Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa wachangiaji kwa siku ya leo. Naomba kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya ili niweze kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kipekee niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anafanya kwa Taifa hili. Pia naomba kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa na nzuri, na ametupa maneno ya kuiga kwamba Watanzania hawataki maneno, wanataka vitendo, wanataka umeme. Naomba nipongeze kwa moyo wa dhati. Nina uhakika hicho ambacho Watanzania wanakitarajia kimeanza kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa katikati tumepitia katika wakati mgumu sana ambao umeme ulikuwa unakatikakatika, lakini leo hivi tunavyoongea hali ya umeme inazidi kuwa nzuri hasa baada ya hilo bwawa ambalo lingeweza kujaa baada ya miaka mitatu, lakini msimu mmoja tu wa mvua umetosha, huo ni ufundi wa Mwenyezi Mungu kwamba tunavyopanga sisi, yeye akitaka ya kwake yanakuwa kwa urahisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuanza kupatikana kwa umeme wa uhakika lazima kuende na mipango ambayo lazima tuharakishe na hususani ni mpango wa kuunganisha Mkoa wa Rukwa pamoja na Mkoa wa Katavi kwenye Gridi ya Taifa. Katika mpango uliokuwepo hapo awali, walikuwa wametarajia kwamba uunganishwaji wa mikoa hii kwenye Gridi ya Taifa ungefanyika baada ya kipindi cha miezi 18. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, kwa ajili ya upatikanaji wa umeme kwa wingi, huo mpango uliokuwa umewekwa kwamba tuunganishwe baada ya miezi 18, ni vizuri Serikali mpitie utaratibu huo, muuharakishe kwa sababu haileti tija pale ambapo tunaambiwa kwamba tunalazimika kuzima baadhi ya mitambo kwa sababu umeme ni excess, lakini kuna maeneo ambayo bado hatujajiunga kwenye Gridi ya Taifa na umeme unaendelea kukatika.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni muda mrefu tumekuwa tukipata umeme kutoka kwa jirani zetu Zambia na kwa vile Mungu alivyokuwa fundi, wale waliokuwa wanatupatia umeme wa ziada, leo wao wana ukame mkubwa kiasi kwamba hakuna uhakika wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu kwamba it is high time ile mipango muipitie kwa upya ili tuunganishwe na gridi ya Taifa. Maana umeme ni maendeleo na kwa vyovyote vile, ili tuwe na uwekezaji wa kutosha, tuwe na viwanda vya kuchakata mazao, ni pale ambapo watu watakuwa na uhakika wa umeme kupatikana katika mikoa hiyo miwili ambayo nimeitaja na mikoa mingine yoyote ambayo haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia busara hiyo hiyo ambayo ilitumika wakati tukiwa na upungufu wa umeme, tukalazimika kupata umeme kutoka kwa nchi Jirani. Sasa katika mpango wa kuanza kuuza umeme, ili tupate dola, ni vizuri Serikali mkaanza kufikiria wale waliokuwa wanatuuzia sisi, tubadilishe tuwauzie kwa sababu tuna umeme wa ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza hayo maeneo mawili, naomba niende upande wa REA. Katika mikoa ambayo kuna upelekaji wa umeme vijijini kwa maana ya REA kwa kusuasua ni pamoja na Mkoa wa Rukwa; na pia wamesema wenzangu waliotangulia kuhusu Katavi na hata Mkoa wa Kagera, na sababu ni moja tu. Ukitafuta kwa nini umeme vijijini katika maeneo hayo umepelekwa kwa kusuasua, katafute mkandarasi ni nani? Utakuta mkandarasi ambaye yuko Mkoa wa Rukwa, yuko Katavi huyo huyo, ndio unaenda kumpata kwenye Mkoa wa Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika utafiti ambao nimefanya, nini changamoto ambazo nimegundua? Mkandarasi huyo ameshindwa kufuata mpango kazi ambao walikuwa amekubaliana na mwajiri wake, lakini kama hiyo haitoshi, ana magenge machache sana ya wafanyakazi na hata wafanyakazi alioajiri, hawalipi mshahara kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, wakati huo huo, ana magari machache sana ambayo yanatumika katika kusambaza nguzo. Mkandarasi huyo hata akipelekewa taarifa na Mshauri Mwelekezi ha-respond, akitumiwa barua, hajibu na amekuwa akiongezewa muda kila wakati. Ifike mahali pale ambapo mkandarasi hatimizi wajibu wake kwa wakati, yale makubaliano ya kimkataba ikiwa ni pamoja na performance bond, itumike kukata ili iwe fundisho kwa wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo vijiji ningependa Mheshimiwa Waziri uhakikishe kwamba umeme unaenda ni Kijiji cha Kapele, Kipwa, Tunyi, Kachele, Safu, Kifone, Ilango, Katapulo, Jengeni, Nondo na Mozi. Haipendezi pale ambapo wengine wanaongelea habari ya vitongoji kupelekewa umeme, sisi tunaongelea vijiji.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo Serikali yetu ilifanya vizuri katika operation vijiji ni Mkoa wa Rukwa. Ukienda vijiji vyetu center ni sawasawa na mijini. Kwa hiyo, tunaposema upelekwe umeme kwenye vijiji hivi, tunamaanisha uhitaji ni mkubwa sana. Ni vizuri Serikali ifike mahali ambapo baadhi ya wakandarasi mvunje nao mikataba, mtafute wakandarasi ambao watahakikisha kwamba umeme unafika kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ni vizuri pia tuiombe Serikali, baada ya tamko la Makao Makuu kuwa Dodoma, nayo iangaliwe katika matumizi ya gesi kwenye magari. Nami naomba nisisitize kwamba iko haja ya kuhakikisha kwamba vituo kwa ajili ya ku-convert magari ambayo yanatumia diesel na petrol sasa yaanze kutumia gesi ambayo inatoka Tanzania. Hatuhitaji dola, tunahitaji shilingi ili tuweze kutumia gesi yetu na itasaidia katika kupunguza matumizi, na hasa Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)