Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kibali hiki cha pekee alichonipa kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuchangia Bajeti ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, binafsi nakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko na Naibu Waziri wako wa Nishati kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya kwa Watanzania. Kumbe inawezekana Tanzania bila kukatika umeme chini ya uongozi wako na chini ya uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumwomba Mheshimiwa Waziri kwamba kwa upande wa Jimbo la Ushetu, tuna vijiji 112 lakini vijiji 112 vilivyopata umeme mpaka sasa ni vijiji 86. Tuna upungufu wa vijiji vyetu 26 havijapata umeme. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, wananchi wa Ushetu wanahitaji umeme, wananchi wa Ushetu ni wakulima, kila wanapopata mazao yao wanahitaji waweze kufunga mashine. Sasa tunapokosa umeme kwenye vijiji 26, inakuwa ni shida.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye vitongoji vyangu 554 tutapata umeme lini? Niendelee kumwomba sana Mheshimiwa Waziri, kuna vijiji vyangu viwili vimesahaulika, havijaingizwa kabisa kwenye mpango. Kuna Kijiji cha Kalama ambacho kipo Kata ya Kinamapula, kuna Kijiji cha Bukale ambacho kipo Kata ya Bulungwa, vilisahaulika kwenye mradi, naomba vijiji hivi viweze kuingizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliahidiwa hapa wakati wa swali langu la msingi kwamba tutajengewa kituo cha kupoozea umeme katika Halmashauri ya Ushetu, ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu mwenyewe hapa kwamba kitajengwa katika Halmashauri ya Nyamilangano, katika Kijiji cha Nyamilangano lakini nimesoma bajeti nzima ya Wizara ya Nishati sijaona mpango huo.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba ahadi yangu hii iweze kutekelezwa kwa sababu wakati najibiwa swali langu, wananchi wa Ushetu walikuwa wanafuatilia na kusikiliza. Naomba hili suala liingizwe kwenye bajeti ili anapokuja kuhitimisha Mheshimiwa Waziri naomba nisikie kituo changu cha kupoozea umeme katika Halmashauri yangu ya Ushetu. La sivyo, nitaondoka na mshahara. Nikiondoka na mshahara ndugu yangu naenda kwenye tumbaku huko, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu huwezi kunipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisimama hapa kusema kwamba eneo la Kahama, Wilaya ya Kahama yote na majimbo yake matatu yanazungukwa na mbuga, sisi hatujawahi kupata hizi nguzo za zege na majaruba haya, hawa ndege weupe wakianguka tu kwenye nguzo, nguzo inadondoka. Wilaya ya Kahama inakosa umeme, halmashauri zake zote zinakosa umeme.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2023 nilisema hapa kwamba tunahitaji Mkoa wa Ki-TANESCO Kahama kwa sababu ya makusanyo, lakini pia na shughuli za kibiashara zinazofanyika katika Wilaya yetu ya Kahama. Wilaya ya Kahama ina majimbo matatu; Wilaya ya Kahama ina makusanyo makubwa sana kwa upande wa TANESCO. Ndiyo maana hata mwaka 2023 kwenye bajeti nilisema, mtakapotupa Mkoa wa Ki-TANESCO makusanyo kwenye Serikali yetu yataongezeka.

Mheshimiwa Spika, leo tu pamoja na kwamba na umeme wa kuzimazima hivi, umeme unakatika, Kahama inakusanya zaidi ya shilingi bilioni 5.6 kwa mwezi upande wa TANESCO. Sasa kwa miezi mitatu iliyopita wilaya tumekusanya zaidi ya shilingi bilioni 15,600. Sasa kwa nini tusipewe Mkoa wa Ki-TANESCO ili Halmashauri ya Msalala iweze kuwa Wilaya na pia Ushetu iweze kuwa Wilaya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kuomba, Wizara itakapokuja kuhitimisha, waje na majibu ya lini watatupa Mkoa wa Ki-TANESCO kwa upande wa Kahama? Tunaomba Mkoa kwa sababu, hata Manispaa ya Kahama tu makusanyo yake, ukiangalia hoteli kubwa zilizopo Kahama ni zaidi ya 11, nenda viwanda vidogo vidogo vilivyosajiliwa ni zaidi ya 491, nenda kwenye biashara Kahama zilizosajiliwa ni zaidi ya 7,680. Kwa hiyo, ni eneo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa macho kwa upande wa TANESCO ili kukatikakatika kwa umeme Kahama ikome kama maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo mengine watu wameshasahau kukatikakatika kwa umeme. Mahali kwenye uchumi ambapo unajua kabisa kwamba nitaenda kukusanya mapato, kwa nini msielekeze nguvu? Kwani kutupa Mkoa pale wa ki-TANESCO ili maeneo haya yote ya viwanda; ukiangalia Msalala ina wachimbaji wazuri sana, vijana wanajiwekeza kwenye madini lakini umeme unakuwa wa kusuasua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukienda Ushetu tuna wakulima tunajenga viwanda vya kusindika tumbaku lakini umeme haupo. Tutengeeni mkoa Mheshimiwa Waziri ili tuweze kuzalisha na tuweze kuchangia mapato ya halmashauri yetu pamoja na nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni transformer; transformer za REA zinakuwa ndogo sana, dakika moja tu wananchi wanapofikiwa pale wanaweka mashine, transformer inakuwa inasumbua. Wananchi wangu wanalalamika sana kila eneo. Nenda Kata ya Ulowa wananchi wanalalamika, nenda Kata ya Bulungwa wananchi wanalalamika, nenda Kata ya Nyamilangano pale wananchi wanalalamika, kwa sababu ni maeneo ambayo wananchi wake wanawekeza sana kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, sasa wanapopata tu umeme pale, wanajenga mashine, wanaweka mashine ya kukamua, ya kusindika mpunga, wanaleta mashine ya kusaga, mashine ya kukoboa mchele, sasa umeme unakuwa ni wakukatikakatika. Kazi wanayofanya na sisi ni kututukana na kutulaumu pamoja na umeme wa REA, lakini transformer zote zinakuwa ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuomba Wizara itusaidie sana kwenye maeneo ya transformer, ziwekwe transformer kubwa ambazo zinahimili hali ya uchumi wa wananchi wa sasa. Kwa sababu Serikali ya Mheshimiwa Rais imeweka mapato makubwa sana na fedha zinaongezeka kwenye upatikanaji wa fedha kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye mazao, ruzuku ya mbolea imewekwa nyingi, wakulima wamelima kwa wingi, kila mahali wanahitaji wananchi wawekeze. Sasa bila umeme hatuwezi kuendelea. Kwa hiyo, niendelee kuomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati tupeni Mkoa wa Ki-TANESCO. Usipokuja tu na hoja hiyo sisi tunaondoka na shilingi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)