Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Nishati. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutufikisha siku ya leo na nikapata muda wa kuchangia bajeti hii. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu kipenzi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi ambazo anaendelea kuzifanya katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza Waziri wa Nishati, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri, Mheshimiwa Judith Kapinga, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na viongozi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kuchangia kuhusu umeme vijijini (REA), katika Mkoa wa Kilimanjaro. Katika miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia, tumepokea shilingi bilioni 79.683 ya kutekeleza miradi minne katika Mkoa wa Kilimanjaro. Mradi wa kwanza ni kusogeza miundombinu kwa wateja ambapo tumepokea shilingi bilioni 16.048. Mradi wa pili ni kuimarisha nguvu za umeme, shilingi bilioni 12.385. Mradi wa tatu ni matengenezo ya miundombinu, shilingi bilioni 16.538. Mradi wa nne ni kuunganisha umeme kwa wateja wapya, shilingi bilioni 25.379. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika miradi yote, mradi wa nne ambao ni mradi wa kuunganisha wateja wapya umechukua fedha nyingi sana, shilingi bilioni 25. Maana yake ni nini? Ina maana kwamba Watanzania wengi wanaoishi maeneo ya vijijini wamehamasika kupata umeme. Naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri na fedha nyingi ambazo tumezipata katika mkoa wetu wa Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, tunazo changamoto kidogo. Katika Mkoa wa Kilimanjaro tuna vijiji 519, vilivyopata umeme ni 506, vilivyobaki ambavyo mpaka leo havijapata umeme ni vijiji 13 na vijiji hivi 13 vinatoka katika wilaya mbili tu, Same pamoja na Mwanga. Same Mashariki ni vijiji vitano, nitavitaja: Kijiji cha Kirore, Kirongwe, Lugulu, Kanza na Makokane. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Same Magharibi ni vijiji vitano pia; Kijiji cha Gavao Ngarito, Ruvu Mbuyuni, Chekereni, Gundesinde na Imugiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado vijiji vitatu vya Mwanga; Kijiji cha Mwanga Karamba, Mwai, na Pangoro. Inasikitisha sana. Inasikitisha kwa sababu wenzetu sasa hivi wanaongea habari ya vitongoji, lakini sisi vijiji 13 katika wilaya mbili havijapata umeme. Maana yake ni nini? Wananchi wanadhoofika, wanashindwa hata kufanya shughuli za kuongeza uchumi wao na kwa Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo sitaunga mkono hoja. Nataka Waziri akija atuambie tatizo liko wapi? Shida iko wapi? Ni ile milima ya upareni wanashindwa kupanda au ni nini? Sitaunga mkono hoja na nitashika shilingi ya Waziri kama hatanipa majibu ya kuridhisha. Wale wananchi wanataka kusikia kwa nini wao wanashindwa kufanya biashara? Kwa nini wao wanashindwa kujiendeleza kiuchumi? Leo nitashika shilingi ya Waziri kama sitapata majibu ya kuridhisha ni kwa nini vijiji 13 mpaka leo havijapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, nitaongea kuhusu changamoto ya wakandarasi. Baadhi ya wenzangu wameongea, kuna wakandarasi wengine ambao wameshika kazi nyingi na unakuta kuna maeneo mengine sasa kutokana na wingi wa kazi, kazi nyingine zinazorota. Inaamanisha kwamba wananchi wanachelewa kupata umeme kwa muda.

Mheshimiwa Spika, nitolee mfano katika vitongoji 24 vya Mwanga. Mkandarasi juzi amekaa na uongozi na akakiri kwamba amechelewesha kutekeleza mradi ule wa vitongoji 24 Mwanga kwa sababu alikuwa na kazi nyingine Tanga. Namwomba Waziri, wanapofanya mipango hiyo ya wakandarasi waangalie na mkandarasi. Kwanza nguvu ya mkandarasi na kazi alizonazo ili kugawa kazi ziweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya changamoto hiyo, nitaongelea kuhusu changamoto ya nguzo za zamani. Ni ukweli tumepata mvua nyingi sana na maeneo mengi nguzo zetu za zamani zimechoka, maeneo ambayo yana mchwa mpaka zimepinda, ambayo ni hatari hata kwa wananchi. Naiomba Serikali ihimize kuhakikisha kwamba nguzo za zege za kisasa zinasambazwa katika maeneo mengi hasa maeneo ya vijijini na maeneo ambayo yana maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ambayo ipo ni kuhusu transformer. Mwanzo kabisa tulivyoanza zoezi la umeme vijijini nakumbuka Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli alikuwa anasema hapa hakuna Mtanzania ambaye atashindwa kufanya. Tulikuwa tunasema jogoo mmoja tu unaweka umeme ndani ya nyumba.

Mheshimiwa Spika, wakati ule watu wengi walikuwa hawajajiunga, sasa hivi watu wengi wamejiunga na umeme, wamehamasika, wameona faida ya kuwa na umeme. Vijana wengi badala ya kukimbilia mijini, sasa hivi wako vijijini. Nitatoa mfano, mimi natoka katika Jimbo la Same Mashariki, katika Kijiji cha Gonja Maore, kuna transformer ambayo imezidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule kwetu kipindi kama hiki tunavuna mpunga, vijana wengi wamenunua mashine zao za kisasa wanasaga mchele na kupeleka katika mikoa mbalimbali. Inasikitisha kwa sababu unakuta kutwa nzima mashine hazifanyi kazi kwa sababu umeme ni mdogo. Naiomba Serikali ijaribu kuangalia, kutokana na hali ambayo sasa hivi wananchi wengi wamejiunga, waongeze nguvu katika vituo vya kuongeza umeme. (Makofi)

(Hapa kengele Ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Wooi! Haya, ahsante. (Makofi)