Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Leo naomba mchango wangu ujikite kwa pongezi, kwa sababu kwa kipindi chote niko Bungeni tangu mwaka 2015 sijawahi kuacha kuchangia hotuba ya kilimo. Natangulia kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge siku zote kilio chetu kilikuwa ni kwamba Serikali imfuate mkulima shambani. Serikali hii ilikuwa inamwacha mkulima anateseka, wanakuja kukutana naye kwenye mavuno wakitafuta soko kwa tozo, sijui kwenye mageti, lakini leo hii tuseme ukweli, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inamfuata mkulima shambani na kipima udongo na kumpa ushauri wa kitaalamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii inamfuata mkulima kwa kumuuzia mbegu kwa ruzuku, Serikali hii inamfuata mkulima mdogo kwa kumpa mbolea ya ruzuku, Serikali hii pale mkulima ambapo anakwama kwamba bei ya soko imeshuka, kupitia Wizarani, NFRA inakwenda kununua hayo mazao ili kumnusuru mkulima asipate hasara, vilevile hali ya mavuno ikiwa mbaya Serikali hii inaleta chakula cha msaada. Jamani Serikali hii kupitia Wizara ya Kilimo inaupiga mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii haijarudi nyuma, leo inaandaa mpango wa miaka 25 kwa ajili ya kwenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye kilimo. Naomba kuwaambia, waweke mfumo mzuri wa kupokea ushauri ili wapate ushauri hadi wa wakulima ambao hawajui kusoma na kuandika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba, hizi documents za Mpango huu ziwepo kwenye lugha zote mbili; Kiswahili pamoja na Kiingereza. Serikali hii imebuni kuanzisha ajira mpya milioni tatu ambazo wamejikita kwa wanawake na vijana na leo hii wameanzisha mashamba makubwa ya pamoja, yaani Miradi ya BBT, na vilevile ni wasikivu na wanapokea ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili liliwashauri kwamba pamoja na hizi mpya, wawafuate wakulima kule site walipo. Leo hii kupitia bajeti ya mwaka huu tunaona wanaenda kupeleka miradi ya BBT kwenye halmashauri 100. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kuna hizi halmashauri zenye maneno kama mji au jiji, watukumbuke, kwa sababu siyo zote ni ya mjini, wengine tuna mashamba. Pale kwangu mimi ni Diwani wa Halmashauri ya Kondoa Mji, tunayo Skimu ya Umwagiliaji ya King’ang’a Mtaa wa Iyoli Kata ya Kingale, pale tuna ekari 30,000. Tunaomba watuletee ili vijana na akina mama wa Halmashauri ya Kondoa Mji waweze kujiajiri na waweze kunyanyua uchumi wa mtu mmoja mmoja.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa kwa mzungumzaji. Anazungumza vizuri sana, lakini ningeomba amwombe pia Mheshimiwa Waziri kujumuisha siyo wanawake na vijana peke yake, iwe ni pamoja na watu wenye ulemavu. Ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam, unapokea hiyo Taarifa.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa, lakini pia niongezee hapo kwenye jiji, Mheshimiwa Spika ndiye kiongozi wa Bunge letu, tusimsahau. Halmashauri ya Jiji la Mbeya haina mradi wa umwagiliaji. Naomba kwenye hitimisho naye useme neno ili kiongozi wetu wa mhimili naye apone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, BBT hii leo kwa ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na Wizara imepitisha, inakwenda kutoa mikopo kwa vijana na wanawake ambao tayari wamejiajiri katika kilimo. Jamani Serikali hii pamoja na miradi mikubwa ya umwagiliaji, bado inakwenda kuchimba kisima kule kwa mkulima wa chini kabisa. Jamani naomba mmwage makofi mengi na mumpatie maua yake Mheshimiwa Waziri Bashe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na kilio kikubwa kuhusiana na tafiti. Tumeona ana mpango wa kuanzisha Genebank. Mimi nimekuwa ni muumini wa kuitaka Serikali isiache teknolojia. Dunia sasa hivi inaongelea GMO, kwa hiyo, tuanze tafiti tujue kibaya ni kipi na kizuri ni kipi ili sisi wenyewe tujiamulie kuliko kusikia tu makelele. Kwa hiyo, suala la uanzishwaji wa Genebank naona sasa ile hoja yangu niliyokuwa naisema muda mrefu sasa inafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waziri hapa aliwahi kufunga mipaka wakati watu wamezalisha mahindi ya kutosha, hakurudi Bungeni, lakini tumeona kwa Mheshimiwa Bashe, Mungu atampa baraka kwa kufungua masoko na kumruhusu mkulima. Basi Wana-Nzega watamrudisha kwa kishindo na tunamwomba Mheshimiwa Rais amwache akamilishe Ajenda 10 - 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongee kama Mbunge wa Mkoa wa Dodoma. Dodoma tumekuwa tukilima kinyonge miaka yote kwa sababu ya hali yetu ya hewa tuliyokuwa nayo. Ni hali ya nusu ukame na mvua zinakuwa finyu; lakini ardhi yetu sisi ina rutuba na inakubali mazao yote ya chakula pamoja na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilifikia hatua tukaambiwa Dodoma tusilime mahindi. Kwa mara ya kwanza tangu uhuru wa hii nchi ni Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Wizara ya Kilimo chini ya Mheshimiwa Bashe, leo hii tunayo miradi 29 kwenye wilaya zote saba za mkoa wetu, ambapo miradi hii ikishakamilika tutakuwa na hekta za umwagiliaji zaidi ya 70,579 ndani ya mkoa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na wakulima wa Mkoa wa Dodoma na kwa vile dira ya nchi ni kujilisha, sisi pamoja na Afrika na dunia, Mkoa wa Dodoma unaenda kujilisha wenyewe na unaenda kulisha nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye BBT sisi ndio pioneers, tunayo miradi mikubwa ya kwanza ya BBT pale Chinangali pamoja na Ndogowe ambako kuna zaidi ya ekari 11,000; na kwenye ekari hizo, ekari 1,000 Wizara imewapa wananchi wangu wa pale. Pokea salaam kutoka kwa Mwenyekiti wa Mlazo, na anasema Jumatatu atakuwepo hapa ili tuweze kuongea kwa ajili ya maendeleo ya mradi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo naomba nichomekee kwamba halmashauri zote zimepata miradi ya hizi skimu za umwagiliaji na mabwawa isipokuwa Halmashauri ya Mji wa Kondoa ambayo mimi ni Makamu Mwenyekiti wake, na jana ameshuhudia nilivyommiminia sifa kwa niaba ya Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana, 2023 nilimwomba na akanipa mradi kwenye Mwongoroma Irrigation Scheme, lakini sijaiona kwenye karatasi zake. Naomba Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha aseme neno ili mimi, vijana wangu na wanawake wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa tupone kupitia mradi huu wa Mwongoroma Irrigation Scheme wenye zaidi ya ekari 3,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba niipongeze sana Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, inafanya kazi kubwa. Bila upendeleo nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu, Ndugu Raymond Mndolwa. Sisi kama Kamati tumetembelea miradi yake, anajua kila detail, hadi rangi ya kupaka, halafu huyu ni mwana CCM mzuri ndiyo maana majengo ya pale Chinangali ni ya kijani, na huo ndiyo utekelezaji wa ilani. Achape kazi, kwani Mheshimiwa Rais amemwamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe. Vilevile huyu ni muumini wa jinsia “ke,” zaidi ya 80% ya watendaji wake pale kwenye Tume ni akina mama na ndiyo maana mambo yanaenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali watoe fedha za kutosha na kwa wakati ili kurahisisha kazi ya Tume ya Umwagiliaji kwa sababu upelekaji wa fedha siyo mzuri. Kwa hiyo naomba warekebishe, kwa sababu tunasema kilimo cha umwagiliaji ndicho kilimo cha uhakika. Nawapongeza kwa kutenga fedha kwa ajili ya feasibility study pamoja na detailed design. Sasa wasije wakapotoka, wasifanye miradi bila ya feasibility study na detailed design. Huo ndiyo uwe msimamo wao. Miradi mingi imekufa kwa kukosa feasibility study na detailed design.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, tunalalamika kwamba maduhuli siyo mazuri kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, nashauri kwamba hebu sasa wakae na Wizara ya Kilimo, wateue maeneo na wayarasimishe ili sasa hii Tume iende kuingia PPP na hivyo iweze kujiendesha na kutuletea vyanzo kwa sababu uwekezaji unaofanyika na Serikali ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusiana na zao la zabibu. Nakumbuka jitihada za aliyekuwa Naibu Waziri wake ambaye sasa hivi ni Waziri wa Madini, na alishirikiana naye sana katika kuanzisha Ajenda 10 - 30; alikuwa ni pioneer sana wa zao hili. Hili ndilo zao letu la asili Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba hata tuwe na bodi ndogo ya zao hili. Leo hii tuna zabibu kavu tunaingiza kutoka nje, tuna zabibu za meza wakati tunaweza kuzalisha, lakini watu wanakamua michuzi hawana sehemu ya kuweka. Naomba Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha, aseme neno ili wakulima wa zabibu wa Dodoma wapone. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kumalizia. Ninao ujumbe wa kutoka kwa wanawake wa Mkoa wa Dodoma. Kwa kweli tumeona namna gani Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyompa kipaumbele mwanamke. Kwenye uzalishaji wa kilimo mwanamke utamkuta shambani, utamkuta sokoni akiuza mboga mpaka pamoja na nafaka. Mwanamke huyo alikuwa hapewi kipaumbele, lakini leo miradi yote, mipango yote mikubwa ya Wizara ya Kilimo mwana mama anawekwa, mwanamke anathaminiwa, na kwa kweli hiyo ni heshima kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia na wanasema hivi, hawayumbishwi na maneno ya wakosaji. Ukishawashinda kwa hoja, watakuja na viroja. Haya ninayoyasema ni msimamo thabiti. Kule Kondoa wananiita Kivaravumba, kundi liko nyuma. Nikisema akina mama wamenituma, namaanisha kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wanachokiomba, Mwenyezi Mungu ampe afya Mheshimiwa Rais, uzima, na utimamu wa kila kitu. Mwaka 2025 wanasema Samia wanaye na wanatamba naye. Wao wanachosema watamuunga mkono kwa wao kugombea nafasi za kuchaguliwa kuanzia Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji pamoja na Uchaguzi Mkuu, kwa maana ya Udiwani na Ubunge. Mimi mwenyewe binafsi wameniomba nikajaribu jimboni, na nimekubali nitamuunga mkono Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, naomba hitimisha.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Mkoa wa Dodoma wanasema wanaunga mkono kauli ya Katibu Mkuu wetu, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi aliyesema mwakani fomu ni moja na fomu ni ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wapo watu wenye viroja ambao wanatumwa tumwa kwenye mitandao kusema eti Katibu Mkuu amevunja demokrasia…
MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba uhitimishe, muda umekwisha.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama chetu kinaongozwa na Katiba na Kanuni…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: …lakini tuna utamaduni wetu na heshima tulishajipangia, Rais aliyekuwepo madarakani,…
MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba uhitimishe hoja yako.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: …Rais aliyepo madarakani habughudhiwi, hafananishwi na yeyote. Tunamwongezea muda wake kwa mujibu wa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Naomba umalize Mheshimiwa.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: …tunamwongezea muda Mheshimiwa Rais amalizie, leo kilimo tuna Ajenda ya 10-30 chini ya maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwingine wa nini? Fomu ni moja, na ni ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, naomba kuunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)