Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nianze moja kwa moja kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo anafanya juhudi za kuboresha Sekta hii ya Sheria nchini, hasa kwenye eneo hili la usimamizi wa vyombo vya utoaji haki. Katika zile ‘R’ nne za Mheshimiwa Rais, ‘R’ ya tatu ni Reform na hapo kwenye Reform ndipo tunapokuta kuna masuala ya kurekebisha sheria na mifumo na hii imefanyika vizuri sana. Tunahitaji mabadiliko mengi ya sheria ili Serikali iweze kujipambanua kufanya kazi vizuri zaidi, ku-respond katika mahitaji ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuwa na sera, lakini kama una sera halafu huna Sheria maana yake ni kwamba, unakuwa huna nguvu ya kutekeleza hiyo sera. Kwa hiyo, kama una sera yoyote ile, lazima hiyo sera iwe backed na sheria ili sheria itoe nguvu kwa watekelezaji wa hiyo sera. Nikirejea kwenye maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa tarehe 15 Julai, 2023 siku alipopokea Taarifa ya Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mohamed Chande, alitoa maagizo makuu matatu yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, agizo kuu la kwanza, Rais aliagiza Taasisi zote za Haki Jinai zifanye marekebisho ya mifumo yao ya kiutendaji ili kusimamia vizuri zaidi upatikanaji wa haki kwa wananchi, hilo lilikuwa agizo kuu la kwanza. Nilitegemea katika speech ya Mheshimiwa Waziri angeainisha marekebisho ambayo yameanza kufanyika, kama Rais alivyoagiza, lakini sikusikia. Pengine labda wakati anahitimisha atakuja atueleze hapa kwamba, ni marekebisho gani ambayo yanaendelea kufanyika kupitia utekelezaji wa agizo hili kuu la Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili, Mheshimiwa Rais aliagiza taasisi zinazohusika ziheshimu utu wa watuhumiwa wakati wa ukamataji, wakati wa upelelezi pamoja na wakati wa uendeshaji wa mashtaka ili haki ionekane inatendeka. Sasa, hapa kidogo nawasifu Polisi, kule kwenye Polisi kuna maboresho mengi katika utekelezaji wa suala hili. Polisi wamejielimisha sana, wanapokamata wanakamata kwa ustaarabu, wanaendesha upelelezi wao kistaarabu na wanampeleka mtuhumiwa Mahakamani kistaarabu. Kwenye kipengele hicho malalamiko ni machache kwa upande wa polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vyombo vyetu vingine, jinsi TFS wanavyokamata watuhumiwa kwenye hifadhi zetu, jinsi wanavyokamata TAWA, hata TANAPA na vyombo vingine inaleta malalamiko makubwa kwa wananchi na hili ni jambo ambalo ni la kuelimishana tu. Kwa nini Polisi wameweza halafu hawa TFS bado wawe na shida kwenye eneo hilo? Kwa hiyo, ni maeneo ambayo ni ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais ambayo kwa kweli, inahitajika elimu kubwa iweze kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengine ambao wanahitaji kupata elimu ni Askari Mgambo. Nao wanakamata kule vijijini, wanatumwa na Maafisa Watendaji wa Vijiji, wanatumwa na Maafisa Watendaji wa Kata, wanakamata kwa vipigo, yaani kidogo kuna shida kwenye eneo la ukamataji. Kwa hiyo, elimu inahitajika kwa vyombo vingi vya Serikali ili waboreshe eneo hili la ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa mashtaka kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliagiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, agizo la tatu ambalo alitoa Mheshimiwa Rais ni Vyombo vya Ulinzi na Usalama vitoe kipaumbele katika kuzuia uhalifu badala ya kutoa kipaumbele katika kukamata, yaani kuviziavizia. Toa kipaumbele katika kuzuia uhalifu badala ya kuvizia kukamata. Nalipongeza tena hapa Jeshi la Polisi, hasa upande wa Polisi Barabarani, wamejikita zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi. Anamwambia kufanya hivi ni kosa la usalama barabarani, kufanya hivi ni kosa, kufanya hivi ni kosa, labda wakirudia hilo gari wanalipiga faini zile za kwenye karatasi. Angalau kidogo upande wa Polisi, lakini vyombo vingine bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, Rais alipotoa maagizo kama hayo alikuwa serious na Taifa lilimwangalia na lilimwelewa. Kwa hiyo, nategemea sana, watekelezaji sasa nao wamwelewe Mheshimiwa Rais ili waende kama anavyotaka. Mheshimiwa Rais anataka nchi iongozwe vizuri na kuiongoza nchi vizuri ni kupunguza malalamiko ya wananchi, wananchi wasiendelee kuvilalamikia vyombo vya Serikali. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aongoze katika utekelezaji wa maagizo hayo ili kweli tuwe na maboresho katika eneo hili la sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu sasa, ukiacha hayo maagizo makuu matatu ya Mheshimiwa Rais. Pendekezo la kwanza, Watanzania wengi wanaoishi vijijini asilimia kubwa ni wahanga wa haki. Mimi ni Mbunge wa vijijini, siyo Mbunge wa mjini kwa hiyo, nina uzoefu zaidi na vijijini. Kule vijijini mfumo wa haki ni kandamizi, yaani ukiitwa kwa Mtendaji wa Kijiji ni hatari, ukiitwa kwa Mtendaji wa Kata ni hatari. Sasa mambo kama haya sidhani kama huku juu wanayafahamu, lakini sisi tunayafahamu. Nafikiri Wabunge wanaotoka vijijini labda wangehusishwa katika mjadala ili kuboresha haki jinai kwenye maeneo ya vijijini kwani limekuwa ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hukumu nyingi kule vijijini zinatolewa na Afisa Mtendaji wa Kijiji, Afisa Mtendaji wa Kata ndiyo Hakimu kule kijijini. Kule kijijini hakuna Mahakama, hata Baraza la Kata utendaji wake ni wa kusuasua kabisa, wale ndiyo Mahakimu, wale ndiyo wanatoza faini. Wewe umekamatwa ugoni? Lipa shilingi milioni tatu. Umempiga mwenzako? Tena Maafisa Watendaji wa Vijiji wengine wana, wewe umempiga mwenzako? Kosa la kupigana hadharani ni wote ndani na ili kutoka toa shilingi milioni na wewe toa shilingi milioni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kengele ya kwanza. (Makofi)

Mheshismiwa Naibu Spika, Mabaraza ya Kata mengi yana shida katika kusimamia haki katika maeneo ya vijijini. Kwa bahati mbaya sana Mabaraza ya Kata hayakuingizwa kwenye Hadidu za Rejea za ile Tume ya Haki Jinai. Kwa hiyo, ile Ripoti ya Tume ya Haki Jinai haikutoa angalizo wala agizo lolote kuhusu uboreshaji kwenye hili eneo la Mabaraza ya Kata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mapendekezo mengi sana huko nyuma kwamba, Mabaraza ya Kata yawekwe chini ya Mahakama badala ya kuwa chini ya wanasiasa kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, lakini angalizo na pendekezo hilo halijafanyiwa kazi na Serikali. Naomba wakati Mheshimiwa Waziri anapokuja alieleze Bunge hili Tukufu ni lini Serikali itafanya uamuzi wa dharura na wa haraka wa kuhamishia Mabaraza ya Kata chini ya Idara ya Mahakama ili kuboresha weledi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama za Mwanzo; kwa mujibu wa Tovuti ya Serikali ya Mahakama, hapa nchini tunazo Mahakama za Mwanzo kama 1,105, kati ya tunazohitaji ambazo ni takribani zaidi ya 3,000. Mahakama ambazo zimekamilika kwa maana ya majengo, watumishi kwa maana ya Mahakimu na watumishi wengine ambao siyo Mahakimu ni Mahakama 84 tu ambazo zina-qualify kwamba, kweli hizo ni Mahakama za Mwanzo. Kwa hiyo, tuna shida katika eneo hili na naiomba Serikali iweke kipaumbele cha juu katika kujenga Mahakama angalau 100 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi tu walizopanga sijui 76, sijui 60, kwa mwaka zinashindikana kujengwa. Naiomba Serikali iweke kipaumbele cha juu kujenga Mahakama. Sisi Sikonge tunahitaji Mahakama saba katika Wilaya ya Sikonge peke yake, kwa sasa tunayo moja tu ya pale Sikonge Mjini, lakini tunahitaji Mahakama ya Kipili, Kitunda, Kiloleli, Ipole, Igigwa na Nyahua. Hizi ni kata za mbali, wananchi wanapata shida kupata haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kuna namba za dharura ambazo zimetajwa kwenye tovuti ya Serikali, kama wananchi wana dharura yoyote wanaweza wakapiga. Katika orodha ya hizi namba za dharura namba ya Mahakama haipo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie dakika moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba ya dharura ya Mahakama haipo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa unachukua muda wa mtu mwingine sasa.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapa. Naunga mkono hoja. (Makofi)