Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naanza kwa kukupongeza wewe Mheshimiwa Mwenyekiti Deo Mwanyika kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, natumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Serikali, Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana kwa wasilisho lake zuri la bajeti. Nazipongeza Kamati zetu zote mbili; kwanza, Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa mawasilisho waliyoyafanya kwa niaba yetu yetu Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona nchi yeyote ina amani na utulivu, basi ujue kuwa mifumo yake ya utoaji haki ni bora na imeimarika. Uniruhusu maneno haya niyanukuu tena kutoka kwa Nabii Isaya 32:17. Nabii Isaya aliishi karne ya nane Kabla ya Kristo, alisema, “Amani ni tunda la haki.” Pale ambapo haki inatendeka, amani itapatikana na itadumu. Maneno haya yalizungumzwa miaka mingi sana, nimesema hapa, ni karne ya Nane Kabla ya Kristo. Ninavyosema Kabla ya Kristo, maana yake, kabla ya mwaka sifuri. Karne ya nane, kabla ya mwaka sifuri, maneno haya yalizungumzwa kwamba amani ni tunda la haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii na maneno haya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anayaishi kwa vitendo. Mimi nimekuwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria huko nyuma na sasa Utawala, Katiba na Sheria, sasa ni miaka nane. Mambo niliyoyaona ni mapinduzi makubwa sana ya mfumo wa utoaji na upatikanaji haki nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka hadi mwaka tumeona commitment kubwa ya Mheshimiwa Rais kupitia Watendaji wake Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, kupitia watendaji wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania. Yote tumeyaona, taasisi hizi zote tumeziona zinakwenda na zinatekeleza majukumu kwa ufanisi zaidi mwaka hadi mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa Watanzania kwa sehemu kubwa wanaona umuhimu na wanaona relevance ya Wizara hii ya Katiba na Sheria ambayo ni Wizara mama ambayo ndiyo mhimili na ndiyo nguzo ya amani na utulivu wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunasherehekea miaka 60 ya Muungano wa Tanzania kwa maana ya Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar. Pia ni miaka 63 tangu tupate uhuru Taifa letu limebaki kuwa na amani na utulivu muda wote. Credit kubwa iende kwenye mifumo yetu ya utoaji haki nchini. Mahakama zetu zimekuwa na ubunifu wa hali ya juu ili kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa kila Mtanzania. Tumefuatilia taarifa za Wizara hapa, lakini pia tumefuatilia taarifa za Kamati zetu zote mbili ambazo zimewasilishwa hapa kwa niaba ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika vitu ambavyo tumeona, kwanza ongezeko la miundombinu ya kutolea huduma za haki kwenye ngazi za Mahakama ya Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Rufani na Mahakama Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kote kumekuwa na ujenzi wa miundombinu kwa maana ya ujenzi wa Mahakama. Sasa hizi Mahakama kwa namna moja au nyingine nami naweka msingi zaidi, msingi wa haki tunauona pale ambapo tunaenda kujenga Mahakama nyingi za Mwanzo ambako Watanzania wengi wanaohitaji haki wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona commitment kubwa sana ya Serikali. Hapa natamani sana kuipongeza Serikali katika ujumla wake, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuongoza utendaji mzuri wa Wizara hizi na kuhakikisha haki inawafikia Watanzania katika namna rahisi na namna ya ukaribu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yalikuwa ya jumla, lakini kimahususi kabisa kumefanyika mapinduzi makubwa sana ya kimifumo ndani ya Mahakama ya Tanzania. Hapa naomba kurejea kwenye Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri ambao unafahamika kama TTS au kwa Lugha ya Kiingereza ni Transcription and Translation System.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania ni mashahidi na hapa wananisikiliza, tumekuwa na changamoto kubwa sana ya utoaji haki kwa wakati kwa Watanzania walio wengi. Mahakama zetu zimekuwa zinatumia muda mrefu sana kunukuu mwenendo wa mashtaka na kunukuu hukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pale ambapo wateja wetu ambao ni Watanzania wanahitaji tafsiri kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine kwa haraka, imechukua muda mrefu sana. Jambo hilo limechangia sana kwenye kuchelewesha mwenendo na hukumu za mashtaka mengi. Mashauri mengi yamechukua muda kutolewa maamuzi kwa sababu ya mifumo. Leo Mahakama yetu ya Tanzania ime-adopt Mfumo huu wa Unukuzi na Tafsiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza sana Profesa Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, ambaye amefanya jitihada za kipekee sana kuhakikisha mfumo huu unafungwa kwenye Mahakama zetu. Juu yake yuko Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania. Mapinduzi haya yanakwenda kuwawezesha Watanzania kufikiwa kwa karibu sana na kutendewa haki kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo faida nyingi ambazo kama muda ungeniruhusu, ningezisema lakini natoa tu ushauri kwa Serikali au msisitizo kwa Serikali kwa sababu Kamati zimeshasema mfumo huu umefungwa kwenye Mahakama 11 tu mpaka sasa. Mnajua kabisa mahitaji ni makubwa, Mahakama zetu zote zinahitaji hiyo huduma kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba tu Mheshimiwa Waziri kwa sababu muda hauniruhusu sana, ahakikishe kwamba mifumo hii inakwenda kufungwa kwenye Mahakama zetu zote kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama zetu za Rufani na hivyo kuwawezesha Watanzania kupata haki kwa wakati. Kwa kufanya hivyo, maana yake tutakuwa tumeliweka Taifa letu katika mazingira salama zaidi ya amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru kwa kunipa muda. (Makofi)