Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa. Nikiwa kama Mjumbe wa Kamati, nianze moja kwa moja kwa kuiunga mkono hoja na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo pamoja na msaidizi wake na Watendaji wote wa Wizara ya Kilimo na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye kukiendeleza kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa ushuhuda. Kwenye utoto wangu ilikuwa ni miaka ya 1960, lakini kuanzia miaka ya 1970 nilikuwa kijana. Kuanzia miaka hiyo ya 1970 nimekuwa natoa huduma katika Wizara ya Kilimo hadi leo hii. Kwa hiyo, kuna ushuhuda nataka niseme kwamba, kwa miaka hii ambayo tumeingia huku Bungeni, Bajeti ya Kilimo kwa nia njema ya Mheshimiwa Rais wetu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294 na mpaka sasa hivi tuna bajeti hii ambayo Mheshimiwa Waziri anatuomba pesa ni shilingi trilioni 1.2. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa ushuhuda hapa kwamba mara hii maendeleo na mwenendo wa Wizara ya Kilimo ni mzuri sana. Tumejionea wenyewe kwamba kilimo kinachangia vizuri kwenye Pato la Taifa na kilimo cha sasa hivi kimeleta tija. Mheshimiwa Waziri anapeleka mbolea kule na tija inaonekana ikiwemo kujitosheleza kwa chakula ndani ya nchi yetu na kuna ajira, na vijana wa BBT wapo pale. Pia taasisi zote maendeleo yao ni mazuri sana na zinafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Umwagiliaji pia inafanya kazi nzuri sana, tunaona miradi mingi ya umwagiliaji. Hapa namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwenye Jimbo langu nimeshapata miradi ya umwagiliaji kiasi. Ukanda wa tambarare kule Mandaka Mnono kuna mradi unajengwa. Pale Mabogini kuna mradi ambao ulikuwa ni wa Wajapani, lakini ukanda wa Arusha Chini tunahitaji mradi pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni mengi, ni ya kuua mtu kabisa na sasa hivi wananchi wa Arusha Chini, kwenye vijiji vya Chemchem na Mikocheni kuna mafuriko, watu wapo kambini. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba twende tukawekeze mradi wa umwagiliaji pale Mikocheni na Chemchem maji ni mengi. Haya maji sasa badala ya kutusaidia kuzalisha chakula yanaumiza wananchi na wapo makambini kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utahusu zao la kahawa. Nikiwa kama mtu niliyetoka kwenye eneo linalolima kahawa nitachangia kwenye hili eneo na ndicho kitu ambacho wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wale wanaolima kahawa watapenda wakisikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa ni zao muhimu sana, tunaliita ni dhahabu ya kijani. Zao hili ni bidhaa ya pili kwa umaarufu hapa duniani. Baada ya mafuta ya petrol na diesel kahawa ndiyo zao la pili maarufu hapa duniani. Pia ni kinywaji cha pili kinachotumika duniani baada ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi kama Mwanakilimanjaro naringa sana kwamba tunazalisha kinywaji cha pili kwa matumizi duniani. Inakadiriwa kwamba watu wanaokunywa kahawa duniani wanatumia kama vikombe bilioni 2.6 kwa siku. Wanywaji hawa wa kahawa wanaipenda kahawa kwa sababu ina mambo mengi mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, wataalamu wanasema kwamba kahawa inaondoa msongo wa mawazo, kahawa inaweza ikazuia usipate kisukari (type two diabetes), inaweza ikazuia ugonjwa wa moyo, inaweza ikapunguza maumivu na pia inaweza ikarefusha Maisha. Watafiti wameshaona haya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaringa kwamba mikoa inayozalisha kahawa hapa duniani inachangia kwenye haya mambo kwenye dunia yetu hii. Mikoa hii ni mingi, ipo zaidi ya 12 ikiwepo Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Ruvuma, Lushoto na kule kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa katika maeneo yetu hapa nchini inazalishwa na wakulima wadogo wadogo ambapo duniani kuna wakulima milioni 25 wanaoshiriki kwenye kuzalisha kahawa. Pia sisi Tanzania ni sehemu ya hawa wakulima wadogo wadogo wanaozalisha 80% ya kahawa hapa duniani. Kwa hiyo, tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa kama mzawa wa eneo linalozalisha kahawa, niseme hapa kwamba wakulima wa kahawa kwa ujumla wake wana maisha magumu, siyo jinsi tunavyofikiria ilivyokuwa kule nyuma. Bei wanazopata ni ndogo, hazitoshelezi ukilinganisha na kazi kubwa ambayo ipo kwenye uzalishaji wa kahawa. Zao la kahawa lina kazi ngumu sana na zina gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kahawa ya Arabica, kuna kukata matawi, kuna kufanyia palizi, kuna kuweka mbolea, kuna kupiga dawa, kuna kupukuchua kahawa, kuna kuvuna kahawa, kuna kuchagua na kuondoa zile kahawa mbovu, kuna kukausha na kuisafirisha kuipeleka sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ugumu wa uzalishaji wa hii kahawa kutokana na hivyo vitu ambavyo nimesema wanavifanya wakulima wetu, bei ya kahawa ni ndogo. Kwa mfano, taarifa tulizozipata kutoka kwenye Bodi ya Kahawa kwa mwaka 2022/2023 zimeonyesha kwamba bei ya kahawa ilikuwa shilingi 3,000 kwa kilo kwa kahawa aina ya Arabica na shilingi 2,000 kwa kahawa aina ya Robusta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kilo ya kahawa ambayo tumeuza kwa shilingi 2,000 mpaka shilingi 3,000 huwa ikienda kule nje huzalisha vikombe 120 hadi 140 vya kahawa. Kahawa kilo moja ya kwetu hapa huzalisha vikombe 120 mpaka vikombe 140 vya kahawa na bei ya kikombe kimoja cha kahawa huko wanakoitumia ni sawa na dola 3.5 mpaka dola 3.7. Tukija kwenye pesa za Kitanzania, hiki kikombe kimoja cha kahawa kinauzwa shilingi 8,750 mpaka shilingi 9,300. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima kama nilivyoeleza hapo awali, hupata shilingi 2,000 mpaka shilingi 3,000 kwa kilo moja ambapo hawa wanaokwenda kuinywa kule, mtu anayeuza yule wa mwisho ukizidisha hivyo vikombe 120 mpaka 140 anapata kati ya shilingi 1,050,000 mpaka shilingi 1,300,000. Kwa hiyo, hebu linganisha shilingi 2,000 na shilingi 3,000 mpaka shilingi 1,000,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachoonekana hapa ni kwamba mwananchi anayezalisha kahawa anapata chini ya bei ya nusu kikombe cha kahawa. Kwa hiyo, pamoja na hii bei kuwa ndogo, wananchi hawa wamechangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023/2024, Bodi ya Kahawa imeonyesha kwamba tumeuza tani 81,000 na kuiingizia nchi yetu kiasi cha shilingi bilioni 440.4. Hii inaonyesha kwamba tumevunja rekodi ya mauzo ya kahawa kwenda nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia njema ambayo tunayo, naomba niishauri Serikali kitu kimoja, ili kahawa iweze kuleta tija na wananchi wafurahie hii kazi ya kuzalisha hili zao la kahawa, cha kwanza ambacho ninaishauri Serikali, kwa mfano kwenye Mkoa wa Kilimanjaro, sisi ni wazalishaji wakubwa wa kahawa ya Arabica ambayo ndiyo inapendwa duniani kote. Sasa, shida moja kubwa tuliyonayo kule ni maji. Kahawa inahitaji maji ya kutosha. Muda wote kahawa inahitaji ipate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma tulikuwa na miradi kama ya traditional irrigation project, ilikuwa inahudumia ile mifereji ya asili. Watu wanapata maji wanazalisha kahawa na mazao mengine. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, mimi fedha za Mfuko wa Jimbo nilipeleka kusaidia mifereji ya asili, naomba nao waje waniunge mkono ili turekebishe ile mifereji tupate maji ya kutosha ili wananchi wapate kahawa ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, tumeona disparity iliyopo kati ya bei wanayopata wananchi na kule duniani watu wanavyopata faida kutokana na hii kahawa. Naomba Serikali isaidie wananchi kupata masoko ya uhakika, na tusiwe na ukiritimba ili yule mlaji wa mwisho apate fedha ya kutosha na aweze kunufaika na hili zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitashauri, ninajua Mheshimiwa Bashe ni mtu makini sana, apambane na wale wanaozalisha end products za kahawa, tusindike kahawa yetu hapa hapa nchini. Wakamate wale ma-tycoon wakubwa watano wanaotengeneza products za kahawa, waje waweke viwanda hapa ili tusindike kahawa yetu hapa na tuiuzie hapa hapa ili zile fedha ziweze kubaki hapa nchini na wananchi wetu watapata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwingine ni kuhusu usambazaji wa miche bora ya kahawa. Tumeona kwamba mwaka huu wanategemea kusambaza miche milioni 20. Namwomba Mheshimiwa Waziri, bado tunahitaji miche. Watu wamehamasika, kwa hiyo, miche iongezwe, kwani miche milioni 20 haitoshi. Mikoa inayolima kahawa ni mingi na kwa hiyo, ikiwezekana tushirikishe wadau wengine ili tuweze kuzalisha miche ya kutosha.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Profesa, hitimisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho ni kuboresha huduma za ugani kwa wakulima ili wapate pembejeo kama dawa, kama ilivyokuwa zamani, ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye uzalishaji wa hili zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)