Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa namna ambavyo umeendelea kuusimamia mjadala huu na mimi ninachukua nafasi hii kuwashukuru wale wote waliochangia na wote waliochangia wameendelea kuboresha hoja hii na kutuwekea mazingira mazuri ya namna ya kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitagusia baadhi ya maeneo, hakuna ubishi kwamba tunahitaji manpower eneo hili, hilo halina ubishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la zimamoto na uokoaji, baadhi ya watu wamekimbilia kwenye moto tu, lakini mtoto akitumbukia kwenye shimo la choo kunahitajika utaalamu wa kumtoa. Kwa hiyo, ndiyo maana ninasema kuna vitu vingi vya kufanya kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo maana mimi kuna hoja zinazokuja, kwa mfano ile Tume ya Haki Jinai inataka kurudishwa kwenye halmashauri, mimi hilo siliungi mkono kwa sababu badi ninajua halmashauri nyingi hazina uwezo wa kulisimamia hilo.
Mheshimiwa Spika, siyo kwamba halmashauri tu hazina uwezo, hii shughuli ya uokoaji ni shughuli inayohitaji amri za kijeshi, kutumia amri za kiraia moto unawake watu waende siyo rahisi.
Kwa hiyo, kuna baadhi ya vitu vilivyoko kwenye Haki Jinai, mimi sitaki hata kuvigusa. Kwa hiyo, ndiyo maana bado ninasisitiza jeshi libaki kuwa jeshi na hii kazi ifanyike kijeshi, lakini halmashauri tusiondolewe wajibu wetu au namna ya kushiriki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru mchangiaji mmoja amesema hawajazuiwa lakini ninajua kabisa, sisi Moshi Mjini tulikuwa na magari tuliyopewa na miji dada (miji marafiki), lakini lilipokuwa jeshi tuliwapa na jeshi waliamua iende wapi.
Mheshimiwa Spika, mimi kwenye hoja yangu ninamaanisha, kama Moshi Mjini tukishirikiana na ninyi kununua gari au tumepewa na wadau, libaki pale kwa matumizi yetu, jeshi mwendelee kulisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri, hata pale Moshi Mjini kabla ya gari mpya ambayo tumeipata, gari iliyokuwepo ilikuwa inahitaji service, jeshi halikuwa na hela na halmashauri hawana kifungu cha kwenda kutengeneza gari la Jeshi la Zimamoto. Kwa hiyo, ndiyo maana ninasema kuwe na ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwakumbushe, ushirikiano huu hautakuwa mpya, viwanja vya ndege viliingia makubaliano na jeshi, vyenyewe vinanunua yale magari vinayasimamia, vina-service lakini wanaoyafanyia kazi ni Jeshi la Zimamoto. Kwa hiyo, nilikuwa ninasema hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ninahitaji ufafanuzi, sikusema iwe lazima kwa sababu siyo kila mahali kuna maghorofa. Ninasema kwa halmashauri zenye uwezo na kuna uhitaji huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Moshi Mjini tumeunguliwa Soko la Mbuyuni, ndani ya mwaka mmoja tumeunguliwa mara mbili. Mara ya kwanza tulilizima likiwa nusu, mara ya pili liliisha lote. Sasa shida iko wapi? Wale wafanyabiashara wadogo hawana insurance. Mtaji wake ukiungua pale na vitu vyake maana yake ndiyo ameanza zero, zero kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wale ni wananchi wetu tunahitaji kuwahudumia na ndiyo maana nikasema halmashauri zenye uwezo na kwa nini nimesema kwenye uwezo, gari itakayohitajika Dodoma kwa jinsi ya majengo yaliyoko Dodoma, siyo sawa na Dar es Salaam. Sisi tunaweza tukanunua ya kufanana nchi nzima, lakini Dar es Salaam wana majengo ya ghorofa 36. Gari yao itahitajika ambayo labda ina lift zaidi na uwezo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, halmashauri ikiona ina sababu ya kuwekeza pale kuokoa maisha na uhai wa wananchi wake, basi iweze kufanya hivyo, lakini kuna maeneo kwa mfano, ninakubaliana kabisa na mawazo yaliyoletwa ya kusema kwamba hili suala linahusisha Wizara nyingi, kwa hiyo ni suala mtambuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Wizara ya Ardhi, TAMISEMI, Wizara ya Maji, lazima zikae pamoja katika kupanga kwenye kushughulikia hili jambo. Hilo mimi ninakubaliana nalo 100% kwa sababu fire hydrant nyingi zimefukiwa na barabara na barabara zinajengwa either na TARURA au na TANROADS, lakini fire hydrant ni za Wizara ya Maji na Mamlaka za Maji. Ni lazima wakae pamoja ili kuweza kufanya hayo mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna haja pia ya kuangalia namna ya kuweka ulazima. Kwa mfano, kila mtu anafikiria gari ya fire ni ile ya shilingi bilioni kwa ajili ya kuzima moto, kwenye miji ambayo iko kwenye highway magari yanagongana, mtu yuko hai gari limemminya, kuna vifaa vinahitajika vya kuvunja yale machuma, kukata, kuvuta ili kumtoa, watu wanakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna clips tunazo, mtu alikufa pale Mbeya kwenye Mlima nadhani sijui ni Sekenke, watu wanamwangalia hawawezi kumwokoa. Kwa hiyo, kuna magari madogo labda yanahitajika na vifaa vidogo ambavyo halmashauri inaweza kutokana na eneo lake, basi iweze kufanya hivyo, siyo kuliondoa jukumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jukumu la Serikali na mimi niseme hapa tunasaidiana, ndiyo maana ya ugatuzi, kwa sababu Serikali itaendelea kuwekeza, hata leo ikiwekeza mara mbili ya hela mliyosema, bado mahitaji yapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuseme kwa Dar es Salaam, kwa mfano hata kama mna magari matano, yametokea majanga mawili/matatu, lazima mtahitaji manpower zaidi na magari zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nimeitoa hoja hii ili Serikali iangalie namna ya kuboresha na kushirikiana, lakini halmashauri pia tunaona tuna wajibu wa kuwahudumia wananchi wetu na kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba Serikali ichukue hoja hii na iifanyie kazi pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na Wabunge na yale ambayo nilitoa mwanzo ili basi tuweze kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja hiyo. (Makofi)
SPIKA: Wabunge hawajasikia vizuri. Ili niweze kuwahoji, unatoa hoja tena. Kwa hiyo, hiyo sehemu ya mwisho hawajasikia.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, mawazo niliyoyaleta pamoja na mawazo yaliyoletwa na Wabunge, yale yote ambayo yana tija, ninaomba yachukuliwe na Serikali yafanyiwe kazi ili tuweze kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)