Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Nicodemas Henry Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini. Jambo la kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama tena ndani ya Bunge lako Tukufu ili niweze kuwawakilisha wananchi wangu wa Jimbo la Mbogwe…

SPIKA: Mheshimiwa Maganga, Waziri wa Madini asijekuwa amekusikia. Huyu ni Waziri wa Nishati, Madini ina Waziri mwingine…

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, sawa nimekuelewa, nilimzoea kwa sababu alikuwa Wizara ya Madini, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri wa Nishati ninakushukuru kwanza jinsi unavyotuendesha kama Taifa. Kwanza kabisa napenda kukupongeza kwani toka uteuliwe tumekuwa na neema, malalamiko kidogo yanaenda yanapungua kwa wananchi. Nakupongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, uniruhusu nianze kwa kutoa pole kwenye jimbo langu, mvua zilizonyesha jana watu wameporomokewa na majumba, wengine wamelazwa kwenye Hospitali ya Masumbwe. Kwa hiyo, nitoe pole sana kwa wananchi wangu ili kusudi Mungu awajalie na niwaombe viongozi wote wa dini kwenye Wilaya hiyo ya Mbogwe waweze kuwaombea watu warudi kwenye afya zao.

Mheshimiwa Spika, pia Waziri Mkuu ni salamu kwako, najua kuna Kamati ya Maafa pale Wilayani pamoja na Mkoani na nitoe wito tu waendelee kuwashughulikia wananchi wangu ili kusudi waweze kusaidiwa na kila linalohitajika kwenye ngazi ya Serikali waweze kupata haki yao, hao wananchi wa Mbogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo matano. Kwa vile mimi ni Mjumbe wa Kamati hii, niungane na wenzangu wa Kamati pamoja na Mwenyekiti na Makatibu wote jinsi tulivyoishauri sekta hii. Kwenye upande wa wilaya yangu, bado nina vitongoji 196 ambavyo vinahitaji huduma ya umeme. Mheshimiwa Waziri wewe unapafahamu, nikizungumza neno Mbogwe, vijiji vyote unavifahamu, hakuna sababu ya kuvitaja. Naomba sana uendelee kunisaidia mdogo wako ili kusudi wananchi waweze kupata neema kuwa jirani na wewe kwamba niko na wewe pamoja ili kusudi kwenye hii bajeti ya shilingi 1,000,800,000,000 iweze kuwa msaada kwa Watanzania wote hata Wanambogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwenye ukanda wetu tunalima mazao, kwenye ukanda wetu watu wana mashine za kusaga, ukanda wetu una watu wana ma-crusher wanahitaji huduma ya umeme na Majimbo yetu Wilaya ya Bukombe na Mbogwe hatuna transformer. Namwomba kaka yangu kupitia bajeti yako ya shilingi 1,000,800,000,000 uweze kutenga transformer ili umeme wetu uweze kutulia nasi tuwe na makusudi sasa ya kusema kwamba wilaya zetu zimetulia lazima tuwe na station za kupooza umeme ili kusudi watu waweze kuendesha viwanda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mbogwe ina vijiji 87, namshukuru Mheshimiwa Rais mpaka sasa hivi vijiji vyote vimefikiwa na umeme. Vilevile nawaamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tupitisheni hii bajeti bila wasiwasi, maana tunaona; mimi mwenyewe, tumefanya ziara mwaka uliotutuma kwenda nje kujiridhisha na kujifunza mambo fulani kulingana na sekta hii. Tulijifunza mengi, wenzangu wamesema.

Mheshimiwa Spika, ipo sababu ya kutupa nafasi ili kusudi yale tuliyoyaona India pamoja na Ethiopia kwa sababu tulipita huko, tuweze kuyafundisha hapa ili kusudi yafanyike kwa vitendo. Kwa sababu yanayowezekana India hata kwetu hapa yanawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye Hotuba ya Waziri amebainisha mambo mengi siwezi kuyapitia kulingana na muda, naiomba Serikali itoe pesa haraka kwa sababu tukizungumzia sekta hii ndiyo moyo wa Taifa letu. Pia lipo suala la mafuta, kwa vile Mheshimiwa Waziri anasimamia sekta hii, wasimamie kikamilifu. Mimi nakujua, uhakikishe kwamba unakomesha upandaji holela wa bei ya mafuta, kwa sababu mpaka sasa hivi lita ya mafuta ni shilingi 3,000 na kitu na maisha yanazidi kuwa magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umeme unaonekana sasa ni wa kutosha, mfikirie jinsi ya kushusha bei kwenye unit pamoja na kuwaunganishia watu umeme kwa sababu tuna umeme wa kutosha, hausumbui na mmetuthibitishia siku ya maonesho mbele ya Waziri Mkuu kwamba umeme tunao mwingi kuliko mahitaji. Sasa muone namna ya kuwapunguzia Watanzania matumizi ya umeme ili kusudi maisha yaweze kuwa na unafuu.

Mheshimiwa Spika, hali ya maisha ni ngumu ukijumlisha uendeshaji wa maisha kwenye sekta hii. Ukiangalia bei jinsi sasa hivi wananchi tunavyowaunganishia umeme, vipo vijiji tunavipelekea umeme kwa shilingi 300,000. Mimi naiomba Serikali iangalie upya turudi kwenye shilingi 27,000 kama zamani tulivyokuwa tunawaunganishia wananchi wetu ili kusudi waweze kufurahia matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa kwenye miji yangu 17, hii ya Masumbwe transformer zake Waziri zimeishakuwa. Sasa hivi wakiwasha umeme vifaa vyote vinavyofanya kazi kwa maana ya mashine za mpunga na ma-crusher pamoja na kadhalika na hii uunganishaji wa mita mbili tulioufanya mwaka 2023, umeme unaanza kusinzia.

Mheshimiwa Spika, hii inaonesha kwamba transformer zilizopo Masumbwe, Lulombela na Lugunga ni ndogo. Kwa hiyo, tunaomba transformer nyingine. Kama transformer zilizokuwepo ni za watts 50, basi ziende power meter 100 ili kusudi waweze kupata huduma nzuri kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni vituo vya mafuta. Sheria zetu zinazuia watu kuuza mafuta mitaani, lakini kiukweli na kiuhalisia ipo miji ambayo imeendelea kwa kasi. Hata kama ukiwa hapa Dodoma, ukitoka kidogo tu, kuna watu wanaouza mafuta kwenye makopo, hawana vituo; kwenye bajeti yako, tumezungumza na hata kwenye Kamati.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi vituo vya mafuta, wapewe vipaumbele hao wanaouza mafuta kwenye makopo huko vijijini ili kusudi wajenge wao hivi vituo na Serikali irahisishe, kusiwe tena nambo mengi mengi ya kufanya. Kwa sababu wapo wauza mafuta, wanauza humo humo vijijini na wana uwezo wa kufanya hiyo kazi. Serikali iweze kuwashika mkono kuwajengea hivyo vituo vya mafuta ikiwezekana hata kupanga, wapange wananchi wale ili kusudi wawe kisheria. Hii itaondoa mgongano kwa sababu sasa hivi askari utakuta wanakimbizana na wauza mafuta mitaani na hii ni kukosa mitaji, watu hawana mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali kupitia Wizara yako Mheshimiwa Waziri iende ikawashike mkono machinga, maarufu kama wapiga nyoka ili kusudi waweze kusaidiwa vituo vidogo kwenye kata huko ili waweze kuuza mafuta vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, naomba nikushukuru na kukupongeza wewe kwa jinsi unavyotuendesha na kutufundisha hapa Bungeni na unavyotupanga kwenda kwenye nchi mbalimbali kujifunza. Nataka nikuhakikishie, huwa unatutuma tunaenda kujifundisha kabisa, kile kilichopo tunakileta huku kuja kukifundisha. Kwa hiyo tutume tena mwaka huu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya ahsante sana.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: ...twende tukajifunze ili kusudi tuweze kulitoa Taifa letu hapa lilipo twende sehemu nyingine... (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga, shukurani. (Kicheko)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)