Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza kwanza kwa ushirikishwaji na wepesi katika ku-respond kwenye changamoto kila zinapojitokeza.

Mheshimiwa Spika, pili nawapongeza sana REA ambao tarehe 17 Aprili, 2024 walitoa mafunzo ya nishati safi ya kupikia kwa viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga ambapo pia mafunzo hayo yalihudhuriwa na viongozi wa dini na wazee maarufu wa Mji wa Mafinga. Katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Nishati Mbadala kutoka REA Bi. Advera Mwijage alitoa taarifa kuhusu hali ya umeme na hatua za utekelezaji wa hatua ya Ujazilizi 2C na pia alieleza fursa ya mkopo wa vituo vidogo vya mafuta somo ambalo liliwavutia wengi. Kwa ufupi mafunzo hayo sambamba na kugawa mitungi 350 ilifanikiwa sana na tunawashukuru sana REA.

Pili, naomba kushukuru utendaji mzuri wa Meneja wetu wa Tanesco Mhandisi Modest na timu yake, amekuwa very sharp hasa katika mawasiliano, sote kuanzia Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Madiwani tunashirikiana naye vizuri mno na kwa wakati. Ni kawaida yetu binadamu hasa sisi wanasiasa kutoa taarifa za kulalamika tu, lakini mtu akifanya vema tuna-mute. Hivyo nimeona ni vyema niseme kuhusu utendaji mwema na wa ushirikiano kutoka kwa Mhandisi Modest. Tunaomba kama anahama basi iwe vertical kwamba anapanda, lakini kama ni horizontal basi ni afadhali abakie Mufindi/Mafinga.

Tatu, suala la bei kwa sisi ambao kwa mujibu wa ile Sheria ya Mipango Miji inayosema kwamba eneo kutambulika kuwa mji kuna vigezo ambavyo kimsingi kuna maeneo bado ni vijiji, kwa sheria hiyo vijiji, hivyo vinakosa sifa ya kupata umeme kwa bei ya vijijini; mfano Mafinga ni mjini, lakini kuna maeneo ni vijiji kijamii na hata kiuchumi, kwa hiyo, bei ile ya shilingi 360,000 ni kubwa mno, nimeuliza maswali mara kadhaa, majibu ni kwamba kuna timu imeundwa kupitia maeneo hayo ili kuja na majibu ya way forward.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo suala hili sasa ni mwaka wa pili hakuna majibu, inawezekana kabisa hii bei ya shilingi 27,000 ikawa ni mzigo mzito kwa Serikali, hata hivyo mnaweza kuja na bei tofauti tofauti kulingana na maeneo, kwa mfano vijijini kabisa inaweza kubakia shilingi 27,000, lakini baadhi ya maeneo ambako ni kama peri-urban pawepo bei ambayo kidogo ni nafuu. Kwa mfano Mafinga kuna maeneo kama Ndolezi, Luganga, Mtura, Sao Hill na kadhalika inasomeka kuwa ni Mafinga Mjini lakini uhalisia wa kipato kwa maana ya uchumi na hata kijamii maisha ni ya kijijini, kwa sababu hiyo maeneo ya aina hiyo iwepo bei elekezi ambayo sio shilingi 27,000 na wala sio shilingi 360,000 lakini inaweza kuwa hata shilingi 100,000 kulingana na namna ambavyo hiyo timu ambayo tuliambiwa kuwa imeenda kufanya mapitio imejionea.

Mheshimiwa Spika, hitimisho; katika ujazilizi yapo maeneo imeonekana kuwa yapo mbali na HT hivyo vitongoji kadhaa Mafinga vitakosa fursa kwa sababu hiyo, hivyo naomba tuone uwezekano kupitia TANESCO kupata HT ili kuwezesha REA kupitia mkandarasi wa ujazilizi waweze kuendelea.

Mwisho, ni lini utekelezaji wa ahadi ya vitongoji 15 kila jimbo utaanza? Hii ni kwa sababu suala hili limo kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 na bado kama mwezi mwaka wa fedha kumalizika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.