Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa nafasi hii. Napenda kuanza kwa kushukuru na tunashukuru ili tuweze kuomba tena. Kushukuru ni jambo la kibinadamu lililoelekezwa na Mwenyezi Mungu hata katika vitabu vyake vitukufu. Mimi najua Quran Tufuku kidogo kwa Kiswahili, Mheshimiwa Twaha anajua kwa Kiarabu. Yapo maandiko yanasema kwamba; "Waheshimuni na mwashukuru wenye mamlaka juu yenu na yule ambaye hamshukuru mtu, basi hata Mwenyezi Mungu hawezi kumshukuru."
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunavyosimama hapa tunamshukuru Mheshimiwa Rais na Serikali nzima ya Awamu ya Sita akiwemo Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa nchi yetu. Kawaida yetu sisi binadamu ni kusema wakati wa changamoto na mambo yanapokuwa mazuri hatusemi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati, amefanya ziara Kilombero. Nilikwenda hapo kwake nikakaa, nikamweleza kwamba Kilombero ina mgodi wa Kihansi na Mgodi wa Kidatu, lakini tunapata mgao wao wa umeme zaidi ya miaka miwili. Akaniitikia kwamba atalifanyia kazi na kweli amefika na helikopta, ametua Kidatu na Kihansi.
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, tangu amefika na ametoa kauli kwamba, ‘hapa kuna mgodi wa Kidatu, kwa nini kilometa mbili? Pia kuna kijiji na kuna eneo umeme hakuna. Hii siyo sawa.” Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba mpaka leo umeme haujakatika. Kwa hiyo, tunashukuru kwa kweli na tunaomba hali hii ya kupungua kwa umeme na kupungua kwa mgao, iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jenerali Ulimwengu ameandika katika kitabu chake; "Wakati mzuri wa kwenda kwa daktari ni wakati ambako unajisikia vizuri, mzima," unaenda unapima sukari na pressure. Ukishajua majibu yako, vipimo vinaonesha nini, ndiyo unamwambia daktari, nifanye nini ili niwe kama hivi nilivyo, sukari iwe kiasi hiki, au presha iwe kiasi hiki? Kwa hiyo, tunachoshauri ni kwamba hali hii inayoendelea ya kupungua kwa mgao wa umeme, vitu vinavyofanyika viwe maintained tuendelee kuwa na hali hii wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amefika katika maeneo yangu, kwa hiyo, nikizungumza hapa nafikiri utanielewa. Ule mto mkubwa unaozalisha Mgodi wa Kidatu ukijaa kama kipindi hiki cha mvua kwa kweli hali inakuwa mbaya sana katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Jimbo la Kilombero.
Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza hivi, nitakuwa niko njiani kwenda jimboni. Asubuhi ya leo Ifakara tumeamka na mafuriko makubwa kweli kweli. Makubwa sana, karibu nyumba za Ifakara Mjini zinaingia maji. Changamoto hiyo inatokana na Mto Lumemo ambao unaenda kumwaga maji katika Mto Kilombero ambapo Mto Kilombero unaenda kumwaga maji katika Mto Rufiji na Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Spika, Bwawa la Mwalimu Nyerere ukiangalia ramani 46% ya lile bwawa ni bonde la Kilombero na ukisoma, ukiangalia ramani ya bwawa Kata ya Kisawasawa na Kata ya Kiberege ziko kwangu.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali kuwa na mkakati mzuri, mkakati maalumu na mkubwa utaotokana labda na hiyo community social responsibility (fedha hizo) ama chochote kuhakikisha mto unaopita Ifakara Mjini unaenda kumwaga maji Mto Kilombero kwenda Rufiji unafukuliwa na unarudisha tuta lililowekwa na wazee zamani. Kwa sababu mafuriko ya Ifakara yanatokana na kingo, yaani kuna kingo zinajulikana kabisa zimebomoka, maji yanapita yanakuja kumwaga mjini. Zikirudishwa zile kingo na mto ukafukuliwa pale Ifakara Mjini, maji hayapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa sisi tuna 46% ya bwawa mpaka sasa hivi hata community social responsibility hata shilingi mia hatujapata. Soma ramani ya Kilombero Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu mwangalie ramani ile muone, Kilombero na Kata ya Kisawasawa na Kiberege ziko kwangu. Kwa hiyo, naomba kwa unyenyekevu mkubwa sana jitahidini tupate mradi mkubwa wa kufukua huu mto, tuachane na hii changamoto. Hali ya watu wetu ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka jana TANESCO walitusaidia kiasi kuhusu fedha na mkandarasi yuko pale hajaanza kufanya kazi. Nafikiri hajapewa advance payment kufukua huu mto. Kwa hela kidogo, hawezi kumaliza wote, lakini hata hivyo hajaanza kwa sababu ya changamoto za pesa.
Mheshimiwa Spika, mwisho, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ina vijiji 48, tunaomba vile vijiji vyote zaidi ya 16 ambavyo vimeambiwa walipe shilingi 300,000 na zaidi ya kuunganishiwa umeme warudishiwe ile shilingi 27,000 kama tulivyoomba. TANESCO wamefanya kazi kubwa, TANESCO Mkoa na TANESCO Wilaya kuhakikisha kwamba wanapata sifa hiyo...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga…
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)