Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Mwanzo kabisa kabla sijasahau niseme naunga mkono hoja ya Waziri wa Katiba na Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza Watanzania kwa kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Miungano mingi imekufa, wamejaribu wenzetu katika Bara la Afrika, katika Mabara mengine, kuna watu wameungana miaka miwili, mitatu, miaka 10, miaka mitano imeshindikana. Sisi miaka 60 imewezekana, hongereni sana Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa niwapongeze waasisi wetu Mwalimu Nyerere na Karume kwa kuasisi jambo ambalo kwa kweli limedumu kwa miaka hii 60. Niwapongeze Marais wote kuanzia Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wa Awamu ya Pili, ya Tatu, ya Nne, ya Tano na sasa tupo na Mama Samia, Awamu ya Sita tunasonga naye mbele na amesema kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiona vinaelea vimeundwa. Tumefikishwa hapa na misingi ambayo ndiyo imelifanya Taifa letu leo tunajivunia. Misingi hii mojawapo ni Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Toka imeasisiwa yamefanyika marekebisho kadhaa, lakini kubwa kuliko yote utamaduni tulioujenga wa kuiheshimu Katiba yetu. Hii Katiba imetuunganisha Watanzania bila kujali makabila yetu, bila kujali dini zetu, bila kujali tunapotoka na imetupa amani na utulivu tunaheshimiana, tunaenda salama kwa sababu hii Katiba imetufikisha hapo. Ukajengwa utamaduni wa kuiheshimu, kuifuata na ndiyo maana tukiapa tunashika Katiba na tumeapa kuilinda na kuitetea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Watanzania 70% mpaka 80 tumezaliwa baada ya Muungano. Kwa hiyo hatujui kule nyuma, sisi tunajua Muungano wetu na ndiyo maana ni muhimu sana Watanzania tukahamasishana kuulinda na kuutetea kwa wivu na nguvu kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya kumeanza kutokea wanasiasa wenzetu na nadhani kwa kufilisika kisiasa wameanza kutomasatomasa utamaduni wa kuheshimu Katiba yetu, utamaduni wa kuheshimu Muungano wetu na wanatumia maneno ya hovyo kidogo ambayo tukinyamaza na tukayavumilia kidogo kidogo huu utamaduni utaporomoka na hivyo tutaliangamiza Taifa letu, ni muhimu tuwakemee. Hapa nataka nitoe mfano, yuko mjomba wangu mmoja anaitwa Tundu Antipas Lissu, juzi akiwa Babati, Mkoani Manyara amesimama mchana kweupe akaanza kukosoa baadhi ya mambo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kukosoa siyo tatizo, lakini alikuwa anakosoa akisema kwamba haya mambo yamefanywa kwa sababu Rais aliyepo ni Mzanzibari. Hili tukilinyamazia litaota mizizi na litabomoa Taifa letu. Hatuwezi kukubali mtu mmoja amelewa na ameleweshwa na utu, ubinadamu, uzalendo na uungwana wa huyu anayemwita Mzanzibari. Lissu alikuwa amekimbia nchi yetu amerudishwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, akalipwa fedha zake, akaruhusiwa kupanua mdomo hadharani kweupe na mikutano ya hadhara, lakini leo kakereka. Kukereka ni jambo la kawaida kwa sababu hatuwazi sawasawa wote. Leo tukiruhusu maamuzi ya Serikali zetu, maamuzi ya viongozi wetu yakakosolewa kwa namna ya anakotokea, kwa jinsia yake, kwa dini yake, kwa kabila lake au ukanda anakotoka, tutakuwa hatuitendei haki nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka kuwaomba Watanzania. Hili jambo limesemwa siku mbili, tatu zilizopita. Nilitegemea chama chake na viongozi wake watamkemea. Kwa kuwa wameshindwa kumkemea nataka tutumie Bunge hili tuwaambie Watanzania wakikemee chama hiki na viongozi wao, na tukitenge, kwa sababu sisi tunaujua Utanzania wetu na makabila yetu yote. Mimi ni Mmakonde, mke wangu ni Mkurya na watoto wangu hata ukiwauliza hawajui ni kabila gani. Leo kila jambo wanasema huyu amefanya kwa sababu ni Mzanzibari angekuwa Mtanganyika asingefanya haya. Halafu bila aibu anakwenda kuwaomba Wazanzibari kura na kuwataka waunge mkono chama chake. Hili jambo lazima tulikatae, kama Watanzania tutumie nguvu zetu zote kulaani na kukemea upuuzi huu ambao unataka kuligawa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais huyu amekuwa muungwana sana, ametumia Katiba hii ambayo, sawa, kama yapo mapungufu ya Katiba, hata ilipotungwa mwaka 1977 siyo hii tuliyonayo, tumekuwa tukirekebisha hapa na pale kulingana na mahitaji na mazingira, hakuna shida, lakini Watanzania tuna utamaduni wa kuheshimiana, hata tukikosoana basi tuheshimiane. Leo anatokea mwanasiasa kwa kutaka tu madaraka yuko tayari kuligawa Taifa letu na anasema kwa kusisitiza kwamba huyu ni Mzanzibari, huyu ni Mtanganyika. Leo tukiruhusu haya tunataka kuligawa Taifa letu. Nimesimama kusema Watanzania tusikubali upuuzi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kusema Watanzania tusikubali upuuzi huu. Nitawashangaa Watanzania waliozaliwa wakati wa Muungano na hata wanaokwenda kumsikiliza mpuuzi huyu. Tumkemee, tumtenge na tumlaani ili awe fundisho kwa wenzake na waache kutumia tamaa zao kuligawa Taifa letu, tusikubali, kwa sababu, kama ana hoja platform zipo. Ni Rais huyu Mzanzibari anayemsema ndiye aliyesema andamaneni, Polisi kawalindeni. Leo walikuwa wanaandamana hapa wamelindwa na Polisi, wamesindikizwa walipoenda. Wamesababisha foleni hapa Dodoma, magari yamesimamishwa ili wao waandamane kwa uungwana wa huyu Mama wanayemtukana. Wote kwa pamoja tumlaani, tumkemee na kwa sababu chama chake kimenyamaza na chenyewe tukizike, tuachane nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viko vyama na watu ambao hawataki kuheshimu Katiba tuliyojiwekea na Mama anasema Katiba yetu siyo Msahafu, ameruhusu tujadiliane na akasema twendeni kwenye mchakato, akaunda timu na wao walikuwemo wengine wakazira. Sasa kama ameshindwa kutumia platform kujenga hoja yake nadhani tusiharibu Taifa letu, tusikubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Waziri wa Katiba na Sheria, napongeza misingi iliyojengwa ambayo imelifanya Taifa letu lifike hapa, I am proud of my nation. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukizitembelea nchi za majirani zetu watu wanaulizana kwa ukabila wao, kwa udini wao, kwa ukanda wao na wanagawana madaraka kwa utaratibu huo. Mwenyezi Mungu amelibariki Taifa letu, makabila zaidi ya 126 hatugawani kwa makabila. Hawa wapuuzi wanaotaka kutugawanya kwa makabila lazima tuwakemee kwa sauti kubwa, lazima tuwalaani kwa sauti kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe, Muungano huu ni wetu siyo wa wanasiasa wachache. Ni kwa ajili yetu, kwa ajili ya watoto na wajukuu wetu na kwa hiyo tuutetee na tuulinde kwa wivu mkubwa. Kama yapo mapungufu ya kikatiba, kisheria na kiutaratibu tukosoane na turekebishe kwa nidhamu, tukosoe turekebishe kwa kuheshimiana, wawe na adabu kidogo. Hili liwe fundisho kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)
(Hapa Wabunge walipiga makofi mfululizo)