Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutualia afya iliyotuwezesha kusimama hapa tukiwa salama ili kuchangia hoja iliyopo mbele yetu, hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kwa mara nyingine na kunipangia majukumu mengine toka Wizara ya Mambo ya Ndani na sasa kuwa Wizara ya Katiba na Sheria kumsaidia dada yangu Mheshimiwa Balozi Pindi Hazara Chana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru pia Viongozi Wakuu wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Wakuu wangu wote kwa miongozo na ushauri unaoniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ufasaha, lakini bila kumsahau kaka yangu Mheshimiwa Engineer Masauni aliyenilea miaka miwili na ushee nilivyokuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana Balozi kwa ushirikiano na mwongozo anaonipa katika kutimiza majukumu yetu ya Wizara. Niwashukuru pia watendaji wa Wizara wakiongozwa na Bi Marry Gasper Makondo, Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Hatibu Malimi Kazungu, Wakuu wote wa Taasisi za Wizara na Watendaji wote katika Wizara na Taasisi za Wizara hii kwa ushirikiano wao mkubwa katika kufanikisha uwasilishaji wa hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, wote kabisa kwa ushirikiano, urafiki na udugu ambao tumekuwa nao wakati wote na wanaendelea kunipa moyo, tutashirikiana vizuri katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hoja hii. Shukrani zingine kwa umuhimu wa pekee kwa familia yangu kwa kuniruhusu na kunikosa mara nyingi ninapofanya kazi za Serikali na kazi zingine za Ubunge bila kuwasahau wananchi wa Butiama ambao wameridhia na kunivumilia ninapokuwa natekeleza majukumu mengi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda sitaweza kuzungumza hoja nyingi, nitamwachia nafasi Mheshimiwa Waziri wangu ili aweze kuzi-cover. Naomba uniruhusu nizungumzie chache kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. Kizito Mhagama kuhusu Mahakama iwe na mpango wa kuongeza matumizi ya mfumo wa tafsiri na unukuzi TTS katika Mahakama zote nchini. Ushauri wa Mheshimiwa Mbunge umepokelewa na Mahakama ina malengo ya kuweka mfumo huu katika Mahakama zote kwa awamu kwa kuzingatia uwepo wa fedha na miundombinu rafiki ikiwemo upatikanaji wa mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Edward Olelekaita amezungumzia juu ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto na Mahakama nyingine za mwanzo zimetajwa na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali. Kuhusu hili la Mheshimiwa Olelekaita nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kulingana na Mpango wa Ujenzi na Ukarabati wa Majengo ya Mahakama, Mahakama ya Wilaya ya Kiteto itajengwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mashimba Ndaki kwanza alipongeza uwepo wa IJC kwa maana ya Integrated Justice Centre na akashauri ziendelee kujengwa katika maeneo mengine. Tunamshukuru kwanza kwa pongezi, lakini tunapokea ushauri wake wa kuendelea kujenga vituo hivi kwani katika bajeti ijayo, vituo hivi vitajengwa katika mikoa tisa kwa maana ya vituo jumuishi katika Mikoa tisa ifuatayo: Geita, Katavi, Lindi, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Singida, Songwe na Pemba. Kwa hiyo, ni dhamira ya Serikali kuona kwamba vituo hivi vinapekekwa katika maeneo mbalimbali ili Watanzania waweze kunufaika kama ilivyoelezwa vizuri sana na Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala lilizungumzwa na Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei kuhusu uchakavu wa Mahakama za Mwanzo katika Jimbo la Vunjo, Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Marangu, Kilema na kadhalika. Mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge yamepokelewa na yatazingatiwa katika Mpango wa Ujenzi wa Mahakama kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ninayoomba kuichangia iliibuliwa na Mheshimiwa Joseph Kakunda ambaye alizungumzia Serikali kuwa na kipaumbele katika kujenga Mahakama za Mwanzo na akasema Sikonge kuna Mahakama moja tu, zinahitajika nyingine katika kata saba zilizo mbali. Mahakama inayo mpango wa kujenga Mahakama za Mwanzo kwa kila Tarafa nchini kwa sasa. Kwa Mwaka 2024/2025, zitajengwa Mahakama za Mwanzo 72 katika wilaya mbalimbali nchini na Mahakama mojawapo itajengwa katika Kata ya Kipili, Wilayani Sikonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia kwenye eneo la Mheshimiwa Joseph Kakunda kwa nini haijatajwa namba ya kupokea maoni ya malalamiko ya Mahakama? Naomba nimtajie namba hii na kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wote, Mahakama ina kituo cha huduma kwa wateja, call centre kwa ajili ya kupokea na kushughulikia maoni, mapendekezo, malalamiko, pongezi na maulizo. Wananchi wanaweza kupiga simu hiyo bure kupitia namba 255800247 na namba nyingine ni 0752500400, pia kuna namba ya kutuma ujumbe mfupi ambao ni 0739502401.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)