Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi uliyonipa ili nami niweze kuchangia hii hotuba muhimu ya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, masuala ya kiujumla ambayo niliyoyaona, moja ni kwamba taarifa ya Waziri imeacha baadhi ya mambo muhimu sana ambayo Waheshimiwa Wabunge tulitaka tuyasikie, lakini taarifa ya Kamati ibara ya 2.4 na kielelelzo cha tatu imeripoti mkanganyiko wa takwimu. Kwa hiyo, ni vizuri na yenyewe hizo takwimu za mapokezi ya fedha zikafanyiwa marekebisho ili kuweka kumbukumbu sawa.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa LNG umetangazwa kwamba mkataba wake sasa rasimu yake ipo tayari. Sasa ni muhimu sana, kwa sababu tulishafanya makosa huko nyuma. Mradi mkubwa kama huu wa LNG tusifanye makosa tena. Kama rasimu ya mkataba imekamilika, tufuate procedure zilizowekwa, kwa maana ya kwamba mkataba huo kuletwa hapa Bungeni kwa mujibu wa Sheria ya TEIT pamoja na Sheria ya The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act, 2017 inavyotaka.
Mheshimiwa Spika, pia nimeona utekelezaji wa mradi wa ECOP, ule mradi wa bomba, ambapo shilingi milioni 289.74 tayari Serikali imeshalipa kwenye mradi huo na tayari mradi huo umefikia 27.1%. Hiyo ni kazi nzuri ambayo Serikali inapaswa kupongezwa.
Mheshimiwa Spika, nimeona pia kwenye eneo la Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao ni kama unaelekea mwisho sasa na malipo ni kama yameisha. Wenzangu wamesema hapa kwamba mpaka sasa hivi malipo ya CSR shilingi bilioni 270 hayajalipwa, na fedha kwa ucheleweshaji shilingi bilioni 822 haijalipwa.
Mheshimiwa Spika, iwe mchana iwe jioni hizi fedha za Watanzania lazima zilipwe. Hata kama kuna sarakasi kubwa kiasi gani, hizi fedha za Watanzania lazima zilipwe. Waziri leo atuambie hizi shilingi bilioni 270 za CSR na shilingi bilioni 822 za ucheweshaji wa miaka miwili na nusu uliofanywa na kampuni hiyo wahakikishe kwamba zimelipwa kwani fedha hizo ni za Watanzania, na hapo hatutakubali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa REA, vitongoji vyangu vingi (vitongoji 15) bado havijaanza; kule Mumunu, Dabwisha, Machimu na Mwanani miradi hii bado haijaanza. Mheshimiwa Waziri tafadhali hii miradi sasa ianze ili wananchi katika vitongoji vyote kama tulivyonuia kama Serikali wapate.
Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumzia hali ya upatikanaji wa umeme na wamesema kuanzia Januari umeme umeanza kuimarika. Napongeza sana jitihada hizo, na hasa Mheshimiwa Waziri alipoingia tukaanza kuziona jitihada za makusudi. Kwanza, usimamizi makini wa kuhakikisha kwamba Bwawa la Mwalimu Nyerere linakamilika, na sote tumeshuhudia.
Mheshimiwa Spika, vilevile tukaanza kumwona anaenda kwenye ziara moja kwa moja kwenye maeneo yote ya uzalishaji wa umeme. Tukaanza kuona jitihada hizo, akaanza kufuta mpaka likizo ya watumishi wake na yeye mwenyewe likizo za sikukuu ili kuhakikisha kwamba umeme unapatikana.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na sarakasi nyingi sana pale TANESCO. Kwa mfano, waliajiriwa watumishi sita bila usaili wowote, bila ushindani na bila hata kutangazwa na hawajulikani hata waliletwa kutoka wapi na waliletwa kwa ajili ya nini kwenye shirika muhimu kama lile, na hasa hao ndio waliokuja kuanza katakata ya umeme ambayo ilikuwa inafanyika pale TANESCO.
Mheshimiwa Spika, pia hata EWURA yenyewe haikutekeleza majukumu yake sawasawa katika kuisimamia TANESCO katika kuhakikisha kwamba umeme unapatikana. Sasa hizo zote ni sarakasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumwondoa Waziri wa Nishati aliyekuwepo hapo, kumwondoa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO na kuvunja Bodi ya TANESCO na kukuteua. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kukuteua wewe Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko kuwa Waziri wa Nishati ambaye umeonesha uadilifu na unyeyekevu mkubwa sana kwa wananchi kwa kuwajibika kikamilifu. Tunataka Mawaziri wa aina yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tunataka kazi moja tu, Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba sasa anashusha bei za umeme. Bwawa limekamilika, sasa tunataka bei ya umeme ishuke. Adhibiti hitilafu za umeme zinazotokea na wananchi walipwe fidia haraka hitilafu zikitokea, na pia sababu nyingine zilizokuwa zinasababisha katakata ya umeme ziweze kudhibitiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa SONGAS umefika mwisho. Miaka 20 imefika na hivyo mkataba huu umefika mwisho. Waziri hajatujulisha hatima ya mkataba huu ni nini? Hata hivyo, tunajua bei ya umeme ilikuwa kubwa sana. SONGAS ilikuwa inaiuzia TANESCO umeme kwa bei kubwa. Pia hawa watu walianza hata kutu-charge. Hata wakifanya ukarabati wa visima, wanatu-charge. Mpaka sasa hivi wanatudai shilingi bilioni 107 za kutu-charge kwa ajili ya matengezo, kazi ambayo haipo kwenye mkataba.
Mheshimiwa Spika, sasa tunataka tuelezwe, huu mkataba kwa sababu umefika mwisho, maelezo ya utekelezaji wake yakoje? Tusije tukafika tukakuta mkataba tena umerejewa wakati ulikuwa na migogoro yote hii. Mkataba uletwe kwenye Kamati husika, uletwe hapa Bungeni ili tuone tathmini ya utekelezaji wake kabla ya maamuzi mengine yoyote yale ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Erolink. Hii Kampuni ya Erolink ndiyo ambayo imepewa jukumu kwamba wananchi wakitaka kupiga simu wapige kwao kwa ajili ya miito ya simu hasa simu hizi za dharura. Wananchi wetu wameonewa sana na huu mkataba wa TANESCO na Erolink. Kwanza haifahamiki huyo Erolink alitoka wapi, na maamuzi yakafanywa ya kuondoa vituo vya miito ya simu kwenye mikoa, yakawa centralized pale Dar es Salaam?
Mheshimiwa Spika, sasa hivi wananchi wanalazimika mpaka wapige simu Dar es Salaam halafu ndipo wapokelewe na ndipo waende kutatuliwa hitilafu zao za umeme. Watu wameunguza vifaa vyao, viwanda vimeungua, nyumba zimeungua, huduma mpaka upige simu Dar es Salaam; na uwezo wa hiyo Erolink mpaka sasa hivi kupokea simu ni 30% tu. Maana yake ni kwamba 70% yote wananchi hawapati huduma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa siku wananchi wanapiga simu 70% hawapati huduma. Unategemea nini? Upige simu kiwanda kinaungua, nyumba inaungua! La pili kulazimika kulipa. Unalipia huduma kwa wateja.
Mheshimiwa Spika, hivi kwanza tuelezeni, hizi fedha anapewa nani? Ukipiga simu Vodacom au kampuni yoyote ile ya simu kwenye mambo ya dharura hakuna malipo, Polisi hakuna malipo; lakini leo wananchi wanalipia. Usiku wa manane nyumba inaungua, utapata wapi fedha kwenye simu? Haya yamewezekana na hiyo Kampuni ya Erolink hatujui nani kaileta na ni kwa sababu zipi?
Mheshimiwa Spika, lakini siri zinavuja...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja tu.
SPIKA: Sekunde thelathini.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, naomba sana maamuzi kwanza huu mkataba wa Erolink uvunjwe haraka, na hivi vituo virejeshwe kwenye maeneo ya awali na vifanye kazi kama vilivyokuwa vinafanya zamani. Tuelezwe, leo tunaona....
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Ooh, ahsante.