Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kama walivyoanza wenzangu, nami naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwepo hapa toka siku ya jana tukijadili masuala mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa sekta ya nishati hapa nchini kwa manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana wewe mwenyewe kwa kutuongoza vizuri toka tumeanza mjadala huu. Kwa kweli kumekuwa na utulivu mkubwa na karibu kila Mbunge aliyepata nafasi ya kuzungumza kwa kweli amezungumza kwa niaba ya wananchi. Hii ndiyo dhana halisi ya uwakilishi, kwamba yale unayoyasoma kwenye mitandao au kuyasikia watu wakiyasema mahali fulani, ukiwasikiliza Wabunge wanayazungumza tena kisayansi kwa takwimu, kwa namba, kwa mifano na kwa historia ya changamoto ambazo tunapitia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nichukue nafasi hii niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kweli kwa michango yao mizuri ambayo wametupatia toka siku ya jana na leo tunapokwenda kuhitimisha hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unikubalie tena nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kweli mimi ukiniuliza pongezi zote tulizopata kwa wale waliosema wakatupongeza, tunastahili sehemu ndogo sana ya pongezi hizo. Anayestahili ni yeye mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati ananiteua kuwa Waziri wa Nishati aliniambia, katende kila jambo kwa nia njema, hilo la kwanza na la pili, umeme hautaki siasa, unataka matokeo. Akaniambia sema kidogo, tenda sana, kwa sababu ukisema sana usitende mwisho wa siku kuna mahali utajikwaa na utadaiwa kwa kauli yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msemo mmoja mimi nilikuwa siufahamu unasema; “Aliyenyamaza hajuti,” alinifundisha yeye. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ualimu wake, maelekezo yake na namna ambavyo amekuwa na kiu ya kuona Watanzania wanapata umeme na changamoto wanazopitia tunazimaliza kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nimshukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwa maelekezo yake, miongozo yake na usimamizi wake, hasa kwenye Sekta Ndogo ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo yeye Ofisi yake ya Makamu wa Rais inasimamia masuala haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwani toka nimeingia ofisini kwake, amekuwa mwalimu kwangu, amenifundisha mengi. Nataka nimhakikishie hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba, nitaendelea kuwa msaidizi wake mtiifu ninayefuata miongozo yake wakati wote.

Mheshimiwa Spika, kama mnavyomjua Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni mtu rahimu, ambaye hakunyimi maarifa ambayo anayafahamu, lakini hachoki kukukosoa mahali ambako anadhani huendi sawasawa. Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru sana, sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nimshukuru sana Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Judith Kapinga. Huyu, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, pamoja na kwamba ni Naibu Waziri wa Nishati, mtakubaliana nami kwamba sekta ya nishati ameifahamu kwa muda mfupi sana na anajifunza kwa haraka sana. Mheshimiwa Judith Kapinga ni mtu ambaye anasikiliza kila aina ya mtu na hata ikitokea mtu mahali fulani akamwambia lugha ya ukali, ana quality moja ambayo wengi hatuna, anajua kujizuia. Nakupongeza sana Mheshimiwa Judith Kapinga, umekuwa msaidizi bora kwa Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Judith Kapinga amekuwa akiibua vitu vingine wakati mwingine mimi sivifahamu, lakini anakiibua ananiambia kuna hiki cha kufanyia kazi Waziri, tukifanyie kazi. Ninaona fahari kubwa sana kufanya kazi naye na ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa msaidizi ambaye ni Mheshimiwa Judith Kapinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana sana wadau mbalimbali wa sekta ya nishati. Wengi tuliwaalika waje; wadau wa maendeleo, wakandarasi, kampuni mbalimbali zinazoshughulika na masuala ya nishati, kampuni za mafuta, gesi asilia na kadhalika. Wote hawa wamekuwa na mchango mkubwa kwetu na utakumbuka miezi ya nyuma hapa ilikuwa kila wakati tukifika mabadiliko ya bei mafuta yanapotea, lakini ukweli yalikuwa hayapotei, yalikuwa yanahifadhiwa kwa ajili ya ku-attract bei mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulivyoitana, tukawaambia jambo hili lazima lifike mwisho na litafika mwisho kwa jasho lingi na ninawashukuru sana. Wao wenyewe wameamua kuchukua ile principle ya regulate yourself or perish, wakaamua kujisimamia wenyewe. Kila aliyeficha mafuta wameshughulikiana wenyewe na sisi kama Serikali tumechukua hatua. Tunawashukuru, kwa kweli ukipata wadau ambao ukiwaambia jambo wanafanyia kazi, siyo busara tena kuendelea kuwalaumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nichukue nafasi hii kwa kweli kuzishukuru kampuni zote za mafuta hapa nchini kwa kuelewa dhana ya Serikali ya kutaka Watanzania wapate huduma iliyo bora na ya haraka zaidi. Ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo yote haya yanayotendeka hayawezi kutendeka kama hatuna watendaji ambao wana uwezo na kitu cha kuwasaidia Watanzania. Nawashukuru sana watendaji wote wa Wizara na taasisi zake zote chini ya Katibu Mkuu, Mhandisi Felchesmi Mramba na Naibu wake Dkt. Mataragio kwa usimamizi mzuri sana wanaoufanya na kutusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaweza ukawa na watendaji unatoa maelekezo haya, halafu wanakuletea ugumu badala ya urahisi. Ni kawaida mahali fulani ukiwaambia watu tufanye jambo hili wanakutangulizia ugumu badala ya mkakati wa kufika kule mnakotaka kwenda, tofauti sana na watendaji wetu tulionao Wizara ya Nishati. Ukija na wazo watakwambia, tupe muda tutafute namna ya kulitekeleza kwa mujibu wa sheria na kwa haraka kama unavyotaka. Bila wao tusingefika hapa. Ninawashukuru sana na kwa sababu nimepata nafasi hii, naomba niwashukuru sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nawashukuru wenyeviti wa bodi zote za Wizara ya Nishati, ni wenyeviti wabobezi kama mnavyowafahamu, walitambulishwa jana. Wana kalba yao, wana uzoefu wao, wana tajiriba kubwa na mimi nataka niwahakikishie kwamba tutaendelea kuwapa ushirikiano wa kila namna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati wa michango ya Waheshimiwa Wabunge na kwa sababu ya muda, naomba tu unikubalie nitumie fursa hii vilevile kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana kwa namna ya pekee Mheshimiwa Dkt. David Mathayo, Mwenyekiti na Makamu wake Mheshimiwa Kilumbe Ng'enda kwa namna wanavyotusimamia tunapokuwa tunatekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali japo kwa kifupi zilizotolewa kwanza na Kamati ya Kudumu ya Bunge, na pia Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia. Waheshimiwa Wabunge 49 wamechangia kwa kusema hapa Bungeni, nami nilitaka niiweke michango yao kwenye makundi ili wakati wa kujibu, inawezekana nisitaje mchango wa Mbunge mmoja mmoja, lakini walau kwa ujumla wake naweza kuzungumzia hoja walizokuwa wamezizungumzia.

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ambayo takribani kila Mbunge ameizungumza ni hali ya kukatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Suala la kukatika umeme linawakera sana Watanzania, suala la kukatika umeme linawakera sana Waheshimiwa Wabunge, suala la kukatika umeme linakukera sana wewe.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka wakati fulani tukiwa hapa Bungeni, Mbunge mmoja aliuliza swali, nawe ukaamua kutoa mwongozo, ukasema; “Hili suala la kukatikakatika umeme tupeni timeframe, litaisha lini?” Sisi tukasema linaweza kwisha mwezi wa Nne. Wewe ukasema mimi nakupeni hadi mwezi wa Sita. Nadhani ulikuwa na mashaka kidogo kutokana na historia ya kule tulikopita na matamko mengi ambayo tumekuwa tukiyafanya.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie kuwa suala la kukatika umeme hapa nchini lilikuwa linachangiwa kwa kiwango kikubwa na upungufu wa umeme. Nataka nieleze hapa, kuna watu wengine wanaweza kuwa wanachanganya mambo huko nje, kwamba kukatika umeme kunachangiwa kwa kiasi kikubwa huko tulipotoka, ni upungufu wa umeme, kwamba umeme unaozalishwa na umeme unaohitajika, umeme unaozalishwa ni kidogo kuliko mahitaji.

Mheshimiwa Spika, upungufu wa umeme tuliokuwa nao ulikuwa megawatt 410. Megawatt 410 ni umeme mwingi sana, kwa hiyo, kinachotokea ni lazima umeme utakatika kwa sababu kuna mgao wa umeme. Sasa hatua ya kwanza ya kufanya ni kuhakikisha kwamba neno mgao wa umeme linakwisha. Kwa sababu gani? Kwa sababu kile unachozalisha, basi kiwe na uwezo wa kuhimili yale mahitaji yaliyopo. Hiki ndicho kilichofanyika, kwamba uwezo wetu wa kuzalisha umeme unakutana na mahitaji na kunakuwa na ziada kidogo.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana utaona tukiwasha mitambo yetu yote ya umeme, hatuna mahali pengine kwa kupeleka umeme, hivyo inabidi mitambo mingine tuisimamishe iwe standby ili kukitokea madhara au tatizo mahali fulani, basi ule mtambo ambao upo kwa dharura unauwasha kwa ajili ya kuondoa hiyo changamoto ya umeme.

Mheshimiwa Spika, hivi leo ninavyozungumza tuna mitambo mbalimbali ya Kidatu na kadhalika, lakini mitambo ya Kinyerezi mashine zote nne hatujaziwasha kwa sababu mahitaji ya umeme tunayohitaji na uwezo wetu wa kuzalisha unakidhi mahitaji na kwa hiyo hakuna mgao.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna jambo lingine, kwamba umeme utakatika siyo kwa sababu ya upungufu wa umeme, utakatika kwa sababu nyinginezo, na mojawapo ni miundombinu. Ni kweli Waheshimiwa Wabunge wameeleza hapa tena kwa uchungu kwamba miundombinu tuliyonayo mingi imechoka, na kwamba mashine nyingi tulizonazo za kuzalisha umeme ni za muda mrefu. Tukubaliane na ukweli huo kwamba nyingine ni za miaka ya 1970, nyingine ni za miaka ya 1980 na nyingine miaka ya 1990. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile kutakuwa na matengenezo ya hapa na pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, njia za kusafirisha umeme; kwa sababu kuzalisha umeme ni jambo moja na kuufanya umeme umfikie mteja, ni jambo lingine. Njia hizo nazo ni ndefu sana. Utakuta kuna njia nyingine, amezungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja, kuna njia moja ya kuchukua umeme kuutoa Unga Limited upite mpaka uende Loliondo, ambayo ni kilomita nyingi sana. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile, kukitokea shida mahali fulani, labda mti umedondoka au line imeharibika, unawatoa Watanzania wengi sana. Hilo halisababishwi na shida ya uzalishaji, linasababishwa na miundombinu

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingine tuliyonayo ya uhujumu tu wa miundombinu. Kuna watu tunao, ni Watanzania wenzetu, kwa sababu ya kujipatia fedha za haraka pengine wameamua kuiba transformer. Kwenye transformer kuna product mbili zinanunuliwa sana; zile waya pamoja na mafuta.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, tuna matukio katika kipindi kifupi, transformer zetu 87 zimeibiwa, na unakuta kuna mtu mwingine anakata kwa ajili ya kutoa cable akauze. Sasa hivi tunao watu ambao wana kesi wapo Mahakamani. Huyu akichukua transformer, kuna watu wengi sana utawatoa kwenye umeme. Sasa atakayeonwa ni TANESCO, lakini kumbe kuna watu fulani wamesababisha shida hiyo.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ambayo inatokea ni katika kipindi hiki cha mvua. Waheshimiwa Wabunge tukubaliane na tukubali kwamba mvua hizi zimekuja, pamoja na kwamba ni neema, lakini pia zimeleta na gharama mbalimbali. Barabara zimekatika, kuna watu tunawazungumza hawana mahali pa kukaa. Kwa vyovyote vile, miundombinu yetu mingi itakuwa na matatizo.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tu cha mvua tuna nguzo zaidi ya 651 zimeondolewa na maji. Nguzo ikiondoka maana yake hapo hapatakuwa na umeme. Tuna transformer 39 zimeondolewa na maji. Kwa vyovyote vile zile zikiondolewa hakutakuwa na umeme; na zikiondolewa hizo, maana yake umeme utakatika, siyo kwa sababu ya uzalishaji, bali ni sababu ya kimiundombinu.

Mheshimiwa Spika, sasa tunafanyaje? Tunachukua kila aina ya hatua ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha miundombinu. Ni kweli kwamba tunazo line ndefu, nchi hii tunahitaji vituo vya kupooza umeme (substation) 216 nchi nzima. Tulivyonavyo ni 131 tena na vyenyewe vingi vimechoka, ni vya muda mrefu. Tunahitaji kujenga vituo vipya 85, na tunahitaji kujenga vituo vipya vya kupoozea umeme kwenye maeneo ambayo yapo nje ya gridi 24. Vyote hivi vinahitaji uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametupa kila aina ya support na Wizara ya Fedha pia. Rasilimali fedha tunapewa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kila shilingi tunayoipata inaleta maana ya maisha ya Watanzania kutafsiri shida tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyozungumzwa ni hatua zinazochukuliwa kwa wakandarasi wasiotekeleza miradi. Anayemulika nyoka, anaanzia miguuni mwake. Kabla hatujawalaumu wakandarasi wanaotoka nje, tujiangalie wakandarasi wa Serikali tulionao.

Mheshimiwa Spika, tunazo kampuni za Serikali zinazopewa miradi mbalimbali ya ujenzi. Kwa mfano ITIDICO ni kampuni yetu, ina miradi mingi inajenga. Sasa, performance yao ikoje? Performance yao siyo nzuri. Tunakubaliana na watu wa Tabora wataniambia, watu wa Katavi watazungumza na maeneo mengine. Sasa unafanyaje? Unaendelea kusema ongezeni kasi halafu hali inabaki kama ilivyo, hapana, ni lazima kuchukua hatua.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tuliivunja Bodi ya ITIDICO kwa sababu ya kutaka tuwe na ufanisi. Tukaibadilisha Menejimenti ya ITIDICO ili tupate ufanisi, na tunakwenda kwa wakandarasi wa sekta binafsi ambao wote wamepewa kazi halafu hawajafanya kazi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninajua kuna trick nyingine za kisheria lazima uende kwa tahadhari. Nataka niwaambieni Waheshimiwa Wabunge kwamba tunawafanyia uchambuzi na kwa yeyote yule ambaye performance yake haikufika viwango tunavyohitaji miradi inayokuja baadaye hatutawapa na badala yake tutawapa watu ambao wana uwezo wa kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, tunachotaka, Waheshimiwa Wabunge wakisimama hapa Bungeni na ninamwomba Mungu iwe hivyo, kazi yao iwe kusema umeme umefika, tunataka ufike na mahali fulani. Hili nataka nilieleze na nadhani ni jambo la kueleweshana. Waheshimiwa Wabunge kuna watu wanasema kwamba umepeleka umeme kwenye kijiji fulani, ndiyo, lakini waliopata ni watu 20, ni kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni kufikisha umeme, kwenye kijiji kuwe na access. Dar es Salaam unayoiona hapa 15% ya wakazi wake hawana umeme, haimaanishi kwamba Dar es Salaam hakuna umeme. Jambo la kuwaunganisha wananchi na umeme ni jambo endelevu. Utafikisha umeme leo, kuna watu 20 wamejenga nyumba mpya, kesho nao watahitaji umeme.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni access, umeme ufike, halafu baadaye utaendelea kuunganisha taratibu. Ni jambo ambalo tutaendelea nalo miaka yote, halitaisha. Muhimu umeme ufike kwanza, vijiji vyote 12,000 vipate umeme, tukimaliza vijiji, vitongoji 64,000 vipate umeme, baadaye connectivity itaendelea hatua kwa hatua, hatimaye Watanzania waweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na kwa kweli niwashukuru tena, mnatuvumilia mno. Wakati fulani tukipata changamoto mnakuwa pamoja nasi pamoja na Watanzania. Naomba mtuvumilie, mtukubalie tufanye jambo moja. La kwanza, tuwaambie ukweli na ukweli ni huu kwamba ni lazima umeme ufike kwanza kijijini kabla haujakwenda kitongojini; na umeme ukifika kitongojini utatoka kwenye kitongoji utakwenda kwenye nyumba (household).

Mheshimiwa Spika, haitatokea hata siku moja nyumba zote kwenye kitongoji hicho ziamke siku moja zina umeme zote. Atakayewaambia maneno haya, ni mwongo na Mbinguni hafiki. Tunakwenda hatua kwa hatua kwa utaratibu, na hiki ndicho tutakachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale walio nje ya Gridi ya Taifa, Mikoa ya Kagera, Katavi, Lindi na Mtwara nataka niwahakikishieni kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita imeweka resource ya kutosha ya kuji-connect sisi na mikoa yote hapa nchini. Siyo tu hivyo, tunataka tujiunge vilevile na mataifa ambayo ni jirani zetu.

Mheshimiwa Spika, tayari tumekamilisha Mradi wa Lemguru, tunajiunga na Kenya, Rwanda na Burundi tumeshajiunga. Tunajenga mradi wetu wa Kwenda kujiunga na Zambia. Tukimaliza hiyo, kama tuna ziada kama sasa hivi, basi tuwe na power exchange program pamoja na majirani zetu kwa mujibu wa taratibu zetu za Eastern African Power. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili tunalifanya, sasa tunajenga mradi mkubwa wa kuwaunganisha watu wa Kagera na gridi kule Lindi na Mtwara. Kama tulivyoeleza, miradi inaendelea. Zipo changamoto za fidia za hapa na pale, na kwa upande wa Lindi, tunazifanyia kazi ili tuweze kukamilisha utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, limeelezwa jambo lingine hapa kuhusiana na habari ya CSR kwenye maeneo ambako kuna miradi ya mafuta na gesi. Naomba nikiri kwamba Waheshimiwa Wabunge wote waliozungumza jambo hili wamezungumza ukweli. Sisi Wizara ya Nishati tumepitia tukajiuliza, hivi kweli watu wa Lindi na Mtwara ambao ni wazalishaji wa gesi CSR yao ipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeenda Madimba, tumeenda Songosongo. Watu wa Songosongo; kutoka Songosongo kwenda Makao Makuu ya Wilaya, mahali ambako gesi inatoka, hawana hata usafiri wa kuwafikisha kwenda Makao Makuu ya Wilaya. Unawakuta wananchi wanalalamika umeme unakatika kwenye maeneo yao na gesi inatoka pale; hili halikubaliki, ni lazima tuchukue hatua.

Mheshimiwa Spika, tumeamua sasa kwa pamoja, na kwenye hotuba yangu nimeeleza kwamba tunapitisha kanuni ya uwajibikaji kwa wananchi kwenye miradi yote ya mafuta na gesi ili tuwatoe wananchi kwenye malalamiko ya kuona kwamba gesi hii tunaitoa hapa tunaipeleka mahali fulani huku hali zao bado zipo mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nataka nikuhakikishie kwamba kwa Madimba na Songosongo tunao mpango maalum. Kwa sababu haiwezekani kwenye plant mle ndani wana umeme wa kutosha haukatiki, lakini wananchi nje ya plant umeme unakatika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana kwamba ni lazima tutengeneze utaratibu wa wao kuwa na line mbili; line ya TANESCO na line nyingine inayotoka kwenye plant ambako umeme haukatiki kwenda kwenye maisha ya watu wanaozunguka maeneo hayo ili wakati umeme wa TANESCO ukikatika wawe wana-backup ya umeme mwingine unaotoka kwenye plant.

Mheshiiwa Spika, ni ukweli usiofichika kwamba kwenye plant kule umeme wao haukatiki, kila siku upo, ila pale nje kwa wananchi unakatika; na wananchi bahati njema ni watu rahimu, mabomba yale yakipasuka ndio wanaopiga simu kusema kwamba mabomba yenu yamepasuka, njooni m-fix. Sasa kama wao wana wema mkubwa kwenye miradi hiyo, ni lazima na sisi Serikali tuwaoneshe wema kwa kuwapatia huduma bora kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, wakati tunazungumza hizi kampuni kubwa kufanya CSR kwenye miradi, tukubali kwamba zipo fedha zinalipwa, zinaitwa service levy. Service levy ikilipwa inalipwa kwenye halmashauri, lakini kwa bahati mbaya halmashauri wakati wa kusimamia zile fedha vipaumbele vyao haviangalii maeneo ambako miradi hii ndiyo imezalisha hii service levy.

Mheshimiwa Spika, jambo hili na sisi ni Madiwani, twende tukawaambie wakurugenzi. Hapa nataka niwaombe Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi na Watendaji wa Halmashauri wote, sasa hapa nazungumza kama Naibu Waziri Mkuu. Fedha za service levy zinazokwenda kwenye halmashauri kutoka kwenye miradi yote ya mafuta na gesi ni lazima sehemu ya fedha hizo irudi kwenye vijiji ambavyo kunachimbwa hiyo gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekwenda Songosongo, Waheshimiwa wa Kilwa mpo hapa, shilingi milioni 500 za Service Levy zimechukuliwa pale ndani, zipo kwenye halmashauri, lakini halmashauri hawajawarudishia fedha watu wa Songosongo. Haikubaliki na haiwezi kuwa sawa. Hili tutaanza kulisimamia kuanzia sasa. Katibu Mkuu Wizara ya Nishati wasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI tuje na mpango wa Service Levy zinazotolewa kwenye hayo maeneo ili zianze kurudi kwenye maeneo hayo ambako Serikali inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili wakati tunasaini mkataba wa kununua shares za Wint Wealth Mheshimiwa Rais alilieleza, tena kwa utulivu kabisa, akasema sitaki kuona malalamiko ya wananchi mahali ambapo gesi inachimbwa, wanaendelea kulalamika na maneno kwamba sisi hatuoni manufaa ya gesi. Service Levy, CSR sasa zitaanza kufanyiwa kazi kwa kasi kubwa, na Waheshimiwa Wabunge mtupe taarifa mahali mnapoona haya mambo hayaendi sawa.

Mheshimiwa Spika, nataka nimalizie hili jambo la CSR kwenye EACOP. Mheshimiwa Mbunge amezungumza kwamba walifanya ziara kule, walipofika wakaambiwa CSR ni siri. Aliyesema hivyo ni mwongo, CSR siyo siri, CSR ni kitu cha wazi. Kama Serikali inakuja hapa kutangaza mapato na matumizi kwa Wabunge na mipango yake, CSR ni kitu gani kiwe siri kwa wananchi na Wabunge? Haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, habari ninayotaka kumwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba EACOP sisi kama wabia tena tuliochangia fedha nyingi, dola za kimarekani milioni 289.78 tunalisimamia. Ndiyo maana mtaona CSR kwenye EACOP tumeshatumia shilingi bilioni 27. Shilingi bilioni 3.7 zimekwenda kwenye miradi ya maji, shilingi bilioni 19.6 zimekwenda kwenye miradi ya barabara na shilingi milioni 710 kwenye elimu na afya. Hizi ni fedha ambazo zimetolewa kwenye maeneo ambako miradi inafanyika; Tanga, Tabora kwa maana ya Nzega pamoja na Misenyi, imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kuna local content issue inazungumzwa. Nawaomba Watanzania kupitia Bunge lako tuache kuwa madalali wa kujinyima faida kama nchi. Hapa kwenye EACOP kanuni yetu ipo clear, kwamba kazi ambazo anaweza kufanya Mtanzania afanye Mtanzania na siyo mgeni.

Mheshimiwa Spika, vinatokea vikampuni vya kigeni vinamtafuta Mtanzania mmoja anaitwa Doto Biteko anatoa NIDA yake, anatoa documents zake; kinasajiliwa kikampuni a shell company, yule Mtanzania anapewa hela yake kidogo tu halafu huyu mtu anachukua. Mle ndani kuna Mtanzania, lakini nyuma kuna watu wengine nje ya nchi. Mkienda ku-compete nyaraka zinaonekana ni Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, ukimtafuta huyo Mtanzania ukamwuliza, uliomba kazi gani? Anakwambia, kwani wapi? Maana naye hajui. Yeye kapewa hela yake, dola elfu 50, ameona Mbingu na dunia zimekutana zinamshangilia. Kumbe hiyo kazi unafanya, ni ya kuchukua mtaji ndani ya nchi na kuwapelekea watu nje ya nchi. Tumechukua hatua, tumewachambua wote kupitia EWURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru sana EWURA na TPDC, wale wote ambao wamefanya artificial company kwa kutumia document za Watanzania wakati wao ni watu wa nje tumewaondoa kwenye utaratibu wa kazi na tutaendelea na kazi hizo. Haiwezekani eti kujenga barabara tena barabara ya vumbi inayotaka excavator, compactor na mitambo ambayo kila Mtanzania hapa anayo kazi hiyo, ichukuliwe na mtu kutoka nje ya nchi, haiwezekani. It will never happen under my watch and under Dr. Samia Suluhu Hassan’s watch, kwa sababu tunataka Watanzania wanufaike na rasilimali walizonazo pamoja na miradi hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Deus kwamba hili tumelifanyia kazi na tutalimaliza na Mungu atusaidie tutalifikisha.

Mheshimiwa Spika, najua nina constrain ya muda na nimeshasikia hiyo kengele, nami nakuangalia; najua ukimwangalia mtu kwamba muda umeisha, una jicho la aina fulani, nimeshakuona, unikubalie. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo yanayoitwa vijiji miji ambayo na yenyewe kuna mahali watu wanaambiwa kwamba sasa ni lazima nao walipe shilingi 320,000.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais akiwa ziara Mtwara na Lindi, alitupa kazi mahususi, akasema tuyachambue maeneo hayo. Tumefanya uchambuzi, tumepata maeneo 1,570 ambayo kwa kweli unaweza ukayataja ni miji, lakini kwa kweli ni vijijini, wanastahili kulipa shilingi 27,000.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais amesikia kilio chenu, tunakwenda kuyafanyia kazi maeneo haya na utaratibu utaelezwa hapo baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kusogeza huduma kwa wananchi, yapo maeneo ni makubwa sana, mahitaji yamekuwa makubwa, ni lazima tubadilishe maeneo ya utawala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wameeleza Waheshimiwa Wabunge, kwa mfano Kigamboni. Kigamboni ipo Temeke. Kigamboni peke yake ni eneo kubwa mno. Meneja wa Mkoa wa Temeke atoke huko aliko ndiko watu wengi waliko na watu wanajenga ndani ya Kigamboni kwenda mbali. Tumeamua kama Wizara, tutaongeza maeneo ya kiutawala ili tusogeze huduma zaidi Kigamboni ikiwepo na Kahama kwa sababu tunafahamu mahitaji yale yanahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la CNG tunalichukua kwa uzito mkubwa. Amesema hapa Mheshimiwa Musukuma, kwamba Serikali tuanze. Sisi pamoja na GPSA tumeanza kutafuta mshauri ili vyombo vyote vya Serikali tunavyotumia, basi viwe na hybrid ya kuwa na CNG. Tunasubiri uchambuzi huo ufanyike, ukishafanyika, kiu yetu ni kuona huko tuendako kwa ajili ya kupunguza matumizi ya Serikali, basi tuwe na magari ambayo yanatumia CNG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepunguza masharti ya kufungua Vituo vya CNG, wapo watu wengine wameomba, wakishaomba bahati mbaya wanachelewa kurudi. Kwa mfano, Mheshimiwa Kilumbe amezungumza kwamba, kuna maombi 11. Namwomba Mheshimiwa Kilumbe, kama anawafahamu awaambie walete documents tulizowaomba. Kuna mwingine ameombwa tu alete EIA haraka haraka anakwambia ngoja nije nitachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, tunayo maombi zaidi ya 30 ya watu wanaoomba kufungua vituo vipya vya CNG, ninataka niwahakikishieni kwamba, akileta leo nyaraka zake zimekamilika, kesho yake asubuhi kunapokucha tutakuwa tumeshashughulikia hiyo kazi yake na nyaraka zote zimekamilika, na ndani ya siku tatu tutakuwa tumempa leseni ili aendelee kufanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la call center, amelieleza. Nimalizie la mwisho kabisa kuwaomba ndugu zetu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, watuvumilie, tuna kazi kubwa ya kufanya ndani ya TANESCO kwa sababu tunaamini kwamba, TANESCO ndio wamebeba moyo wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli niwashukuru Waheshimiwa Wabunge, kila Meneja aliyefanya vizuri humu ndani mmempa maua yake. Mimi nikiona mnawapongeza ninyi ninapata nguvu kwamba nina watu sahihi wa kufanya nao kazi. Ninaomba mfanye nao kazi, mahali wanapokosea waambieni na kama mnaona ni kichwa ngumu niambieni mimi ndiyo kazi yangu niliyopewa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepeana utaratibu wa kupimana kila siku. Kila siku Mkurugenzi wetu wa usafirishaji wa umeme wa distribution, tunachukua tiketi, nani amefanya vizuri? Tunawapanga wa kwanza hadi wa mwisho. Tukimaliza kuwapanga wa kwanza hadi wa mwisho, kwa wiki tunatengeneza ripoti moja. Tunajua wiki hii Meneja wa Mkoa gani hajafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, tunapanga wiki nne kutengeneza ripoti ya mwezi. Tukimaliza tunachukua miezi mitatu tunatengeneza robo moja. Hiyo robo moja aliyefanya vizuri tunampa zawadi aliyekuwa wa mwisho kwa kushughulika na wateja, tunamshusha cheo. lazima tukubaliane, tuwe na mipango. Wananchi wanataka tuwe na kitu ambacho wakiwa na tatizo kwenye umeme wapate majibu. (Makofi)
Mhehimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge watupe muda, TANESCO wanafanya kazi kubwa. Wakati mwingine mkiona wanatoa taarifa ya katizo la umeme, jamani tuelewe siyo mgao, wanahitaji kufanya marekebisho.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, kwa mfano, leo kule Kilimanjaro mafuriko yametokea, Meneja wetu wa TANESCO ameombwa azime umeme ili kunusuru hali iliyopo kule. Atafanyaje Meneja huyu akikata umeme? Tuwavumilie. Matangazo yale wanayoyatoa, basi tuyapokee tukiamini kwamba ni ya nia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna tangazo mtu anasema; “Tutazima umeme kwa ajili ya matengenezo ya kinga.” Mtu wa comment ya kwanza anasema; “Ninyi nanyi tumewachoka.” Sasa tufanyaje katika mazingira kama hayo? Ni lazima hii miundombinu iendelee kutengenezwa, kama ambavyo una gari Mheshimiwa Mbunge, utaiendesha kila baada ya muda fulani utaipeleka gereji kutengenezwa. Ukiipeleka gereji kutengenezwa, haimaanishi hauna gari, gari ipo unarekebisha na miundombinu ipo vilevile.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna mahali fulani kikombe kimepasuka, ni lazima turekebishe, na huwezi kurekebisha kukiwa na umeme, ni lazima utazima. Watukubalie wakati tunafanya marekebisho hayo, kwani tutakuwa tukiyafanya hapa na pale. Cha muhimu, wananchi wanapaswa kufahamu kwamba kuna jambo gani linakuja kukata umeme. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, na ninaushukuru sana Uongozi wa Bunge. Kwa kweli tumesikiliza hoja zenu, tunakwenda kufanyia kazi. Kwa unyeyekevu mkubwa, wale ambao mmeahidi kushika shilingi yangu, naomba mnifanyie hisani moja, mnipe fedha pamoja na wasaidizi wangu tukatatue changamoto ya yale yote mliyoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi hatutakuja hapa; na moja ya jambo ambalo nimewaambia wenzangu ni kwamba, msiende kusema uwongo kwa ajili ya kutafuta makofi. Utapigiwa makofi leo, kesho makofi hayo yatageuka kuwa kuzomewa. Tutafute heshima ya kusema ukweli na kuwa na matokeo kwa kazi yetu na kusema kidogo na kuwa na matokeo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawaomba mtupitishie fedha hizi shilingi trilioni 1.8, tulizoomba. Ukweli ni kwamba, zitakwenda kutatua changamoto tulizonazo. Baada ya robo inayokuja, tutakuja kujipima kwenu, wapi tumefikia kupitia Kamati yenu?

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba tena kutoa hoja na ahsanteni sana. (Makofi)