Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupatia afya njema na fursa ya kusimama katika Bunge lako Tukufu. Kabla ya kuanza kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo aliniamini na kunipa heshima kubwa ya kuhudumu katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Namshukuru sana kwa sababu imenipa upeo mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu mengine ambayo naendelea nayo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, kwa hotuba yake nzuri aliyoiwasilisha pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Judith Kapinga, kwa usikivu wao na namna ambavyo wanajituma katika kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, sasa nianze kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nimepitia hotuba hii na nikaona Wizara ina vipaumbele kama tisa. Moja ya kipaumbele ni kuendelea kupeleka nishati vijijini ikiwemo kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara. Nawapongeza sana kwa sababu malengo haya ni mazuri na ni makubwa kwa ajili ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Mwanza, nasikitika kuona takribani vitongoji 2,476 bado havijafikiwa na huduma hii ya umeme, kikubwa zaidi Mkoa wa Mwanza umezungukwa na visiwa, takribani Majimbo matano yana visiwa. Moja ya Jimbo ambalo lina visiwa vingi zaidi ni hili Jimbo la Ukerewe ambako kuna visiwa takribani 38. Jimbo hili halina umeme wa uhakika. Mfano, katika Kisiwa cha Irugwa pamoja na Ukara ambapo kuna population kubwa ya wananchi, hawana umeme wa uhakika, umeme wanaoutumia ni umeme wa jua.
Mheshimiwa Spika, unit moja ya umeme huu inauzwa kwa takribani shilingi 1,500 mpaka shilingi 2,000, hii ni gharama kubwa na ukizingatia umeme huu hawautumii kwa masaa 24, ikifika saa nne usiku tu umeme huu unakatwa. Hivyo, tunaiomba Serikali iweze kuharakisha mradi uliopo pale Ukerewe upelekwe moja kwa moja katika visiwa hivi ili kupunguza changamoto iliyopo katika visiwa hivi na kuharakisha uchumi katika maeneo haya ya visiwani.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Magu ambako kuna Kisiwa cha Ijinga napo kuna giza, tunaomba sana Serikali iweke jicho pale. Kuna Jimbo la Sengerema, kuna Visiwa vya Lyakanyasi, Bihila, Chitandele, Chikomelo, Jimbo la Buchosa pia kuna Soswa, Nyamg’honge, Itole, Ikuru, Yodzu, Kasalazi na Gembale, maeneo haya yapo gizani. Tunaomba sana Serikali kama imeamua kutupatia sasa umeme wa solar basi wananchi waweze kupata kwa bei iliyo nafuu ili uchumi wa wananchi hawa uweze kuendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu nishati safi ya kupikia. Niipongeze sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo imeweka mkazo katika matumizi safi ya nishati safi ya kupikia. Nina masikitiko makubwa sana katika eneo hili, takribani 90% ya nishati inayotumika ni ya mkaa na kuni, nishati ya gesi inayotumika mpaka sasa ni asilimia tano tu. Naiomba Serikali iweze kuhamasisha katika maeneo haya ili wananchi wabadilishe namna ya matumizi ya kutumia nishati safi ili kuokoa mazingira pia kuangalia namna ya kuepukana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakiikumba dunia mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, wananchi sasa hivi wamehamasika sana kutumia nishati safi ya gesi, lakini gesi hii ina gharama kubwa sana. Tunaiomba Serikali na kwa kupitia hotuba ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, tumeona kuna punguzo la bajeti ambapo mwaka jana kwa bajeti hii inayoishia Juni walikuwa na trilioni 3.08 na sasa imepungua mpaka trilioni 1.88, tunaiomba Serikali kwa hili punguzo basi iweke ruzuku kwenye nishati safi ya kupikia ili akinamama ambao kwa 90% ndiyo wahanga wa eneo hili, waweze kunufaika na nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kuona tunawahamasisha wananchi wasikate miti hovyo, wasiharibu mazingira lakini wanaporudi kwenye upande wa pili wanakutana na gharama kubwa za matumizi ya nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kupitia hotuba ya Wizara niliona TANESCO ina deni ambalo wanazidai taasisi takribani bilioni 86, deni hili linaonesha kwamba limesababishwa na baadhi ya taasisi hazijaunganishwa katika umeme wa LUKU. Wananchi wanapokuwa na changamoto ya umeme mara nyingi madeni yao wanahakikisha wamekamilisha na ndipo LUKU ianze kuendelea kutumika, hivyo naziomba hizi taasisi kupitia Wizara wawaingize kwenye LUKU ili madeni yao wawe wanakatwa taratibu wakati huo huo wanalipa deni la TANESCO ili kuiwezesha TANESCO kujiendesha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)