Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii ya kuongea tena Bungeni kwenye Wizara hii ya Nishati. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi, uwezo na uhai aliotupatia ili kuweza kuifikia siku ya leo na kuweza kupata nafasi ya kuongelea nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa utashi na kukubali kuendelea kutoa fedha nyingi kwenye Wizara hii ya Nishati na tukaona mambo mengi yanayotekelezwa sasa kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza sana ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati akiwemo Naibu wake mdogo wangu Mheshimiwa Judith Kapinga kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwenye Wizara hii. Ni ukweli usiopingika kwamba tunakumbuka tulikuwa na changamoto kubwa sana ya umeme na sasa tuna mazungumzo kwamba kuna ziada kidogo kwenye umeme, maana yake kuna kazi kubwa sana imefanyika hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nawapongeza sana wataalamu wakiongozwa na Katibu Mkuu ndugu yangu Mramba. Vilevile nawapongeza viongozi na wataalamu mbalimbali katika Taasisi za Wizara hii ya Nishati ikiwemo TANESCO, TPDC, REA, EWURA na PURA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukipita kwenye Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa nane kifungu cha 11 utaona utekelezaji mkubwa uliofanyika mwaka jana pia ulifanyika kwa mwaka huu wa fedha ambao unamalizika kwa sababu tulipewa shilingi trilioni tatu. Kwa hiyo yako mambo mengi sana yamefanyika. Ukiangalia fedha ya maendeleo takribani shilingi trilioni 2.6 mpaka Machi imekwishatolewa shilingi trilioni 1.7, maana yake pesa nyingi imetolewa kwa ajili ya utekelezaji huu. Kwa hiyo nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu iko pesa nyingi imeingia kwenye maeneo haya na wanamalizia mwaka huu kwa kuendelea kufanya hizi kazi ambazo zimeandikwa hapo chini kwenye utekelezaji. Wamepeleka umeme kwanza kwenye uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na umeme kote nchini.
Mheshimiwa Spika, pia, tumeuona umeme vijijini, vitongojini, mahali fulani kwenye visiwa, kwenye vituo vya afya na maeneo mengine mengi. Labda tu niseme hapa kwamba nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa sababu mimi nilikuwa na vijiji 58 vilivyokuwa havina umeme, hivi ninavyozungumza leo Jimboni Busanda vijiji vyote vina umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja tu ninayobaki nayo ambayo naendelea kuiomba Serikali ni vitongoji. Nilivyoiona bajeti imepungua kutoka shilingi trilioni 3.0 kwenda trilioni 1.8 nikawa na mashaka. Nilitegemea hiyo bajeti iwe maintained yaani isipungue kwa sababu bado tuna vitongoji vingi.
Mheshimiwa Spika, ndugu zangu wa REA wanashindwa kusema tu, lakini ukweli ni kwamba wanahitaji fedha nyingi kwa sababu zaidi ya 40% ya vitongoji ndani ya nchi hii havijapata umeme. Kwa hiyo niombe sana Serikali pamoja na kazi nzuri iliyofanyika, ndugu zangu wa Wizara ya Fedha waone namna gani wanavyoweza kushughulika na hii REA. Itakuwa ni kitu cha ajabu kama kitongoji kimoja kina umeme kingine hakina na watu wanaishi ndani ya kata moja au ndani ya kijiji kimoja. Tutaanza kutengeneza mambo ambayo yanaonekana kama kuna kupishana na matabaka yatatokea. Kwa hiyo ni ombi langu kwamba tungeshughulikia vitongoji vyote vikaisha, REA wawezeshwe vitongoji vyote viweze kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia vizuri uzalishaji wetu (installed capacity) ndani ya nchi hii inaonekana kuna umeme wa maji unaotokana na maji, gesi asilia, mafuta na tungamotaka. Vyote hivi kwa pamoja ukiviangalia vimetuletea megawatt 2,138. Ukiangalia kiuhalisia tunaweza leo tukaridhika kwamba installed capacity ile inaweza kuwa inatupeleka kwenye hiyo megawatt 1,756 ambayo ndiyo tunaipata, lakini kiuhalisia ni kwamba tukiruhusu watu wote watumie umeme tunaweza kuona kama umeme tulionao huu ni kidogo sana. Hii ni kwa sababu tunakutana na power ratio ya mahali fulani, umeme unagawanywa ndiyo sababu tunaona kama mahali fulani tunaenda vizuri. Kuna watu ambao sasa wanatumia mitambo yao kuzalisha umeme ili kuendesha shughuli zao.
Mheshimiwa Spika, wote wakianza kutumia mashine ya kutumia umeme wa TANESCO, tutafika mahali tutagundua hiki tunachokipata sasa hivi ni kidogo. Kwa hiyo ni ombi langu tu kwamba tuendelee kuzalisha na kuanza kubuni vyanzo vingine vingi. Nimeona mahali fulani kwamba sasa tunakwenda kwenye dunia ya renewable energy, tunakwenda kwenye habari ya jua. Shinyanga pale tunaanza na megawatt 150, bado ni kidogo. Kuna mahali tunakwenda kuanza hydro-powers bado ni kidogo kwa sababu naona kabisa kwamba ndani ya miaka miwili baada ya watu kuufahamu huu umeme tunaweza kwenda kwenye megawatt 7,000 ambazo tutakuwa hatuna, tutarudi kwenye shida hii ambayo tulikuwa nayo hivi karibuni. Kwa hiyo nawapongeza kwamba chanzo kimoja cha Julius Nyerere chenye megawatt 2,115 kwa mashine moja tu au mbili, kimetupunguzia tatizo hili lakini tujiandae kuhakikisha kwamba tunapata uzalishaji mkubwa.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, nilikuwa napitia hali ya usafirishaji ikaonekana Mwaka wa Fedha 2022/2023, tulikuwa tumeshapita kwenye njia za usafirishaji takribani kilometa 6,363, lakini mpaka leo tunavyozungumza tumekwenda 7,745, maana yake tumeongeza njia za usafirishaji. Ukiangalia hali ya usambazaji tulikuwa na kilomita 168,548 na sasa tumeshakwenda kwenye 176,000, maana yake kuna mahali fulani tunakwenda. Kwa hiyo nimpongeze Mheshimiwa Waziri amekuwa mwepesi wa kufanya hizi kazi.
Mheshimiwa Spika, nilitegemea kabisa kazi za kiuhandisi hizi zingekuwa changamoto lakini, sasa anaonekana anajifunza haraka. Sasa ameshajua penstock, spillways utafikiri naye ni Mhandisi, lakini ni uwezo wake mkubwa wa kufanya haya mambo na dada yangu Mheshimiwa Judith naye ameingia hukohuko naye kama Mhandisi kumbe ni Mwanasheria. Kwa hiyo niwapongeze sana kwa kazi kubwa ambayo imefanyika. Nigusie kidogo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)