetu na mambo mengine yaweze kutumia umeme huo, lakini tayari kuna baadhi ya miji kwa mfano, Dar es Salaam umeanza kuingia katika maeneo ya nyumba zetu lakini pia na magari yanatumika. Ombi langu na rai kwa Serikali, tunahitaji kuwa na vijana wengi wanaobadilisha mfumo wa magari kwenda kwenye mfumo wa kutumia gesi, waliopo ni wachache na mahitaji ni makubwa.
Mheshimiwa Spika, pia, uingizaji wa magari nchini ni vyema sasa kwa sababu tuna gesi nyingi tuone tu namna ya kuingiza magari ambayo yatakuja na mifumo tayari ambayo itakuwa imeshawekwa. Unapowekwa kwa utaratibu wetu na ujuzi wa vijana wetu kidogo hata ile hali ya mazingira kwenye gari inakuwa siyo nzuri. Kwa sababu gari limeandaliwa kuweka pengine mizigo kwa nyuma lakini unakuta ndiyo mtungi wa gesi umewekwa kule. Kwa hiyo, yale matumizi yanakuwa si sahihi sana. Kwa hiyo, tuombe kwa yale yatakayokuwa yanakuja, basi yawe na hiyo mifumo tayari imewekwa, lakini vijana waweze kupata ajira na waongezeke wale wanaokwenda kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni vituo ambavyo vinasambaza gesi hii, tuna vituo viwili tu kwa Dar es Salaam. Kipo kile kimoja cha kule Airport na Ubungo. Kama alivyosema Mheshimiwa Kanyasu juzi ni adha kubwa kwa sababu foleni ni kubwa, mahitaji ni makubwa, mtu anapoteza zaidi ya masaa nane anasubiri kuweka gesi. Kazi zake anafanya saa ngapi? Kwa hiyo, tuombe sana vituo viongezeke na ile kasi ya kuweka katika mikoa mingine basi waone hata ile miji mikubwa tuweze kuweka huduma hiyo kwa sababu mahitaji yatakuwa ni makubwa zaidi. Pia, tutakuwa tumesaidia sana kwa suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo nataka kuzungumzia ni suala la Mheshimiwa Rais ambaye amekuwa kinara wa kutaka sana kufikia mwaka 2032 tuweze kuwa na nishati safi. Kwa maana kuwa na clean energy katika masuala mazima ya mapishi na mambo mengine. Tumefanya juhudi kubwa Wabunge wote hapa tumesambaza mitungi ya gesi katika maeneo yetu. Bahati nzuri sana wananchi wameitikia vizuri, changamoto inakuja wanapotaka ku-refill zile gesi zao wanatembea mwendo mrefu sana. Matokeo yake hata ile nafuu tunayoitegemea inakuwa haipo. Tuombe sana mawakala wawepo mpaka katika maeneo ya vijijini ambako gesi hii imefika na matumizi ni makubwa. Niombe katika hilo kwa sababu namna bora ya kuweza kuwafikia hawa ni kuwapa huduma ya karibu ili waweze kuona nishati ile ni safi na salama, lakini pia ni nafuu ukilinganisha na suala la matumizi ya kuni au mkaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni umeme wa REA ambao umesambazwa katika nchi yetu na niipongeze tu Serikali kwa sababu imefikia vitongoji na vijiji vingi. Rai yangu, ile scope ya mwanzo katika kufikisha umeme wa REA ilikuwa ni ndogo. Matokeo yake sasa hivi watu wako kata moja, mwingine ana-enjoy umeme wa shilingi 27,000, mwingine anaambiwa sasa alipe 320,000 kwa sababu tu REA imemaliza kazi yake katika yale maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali kwa sababu ni Serikali sikivu na wananchi wanaiamini sana na ndiyo maana tunaye Rais ambaye ni msikivu na ni Rais ambaye katika kujielekeza kwake kwenye kutawala nchi hii amekuja na maridhiano, amekuja na 4R. Sasa niombe hilo hilo katika kumuenzi Mheshimiwa Rais katika ule mtazamo wake, kwa sababu maeneo yale tulishayagusa kwa umeme wa REA katika maeneo yote nchini na Ilemela ikiwemo, basi tuone namna yale ambayo bado yana sura ya vijiji tukamilishe tu kwa kuweka REA badala ya kuwa-charge tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine. Hiyo itatusaidia sana katika suala zima la kupeleka huduma hiyo kwa wananchi ambao wata-enjoy huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa suala zima la usafiri...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga, sekunde thelathini malizia.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja na naipongeza Serikali kwa kazi nzuri, lakini pia naipongeza sana Kamati yangu ya Nishati na Madini kwa kazi nzuri na nakubaliana na yote ambayo yamewekwa mezani. Serikali basi ikapokee ule ushauri wa Kamati ili tuweze kwenda vizuri, ahsante. (Makofi)