Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana hasa inavyogusa maisha ya Watanzania wengi kwa ujumla. Niungane pia na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na wataalam wote waliopo ndani ya Wizara hii. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa na sisi kama Watanzania tunaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulipitia kipindi kigumu hapa katikati cha changamoto kubwa sana ya umeme, lakini tumeona kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa nao na kazi kubwa ambayo wameifanya, leo hii changamoto ya umeme imekwisha. Lazima tuwapongeze sana kwa hili kwa kweli mpewe maua yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba uzalishaji umekuwa mkubwa bado sasa hivi nguvu kubwa sasa tuielekeze kwenye usambazaji pamoja na usafirishaji kwa sababu wananchi sasa hivi wao wanataka kuona umeme unapatikana. Leo tunawaambia kwamba uzalishaji kule upo wa kutosha mpaka kuna ziada, lakini wanapoona baadhi ya maeneo umeme unakatika wanakuwa hawaelewi kwa sababu tu aidha, changamoto ipo kwenye usafirishaji hasa kwenye miundombinu au kwenye usambazaji. Kwa hiyo niombe sana tutenge fedha na bajeti ya kutosha kwenye usafirishaji na kwenye usambazaji ili wananchi wetu waweze kunufaika sana na umeme huu.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwenye upande wa REA. REA wanafanya kazi kubwa, sisi sote tumekuwa mashahidi tunawapongeza wao na DG wao kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya. Tunaomba aongeze nguvu hasa yale maeneo ya vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme na nguvu kubwa iende kwenye vitongoji ili wananchi wetu waweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, Wilayani kwangu Chunya bado nina changamoto, baadhi ya vijiji bado havijafikiwa na umeme na hapa tunapozungumza sasa hivi takribani kata tatu bado hazijapata umeme; Kata ya Lualaje ambayo ina vijiji viwili: Kijiji cha Lualaje na Kijiji cha Mwiji. Tayari miundombinu imeshafika pale na transformer imeshafungwa, lakini umeme bado haujawashwa. Wananchi wanauliza ni lini sasa umeme utawashwa ili waweze kunufaika na umeme huo kwa sababu wameusubiri kwa muda mrefu sana?
Mheshimiwa Spika, wakati mradi huu unapelekwa kwenye Kata hii ya Lualaje mwanzoni kwenye mipango hakukuwa na shule ya sekondari, lakini hapa katikati tumepata shule ya sekondari ambayo haikuwepo kwenye mpango wa kupeleka umeme wa REA. Niiombe sana Wizara na watu wa REA tuifikishie umeme Sekondari ya Lualaje ili na wenyewe waweze kunufaika. Tufanye wakati huu ambao mkandarasi bado yuko site ili na wananchi hawa waweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, kata nyingine ni Kata ya Mafyeko pamoja na Kata ya Kambikatoto. Hizi kata zote mbili bado na zenyewe hazijaweza kufikiwa na umeme kwa sababu mkandarasi aliyekuwepo mwanzoni alipata changamoto na mkataba wake ukawa umesitishwa na taarifa nilizokuwa nazo ni amepatikana mkandarasi mwingine. Naiomba sana Serikali impe nguvu mkandarasi huyu hapa, tumsukume kwa nguvu kubwa aweze kukamilisha mradi huu kwa wakati kwa sababu wananchi wa Kata hizi za Mafyeko pamoja na Kambikatoto wana uhitaji na wanausubiri umeme huu kwa nguvu kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na umeme huu kwenda kwenye vijiji hivi, sisi pia kule Wilaya ya Chunya ni wachimbaji. Tuna mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji hasa wachimbaji wadogo. Mradi unakwenda lakini speed yake mpaka sasa hivi toka mradi umeanza takribani uko kwenye 28% mpaka 30%. Naiomba sana Serikali tuweze kupeleka fedha za kutosha ili tuweze kuwafikia hawa wachimbaji wengi zaidi ili umeme huu uweze kufika katika maeneo yao na wao waweze kunufaika na uzalishaji hasa wa madini ya dhahabu na uweze kufanyika vizuri zaidi ili tuongeze pato la Taifa kwa upande wa uchimbaji.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Chunya tunapata umeme, lakini umeme tunaoupata ni mdogo kwa sababu kwenye chanzo cha umeme cha Mwakibete (Substation Mwakibete) mpaka Chunya Mjini ni umbali takribani kilomita 150. Kutoka Chunya Mjini mpaka mwisho wa wilaya yetu Kambikatoto takribani kilomita 300 zinafika. Kwa hiyo tunaiomba Serikali ilikuwa ina mpango wa kupeleka substation maeneo ya Makongolosi pale, tunaomba ipate fedha ipeleke substation pale ili wananchi hawa waweze kupata umeme mkubwa na wa uhakika na uzalishaji uweze kuendelea vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumze suala la Gesi la CNG. Sisi kama Kamati tulitembelea maeneo kadhaa Dar es Salaam ambako kuna vituo kadhaa vya kujaza hii gesi kwenye magari. Mwitikio wa wananchi sasa hivi umekuwa ni mkubwa sana, lakini changamoto kubwa sana ambazo tumeziona ni mbili. Jambo la kwanza, gharama kubwa sana ya kubadilisha mfumo huu kuweka mfumo wa gesi kwenye magari. Tunaiomba Serikali ione namna ambavyo inaweza ikapunguza kodi kwenye vifaa hivi vya gesi ya kwenye magari ili wananchi waweze kupata au kufunga mifumo hii kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuhakikisha kwamba vituo hivi vya kujaza gesi vinaongezeka. Tumesikia kwenye hotuba mpango wa Serikali ni kuongeza vituo, lakini tunaomba sana Serikali ifanye jambo hili kwa nguvu kubwa na kwa uharaka kwa sababu uhitaji wa wananchi ni mkubwa. Tulikaa pale tukaona watu wanakaa saa mbili mpaka tatu kwenye foleni ya kujaza gesi. Kwa kweli kwenye uchumi wa nchi, mtu kukaa saa mbili kusubiri kujaza gesi, hili jambo halikubaliki. Tunaomba tuone namna ambavyo Serikali italichukua jambo hili kwa udharura wake. Tuongeze vituo hivi ili wananchi hawa wasikae muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa sasa tunaenda kutumia gesi kwenye magari tuanze na sisi, kwenye magari ya Serikali. Serikali kila siku imekuwa ikituambia, lakini utekelezaji wake unaenda kwa kusuasua. Serikali inapoagiza magari yake sasa hivi yaje kwenye mfumo wa gesi moja kwa moja ili wao ndiyo wawe wa kwanza kutumia hii gesi. Wakitumia wao hii gesi itawezesha sasa hata hawa wawekezaji binafsi ambao wanaenda kufungua hivi vituo watakuwa na uhakika wa magari kuwa mengi hasa magari ya Serikali ambayo yatajaza kwenye vituo vyao.
Mheshimiwa Spika, pia pamoja na kwamba sasa hivi tumeanza hasa pale kwa Dar es Salaam, sasa twende kwenye miji mikubwa ikiwemo Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huo mfumo wa gesi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)