Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, kwanza nami nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara hii, halafu nimpongeze Mheshimiwa Rais, mwaka 2020 alipokuwa anaingia, alikuta takribani vijiji vya Jimbo la Igalula 46 kati ya 58 havijapatiwa nishati ya umeme, lakini mpaka leo vijiji vimeshafikiwa na nishati ya umeme katika maeneo yote. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake wote, Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ya kumshauri Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninayo mambo machache sana ya Jimbo. Leo nitayauliza kwa maswali kwa sababu mimi ni mtu wa mwisho, nadhani na Mawaziri wanaanza kujibu. Mheshimiwa Naibu Waziri akianza kujibu ndiyo aanze kujibu maswali yangu.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, kule vijijini tulipeleka umeme sahihi, lakini kuna changamoto sana ya upatikanaji wa control number ili watu waingiziwe umeme, pamekuwa na shida sana. Sasa naiomba Serikali katika vijiji vyangu ambavyo inaonekana transformer ni ndogo hasa katika Kata ya Tura, Kijiji cha Tura, Izumba, Mwisole, Lutende, Kizengi na Lutoni, hebu naomba muongeze transformer ili wale wateja wapate umeme.
Mheshimiwa Spika, hii itakuja kutuletea utenganishi. Tuliwaambiwa wananchi tutawaunganishia umeme kwa shilingi 27,000, muda wenu ukiisha mtawapelekea kwa shilingi 320,000 wakati sisi Serikali ndiyo tuliwachelewesha kwenda kuwanunganishia. Kwa hiyo, naomba mwapelekee mapema ili waweze kupata nishati ya umeme kwa bei elekezi ya shilingi 27,000 kwenye hivi vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili tuliambiwa hapa na Mheshimiwa Waziri, bajeti iliyopita tulileta vitongoji 15 kila mmoja humu kwenye Bunge lako. Tukaandika, tukaenda stationery, tukachapa vizuri ili waweze kuona vizuri maana wengine miandiko siyo mizuri. Tukawachapia kabisa waone vitongoji kwa kitongoji. Hivyo vitongoji lini vitaanza kupelekewa umeme? Kwa maana tumeshaenda kusema, bajeti ya kwanza inaenda ukingoni na hii pia tunapitisha nyingine.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali ipeleke umeme kwenye vitongoji 15 vya Jimbo la Igalula ambavyo niliorodhesha ili waweze kufikiwa na nishati ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna changamoto ya mradi huu wa REA. Pia kuna changamoto kubwa sana ya transformer kuharibika. Leo hii tumekuwa na sisi customer care wa TANESCO, tunapokea message, tunapeleka kwa TANESCO ndiyo watufanyie ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kwa nini tunapeleka transformer na wakienda kuichukua, wanachukua zaidi ya miezi miwili au mitatu? Mwananchi anashindwa amdai nani? Wakienda TANESCO wanaambiwa huu mradi bado uko kwa Mkandarasi REA, akienda REA wanasema TANESCO anasubiri aje akague transformer. Wananchi hawatakiwi kujua TANESCO na REA ni nani, wanahitaji umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali, nendeni mkatatue matatizo ya ndani. Leo hii nimeambiwa kule Lutona kule transformer wamebeba, wiki iliyopita ilikuwa Isuli, kule transformer walibeba miezi mitatu mpaka ulivyoniletea banda hapa, nikambananisha Mkandarasi, TANESCO, kesho yake wakapeleka. Sasa tutaweza hivi!
Mheshimiwa Spika, umeme ukikatika, wakibeba transformer na mimi nianze kushinda tena kwa Waziri au kwa Naibu Waziri, nakaa pale nasubiri. Naomba sasa watumishi wa TANESCO waweze kufanya kazi yao kwa uhakika. Wananchi wanalalamika kule wakipata hitilafu, umeme unarudi kwa kuchelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine Serikali ina nia njema sana ya kutengeneza namba moja ya kupiga simu, wanasema one call center, wametengeneza mfumo mzuri sana lakini bado kuna changamoto. Leo mwananchi wa Igalula anapata tatizo sehemu inaitwa Makoyesengi anapiga Dar es Salaam. Mtu wa Dar es Salaam amekulia Kilimanjaro, unapomwambia Kijiji cha Makoyesengi katika kukiandika pale anakosea, anakuja kuwapa taarifa huku wanaanza kukitafuta Kijiji na kule wananchi hawapati umeme.
Mheshimiwa Spika, naomba hii hali ya kupiga namba moja mliyoiweka ni nzuri, lakini wekeni na namba kila Wilaya iwe na namba yake ili mwananchi akipata shida aweze kupiga kule kwenye Wilaya yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naona viashiria vya muda kwisha, niseme tu, naunga mkono hoja ya Wizara hii na bajeti hii. Ahsante sana. (Makofi)