Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo makubwa, lakini pia pongezi zangu zimwendee Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko na msaidizi wake wa karibu Mheshimiwa Judith S. Kapinga ambao hakika wanaitendea haki sana Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema jana kwenye mchango wangu wa kuzungumza kuhusu kusuasua kwa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA Mkoa wa Rukwa, hili jambo limekuwa na sintofahamu nyingi sana. Mimi binafsi kama Mbunge wa Jimbo la Kwela ambalo ndilo lina vijiji vingi ambavyo havijapata umeme kwa awamu ile ya kilometa moja nimefanya vikao vingi sana bila mafanikio yoyote ambapo mpaka sasa kati ya vijiji 40 vya Mkoa wa Rukwa ambavyo havijapata umeme, vijiji 17 vyote ni vya Jimbo la Kwela.

Mheshimiwa Spika, vijiji ambavyo havijapata umeme 17 katika hivi, vijiji 16 mkandarasi ameanza kufanya kazi na kimoja bado hajaanza kufanya kazi kabisa. Vijiji ambavyo mkandarasi bado hajavuta waya line kubwa amesimika nguzo tu ni Kisalala, Mnokola, Mititi, Ntumbi na Kitete.

Mheshimiwa Spika, vijiji ambavyo mkandarasi amevuta line na transfoma zimefungwa lakini havijawashwa ni Kazi, Tululu, Kilando, Mpona, Kapewa, Mtetezi, Zimba, Mnazimmoja Asilia, Mumbai, Kinambo na Kalumbaleza A. Kijiji ambacho hakijafanyiwa kazi kabisa ni Kijiji cha Liwelyamvula.
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kuunda timu yake ya uchunguzi ili kutambua chanzo cha huyu mkandarasi kususua kwa muda mrefu ni nini, lakini pia hatua za haraka zichukuliwe ili wananchi wa vijiji vyote 17 vya Jimbo la Kwela waweze kupata hii nishati muhimu ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto tulizopata mkandarasi huyu imelazimu binafsi kufuatilia pia maeneo mengine ambayo ametekeleza miradi bado taarifa zake sio za kuridhisha.

Mheshimiwa Spika, mradi huu unatekelezwa kwa ushirika wa Kampuni ya Pomy na Qwihaya, kwa taarifa za nyuma Qwihaya ni kampuni ya nguzo ila kwa sasa ni mkandarasi wa umeme pia Pomy ni mkandarasi wa umeme tangu kipindi cha nyuma hadi sasa. Mkandarasi Pomy alishawahi kupewa kazi ya mradi wa umeme kwa Mkoa wa Tabora, alitekeleza mradi huo kwa kiwango kisichokubalika na hakumaliza, lakini adhabu na lawama ilielekezwa kwa wafanyakazi wa TANESCO.

Mheshimiwa Spika, tangu anaanza mradi huu wa Rukwa kwa kushirikiana na Qwihaya, kumekuwa na migogoro kati yao isiyoisha na kusababisha mradi kutokwenda kwa wakati na kuwa na dalili zote za kutokamilika na huenda mgogoro ukawa ni sawa na kilichotekea Tabora. Tutambue kuwa mradi huu wa Rukwa ulianza kutekelezwa tarehe 9 Julai, 2021 na mwisho wa mradi huu ilikuwa ni tarehe 8 Januari, 2023 ambapo alikuwa amefikia 38%, REA wakaongeza muda wa miezi minne hadi tarehe 30 Aprili, 2023 ili kukamilisha mradi, lakini hadi mwisho wa mwezi wa nne utekelezaji wa mradi ulifikia 41%.

Mheshimiwa Spika, pia REA wameongeza muda wa kutekeleza mradi huu hadi tarehe 31 Oktoba, 2023 lakini bado kazi haikukamilika. Cha kusitisha aliongezewa tena muda mpaka Desemba, 2023 lakini bado kazi haikuisha, kaongezewa tena mpaka Machi, 2024 na kwa taarifa iliyopo sasa ameomba extension nyingine tena, jambo hili linasikitisha.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maendeleo haya ya kusuasua ya mradi kwa Mkoa wa Rukwa ni baada ya kutumia nguvu na kuwa na tabia ya kutembelea mradi mara kwa mara, kuwa na vikao vya kujadili mwenendo wa mradi na kuwa na maelekezo, lakini hakuna juhudu zozote za makusudi kuhakikisha mradi unakamilika.

Kuhusu hali ya kiusafiri katika Jimbo la Kwela kwa ofisi ya TANESCO; kwa upande wetu kama shirika Mkurugenzi Mtendaji alifanya ziara tarehe 5 Aprili, 2024 katika Mkoa wa Rukwa ambapo kati ya changamoto aliyopewa ni uhaba wa usafiri wa uhakika kwa wananchi wanaoishi katika Bonde la Ziwa Rukwa na alichukua na utatuzi unaendelea. Hivyo niendelee kumuomba Mtendaji Mkuu wa TANESCO kulifanyia kazi jambo hili kwani kwa sasa watendaji wa TANESCO hasa kule Bonde la Ziwa Rukwa wanatumia bajaji ambazo kutokana na miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwakilisha.