Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuweka mchango wangu kwenye hoja ya ndugu yetu Mheshimiwa Tarimo ambayo ni hoja nzuri na muhimu.
Mheshimiwa Spika, kwanza naunga mkono hoja kwamba ni nzuri na sisi wote tunakiri kabisa kwamba tunalo Jeshi la Zimamoto na uokoaji lenye wajibu huo ambalo lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini kwa kweli halina vifaa vya kutosha na hata watendakazi Askari wa Zimamoto na Uokoaji si wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo nilitaka niseme kwamba kwa hali ya sasa ya maendeleo hatutaweza kuwa na magari ya zimamoto ya kutosha, hatutaweza kwa hali ya sasa kuwa na vifaa vya kutosha vya uokoaji, ni lazima tujielekeze zaidi katika kuelimisha umma wetu katika baadhi ya maeneo juu ya namna nzuri zaidi ya kujiokoa na kuchukua tahadhari. Magari ya zimamoto na vifaa vya ukokoaji viwepo, lakini tukisema kwamba vya kutosha sehemu fulani yawe magari kumi au 15, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia ninachotaka kusema ni kimoja tu, naungana na wanaosema kwamba kuwabebesha halmashauri kuwa hili ni sehemu ya wajibu wao siungi mkono hiyo hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe unafahamu halmashauri imepewa majukumu ya kutoa taka katika maeneo yetu, magari ya kusomba taka hawajaweza kukidhi, hayajaweza kutosheleza, bado kuna malalamiko ya kurundikana kwa taka katika maeneo ya masoko na maeneo mengine chungu mzima. Pia siyo hilo tu, maboma ya zahanati na shule wanashindwa kuyamalizia mpaka wanakuja kuomba hapa Serikali Kuu isaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi ninachoweza kusema ni kwamba hoja ni nzuri na zaidi tujielekeze kutazama pande zote mbili. Wengi wanazungumza hapa suala la kuzima moto na wengine wanazungumza uokoaji wanafikiri maana yake ni kuokoa mali, ni kuokoa watu na hii ina maana kwamba watu wanaopata matatizo kwenye Ziwa Tanganyika, maziwa mengine na baharini na wengine wanaopata majanga ya mafuriko wanaopata milima ku-slide waweze kuapata nafasi ya kuokolewa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Stanslaus Mabula.
TAARIFA
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka tu nimuongezee Mheshimiwa Kilumbe kwamba, thamani ya gari la zimamoto moja kununua ni kati ya shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja peke yake. Hiyo ni manunuzi tu hujaweka service na matumizi mengine, ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa…
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa unasubiri uitwe tena. Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda unaipokea Taarifa hiyo? (Kicheko)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, napokea Taarifa. Unajua nilikuwa nakimbizana na muda, niwie radhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nasema hiyo bei iliyotajwa ya gari ya zimamoto kwa gari ya taka ni kama shilingi milioni 100 tu nazo zinawashinda halmashauri nyingi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka niseme hoja ni nzuri, lakini tujielekeze katika harakati ambazo Mheshimiwa Rais wetu ameanza kuzionesha kama hivi amepata fedha aongeze vifaa na sisi tuwe tunaitazama mara kwa mara bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani hasa katika watu wa zimamoto na uokoaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kwa upande wangu ni kweli kabisa kwamba halmashauri na hasa watu wa Mipango Miji hizi fire hydrants nyingi zimejengewa majengo, badala ya maeneo haya ya fire hydrants kuwa wazi ili watu waweze kuchukua maji wakati wa kuzima moto, kuna majengio yamejengwa hapo hii miundombinu tena imekuwa haipo.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hilo tuwafundishe na kuwasaidia watu wetu suala la kununua na kuweka katika majumba yako kitu kinaitwa fire detector ili iweze kuonesha ni wakati gani moto unataka kutokea. (Makofi)