Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kutoa mchango wangu. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wake, mdogo wangu Judith Kapinga, nimpongeze sana kwa kazi nzuri. Ameingia katika kipindi kigumu lakini ametumia kipindi hicho vizuri na ameonesha uwezo wake.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa naomba kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya. Wote tunaona ni namna gani ambavyo Mheshimiwa Rais amepambana katika kukamilisha miradi yote ya kimkakati ambayo iliachwa katika awamu iliyopita. Amejijengea historia kubwa na sisi kama Wabunge hatutoacha kulisema hilo na kuendelea kumshukuru.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kuendelea kuzungumzia masuala mbalimbali hususani katika Mkoa wa Songwe. Sote tunafahamu matatizo makubwa ambayo tulikuwa nayo sisi kama nchi hususani suala la kukatikakatika sana kwa umeme katika Nchi ya Tanzania, vilevile katika Mkoa wetu wa Songwe. Hii inatokana na kwamba tumekuwa na vyanzo vichache, Tanzania kwa muda wa miaka mingi tulikuwa tunategemea vyanzo vichache kwa ajili ya kuzalisha umeme. Naomba nitumie nafasi hii kutoa ushauri kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, ni wakati muafaka sasa Serikali iangalie ni namna gani ya kuweza kuongeza vyanzo vingine vya kuzalisha umeme hususan umeme ambao unatumia maji, huu ni miongoni mwa umeme ambao una gharama nafuu. Pia, tumeona namna ambavyo Mheshimiwa Rais amekamilisha Bwawa la Mwalimu Nyerere, kwa hiyo, niiombe sana Wizara ijikite kwenye mikakati madhubuti ya kuja na vyanzo vingine vya kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu, tunao Mradi mkubwa sana wa Ruhuji pamoja na Lumakali kule Njombe, mradi huu ulifanyiwa usanifu mwaka 1998, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa sababu ameamua kuuhuisha mradi huu ambao ulisimama kwa muda mrefu na tayari amakwishatoa maagizo kwa Wizara ili kuhakikisha mradi huu unaanza kutekelezwa. Niiombe sasa Wizara iweze kusimamia ili kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa wakati kwa sababu utasaidia sana kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme katika nchi yetu. Vilevile, kama ambavyo Waziri Mkuu amesema juzi utasaidia sana kama nchi kuuza umeme katika nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba viko vyanzo vingi vya umeme. Pia, tunao umeme wa jotoardhi, Mkoa wetu wa Songwe tumebarikiwa. Katika Mkoa wa Songwe tunayo maeneo mengi sana ambayo tunaweza kuzalisha umeme wa jotoardhi. Kwa mfano, ukienda pale kwenye kile Kijiji cha Majimoto Wilayani Mbozi, tayari pale ipo kampuni tanzu ambayo imeanza kuufanyia kazi ule mradi. Naomba sana Wizara iweze kuongeza msukumo ili mradi ule uweze kukamilika kwa wakati na Mkoa wa Songwe tuweze kuwa na vyanzo vya kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Spika, vilevile, kwa sababu tunayo maeneo mengi niiombe pia Wizara iweze kufanya utafiti kwenye maeneo mengine ndani ya Mkoa wa Songwe ambayo yanaweza kusaidia kuzalisha umeme wa jotoardhi.

Mheshimiwa Spika, pia tunao umeme wa jua. Tumeona Wizara ambavyo imekuja na mkakati na tayari wamekwishaanza kuzalisha umeme wa jua kwenye mikoa mingine kama vile Mkoa wa Singida na Mkoa wa Shinyanga. Naomba watanue wigo kwenye mikoa mingine, kwa mfano Mkoa wa Songwe na mikoa mingine ili tuweze kuzalisha umeme wa jua.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la usambazaji wa umeme, katika Mkoa wa Songwe kwa miaka mingi tulikuwa tuna changamoto ya kukatika kwa umeme. Mkoa wa Songwe ilikuwa ni kawaida umeme unakatika asubuhi, unakuja kuwaka saa nane halafu saa kumi na mbili umeshakatika, lakini ndani ya muda mfupi tumeona tayari umeme umeshatengemaa ndani ya Mkoa wa Songwe. Hizo ni jitihada kubwa ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya pamoja na viongozi wa Wizara, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, ninalo ombi moja, kwa sababu tunayo ile gridi ya Taifa ya kutoa umeme kutoka Iringa kuja Mbeya mpaka Songwe pamoja na nchi nyingine za SADC, naomba sana Wizara iweze kukamilisha huo mradi kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, pia tunayo ile Station ya umeme pale Nkangamo, tunaomba pia Wizara itusaidie kukamilisha ili sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe tuondokane na kutegemea station kutoka katika Mkoa wa Mbeya.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala lingine ambalo nalo ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na umeme wa kuweza kujitegemea. Tunafahamu hali ya usambazaji wa umeme na niipongeze sana Serikali imefanya kazi nzuri sana, sisi kwenye Mkoa wa Songwe tuna vijiji 470, katika vijiji hivyo 470, vyote vimeunganishwa kwenye umeme.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali inapokwenda kwenye mkakati mwingine wa kuhakikisha kwamba wanakwenda kusambaza umeme kwenye vitongoji na sisi Mkoa wa Songwe tuna vitongoji 1,489. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ambaye amekuwa akija sana kwenye Mkoa wetu wa Songwe, watakapoanza kusambaza umeme kwenye hivi vitongoji 789 ambavyo vimebaki, ambavyo havijaunganishwa umeme katika Mkoa wa Songwe, niombe sana usambazaji huo uende kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, kimekuwa ni kilio cha muda mrefu cha wananchi, utakuta kwamba nguzo zimewekwa lakini umeme hawauoni. Naomba wakandarasi wasimamiwe ili waweze kuwaunganishia umeme wananchi kwa wakati ili Mkoa wetu wa Songwe ambao umekaa kimkakati, uweze kuwa na umeme na kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza katika mkoa wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nimalize kwa kumpongeza sana Meneja wetu wa TANESCO, Mkoa wa Songwe, anafanya kazi nzuri sana, sisi kama Wabunge tunapata ushirikiano wa kutosha, nampongeza sana pamoja na wasaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)