Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nianze kwa kutoa ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Kwanza nimpongeze kwa jambo moja anaingia kwenye historia Profesa Muhongo ya kutenga bajeti ya maendeleo ya asilimia 94. Wenzake na Wizara zao tulizozipitisha hapa tumeona Wizara zingine maendeleo asilimia 50, wengine asilimia 40, wengine asilimia 60; yeye ametenga asilimia 94, dhamira ya kuiwasha Tanzania kwa umeme inaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena nimshauri Mheshimiwa Muhongo kama Mbunge ninayetokea Mkoa wa Lindi, kuna suala hapa Wabunge wa Mkoa wa Lindi hawajalielewa vizuri na mimi nimwombe kama kuna uwezekano afanye kikao na Wabunge wa Mkoa wa Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna huu mradi mwema sana, mradi wa LNG ambao unakwenda kufanyika pale Likong‟o kilometa tatu tu kutoka kwenye Jimbo langu. Wabunge hawajauelewa vizuri na ndiyo maana unaona alipokuwa anachangia hapa Mbunge wa Lindi Mjini alikuwa anasema kiwanda hakijengwi wakati LNG siyo issue ya kiwanda, LNG inakwenda kuchochea viwanda. Sasa nilichokiona hapa kuna tatizo la uelewa kwamba huu uelewa wa Wabunge kwanza ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi, fanya kikao na sisi utueleweshe vizuri kabisa. Hii complication unayoiona kwetu Wabunge kwa wananchi huko ndiyo hawaelewi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku napigiwa simu naambiwa Mheshimiwa Mbunge tunaelezwa kwamba sasa Jimbo letu la Mchinga linahamishwa linapelekwa Lindi Mjini. Suala la mradi LNG nawaambia hicho kitu hakipo mbona mimi sijui, sasa mkilihamisha Jimbo la Mchinga kupeleka Lindi Mjini maana yake mimi Mbunge ndiyo basi! Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo huko chini halieleweki. Sasa naona shida kama na Wabunge na sisi hatulielewi vizuri, naomba Mheshimiwa Waziri atenge muda tu hata nusu saa akutane na Wabunge wa Mkoa wa Lindi, ateleweshe vizuri tuweze kulifahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kuhusu suala la usambazaji wa gesi kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara, dhamira njema naiona kwa Mheshimiwa Waziri. Mradi wa usambazaji wa gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani na kwenye vipuri, nimeona wameelezea Miji mitatu ya Kilwa, Lindi Mjini na Mtwara. Mradi ule unagharimu karibu dola milioni kumi karibu shilingi bilioni 22 lakini kwa mwaka huu wametenga shilingi milioni 700, nataka tu kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri hizi milioni 700 walizozitenga mwaka huu za nini? Kwenda kufanya impact assessment au kufanya evaluation maana hizo ndiyo terminologies tulizozizoea, hizi milioni 700 ni za nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hapa aniambie, huu mradi wameuandika vizuri kabisa hapa na kwa takwimu kama mwenzangu alivyotangulia kusema Profesa yupo vizuri sana kwenye takwimu, kwa hiyo, ameainisha vizuri kwamba mradi utagharimu shilingi bilioni 22, lakini mwaka huu wametenga milioni 700 za nini hizi milioni 700? Kwa hiyo, naomba majibu katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu kumebakia vijiji 15 kupata umeme; umeme wa REA phase I na phase II umebakisha vijiji 15, kwa Lindi na Mtwara kubaki na vijiji 15 siyo privilege kwa sababu tuna umeme mwingi unapotea tu, bado ni suala la usambazaji tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, karibu megawatt 30 Waziri unajua zinapotea kila siku kwamba hazitumiki, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri mradi wa REA phase III animalizie vijiji vilivyobakia katika Jimbo la Mchinga vyote vipate umeme kwa sababu ametengeneza fitna kubwa kuonekana vijiji vingine vina umeme na vijiji vingine havina umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Kijiji cha Dimba, Ruvu, Namtamba, Mputwa, Kiwawa, Luchemi, Luhoma, Micheye, Mihandara, Lihimilo na Mkongo, vijiji hivi naomba sana vipatiwe umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine iliyopo Mheshimiwa Waziri hivi sasa ninapoongea kuna vijiji vimepata mradi wa REA phase II. Jambo la ajabu ni kwamba unakuta nguzo zilizopo pale kijijini ni nguzo tatu nne; kijiji kikubwa ambacho vijiji vingine ni Makao Makuu ya Kata, Makao Makuu ya Tarafa, unakuta wanapewa nguzo tatu au nne ndiyo za usambazaji! Kuna shida kubwa sana, unakuta kijiji kizima chenye wakazi karibu 3,000 au 4000 wanapewa nguzo tatu nne, nani atapata umeme? Kwa hiyo, jambo hilo linaleta changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa pale Kitomanga, tatizo kubwa Lutamba, Milola, Mvuleni kuna tatizo kubwa, wamepeleka umeme sawa upo lakini wananchi wanautazama tu, kwa sababu kuna nguzo tatu tu ambazo zimepelekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kwamba hivi sasa ninapoongea nina wananchi kule karibu 200 wamekamilisha taratibu zote za kuingiziwa umeme mpaka sasa huu karibu mwezi wa tatu umeme hawajapata. Nimewahi kuuliza changamoto ni nini? Nguzo ipo karibu wamelipia wamemaliza, wamefanya wiring, kuna shida kubwa watu karibu 200 Mvuleni, Lutamba, Milola, Mchinga, Maloo na Kilolambwani watu wamelipia wanasubiri umeme, umeme hawapati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atueleze tatizo ni nini, mita zimekwisha au LUKU hizo ndiyo shida, tatizo ni nini? Watu wamelipia na wamekamilisha taratibu zote lakini umeme hawapati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo kwa kweli limenipa shida sana ni kuhusu Mchinga. Mchinga ambapo ndiyo Makao Makuu ya Jimbo pale palipata umeme kabla ya hizi program za REA, ndiyo kilikuwa Kijiji pekee, Mchinga na Vijji viwili. Vijiji pekee vya pale katika Jimbo zima vilikuwa na umeme kabla ya kuingia program ya REA, ilipokuja kwenye program ya REA Mchinga haikuwa included. Kilichokuja kutokea ni kwamba ule umeme ambao ulikuwa nguzo tatu, nne pale za awali REA ilikwenda imeiacha kabisa Mchinga hivyo watu wa Mchinga leo hawanufaiki na REA na badala yake kuna madai makubwa ya watu kupatiwa umeme na Mchinga ni sehemu kubwa ina vivutio vingi vya uwekezaji lakini shida ni kwamba umeme hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la madini ya gypsum, naomba tu Mheshimiwa Waziri anisikilize, Mheshimiwa Waziri hapo anayemsemesha Waziri kidogo namwomba dakika moja tu Waziri anisikilize. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba kuna suala la gypsum, Jimbo la Mchinga ni miongoni mwa Majimbo au maeneo ambayo yana gypsum quality. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri aliniunganisha na watendaji wake, nilimletea sample ikapimwa ikaonekana the best gypsum inatoka pale Mchinga, ipo na majibu yapo pale Wizarani kwamba ile gypsum ambayo nimeipeleka one among the best gypsum in Tanzania, ipo pale. Shida iliyokuwepo ni kwamba hivi sasa ninavyoongea kuna maeneo ya vitalu ambavyo tayari vimeshasajiliwa watu zaidi ya 200 wamesajili mimi siwajui, wananchi wenyewe hawawajui. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mkurugenzi wa Madini wa Kanda ya Kusini Ndugu Mtwampaka, kwa sababu niliunganishwa naye, aliniletea orodha ya watu ambao wana certificates karibu 200 za kumili ile migodi. Nilipokwenda kuwahoji wanakijiji hakuna hata mgodi mmoja ambao wananchi wanajua. Hawa watu wenyewe hawajulikani, wako kwenye maandishi tu. Nataka kujua Mheshimiwa Waziri, kuna taratibu gani zinafuatwa ili mtu kupata certificate ya kumiliki eneo la uchimbaji wa madini ama hii migodi ya gypsum.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shida kubwa Mchinga, nikwambie Mheshimiwa Waziri, kama hili litaendelea hawa waliochukua certificates wajue tu kwa Mchinga ni nullified, yaani mimi nikiongea kule kazi imekwisha. Kwa hiyo, kama wataendelea kujificha, Mbunge siwajui, Mkurugenzi wa Halmashauri hawajui, wananchi hawawajui, wajue hizo certificates zao ni za mfukoni, hazita-function Mchinga. Nahitaji watu wote ambao wana certificates za kumiliki maeneo ya uchimbaji waje tuwaone, wasijifiche, waje tuwaone.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shida ya watu kutoka TPDC, hili nilishakueleza Mheshimiwa Waziri, wanakwenda Mchinga kuchukua maeneo, wanakwenda ku-lease wanakatia hati za ardhi kwa sababu tu Mchinga kunaonekana kuna potentiality ya gesi na gypsum. Hili namhakikishia Mheshimiwa Waziri hakuna mtu kutoka TPDC atakayepata eneo Mchinga, ninayeongea ndiye Mbunge wa Jimbo la Mchinga, ndiyo mwisho, ndiyo final say pale. Hakuna mtu ambaye atakwenda kuwadhulumu watu wa Mchinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.