Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nitoe mchango wangu kwenye bajeti hii muhimu kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye yeye kwa uwezo na neema yake ndiye ametuwezesha leo tuko hapa tukijadili mambo kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza kwa dhati kabisa mbeba maono namba moja wa nchi hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Ukiangalia Wizara ya Kilimo ilivyo sasa hivi, fedha inazotengewa na kupelekewa ni ishara kwamba Mheshimiwa Rais yuko kazini na ana nia ya dhati ya kuwatumikia Watanzania. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jambo hili kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Bashe, yeye na Naibu Waziri na watendaji Wizarani. Kwa kweli Wizara ya Kilimo wanatutendea haki, wanafanya kazi nzuri. Hatuna deni na ninyi zaidi ya ushauri kwenye maeneo machache na kukumbushana vitu vichache ili kuboresha na kuendeleza kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo naomba nichangie kwenye maeno matatu. Eneo la kwanza nitachangia kuhusu kilimo cha umwagiliaji, eneo la pili ni zao la chai na eneo la tatu ni zao la mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2019/2020 eneo lililokuwa linafaa kwa shughuli za umwagiliaji na lililokuwa linatumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji lilikuwa ni hekta 475,052. Leo kupitia taarifa ya Mheshimiwa Waziri, nasi wenyewe tunajionea, eneo linalofanya kazi kwa shughuli za umwagiliaji limefika hekta 727,280.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama miradi ikikamilika, kwa mujibu wa taarifa na maelezo na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, tutafika hekta 983,466 sawa na 81.9% ya malengo tuliyowekewa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni kubwa sana, Tume ya Umwagiliaji na Wizara ya Kilimo wanastahili pongezi kwa kazi hii kubwa na nzuri wanayoifanya. Tunawaomba waendelee na kazi hii, na tuongeze eneo linalofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa sababu umwagiliaji ndiyo maisha na ndiko kufanikiwa kwenye kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mambo machache kuhusiana na eneo hilo hilo la umwagiliaji. Moja, namshukuru Mheshimiwa Waziri, yeye ni mtu wa vitendo na anatimiza ahadi zake. Tumekaa naye katika vikao vingi tangu akiwa Naibu Waziri tukihangaika na Bwawa la Mkomazi na Skimu zake ambazo alituahidi. Leo tunapozungumza, kazi iko zaidi ya asilimia saba kule kwenye Bwawa la Mkomazi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto ndogo na pengine Wizarani wanapata hofu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba, najua mimi siyo mtakatifu, lakini nina hofu ya Mungu na ninajua kuna Mungu. Namhakikishia, kama Mungu aishivyo, Mradi wa Mkomazi utatekelezwa kwa sababu ndiyo dhamira yetu, ndiyo nia yetu, ndiyo maisha yetu, ndiyo uhai wetu na ndiyo uchumi wetu, aondoe wasiwasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alikuwa kwenye lile eneo, amezungumza na wananchi, wako wananchi wamepata hofu. Niwatoe hofu wananchi wenzangu wa Kata za Mkomazi, Mkumbara, Mazinde na Mombo kwamba mradi huu hatutakubali hata siku moja ukashindwa kutekelezwa. Kama Mungu aishivyo, mradi huu utatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mheshimiwa Waziri, tulikubaliana kuhusu Chekelei, tumeona wameshatangaza, tunamshukuru sana. Ninao ushauri kwenye maeneo machache kwenye eneo hilo la umwagiliaji. Moja, miradi ya umwagiliaji inatumia fedha nyingi sana. Naomba Wizarani waweke utaratibu thabiti kabisa wa kufanya miradi hii iwe endelevu na isiwe kwamba baada ya kujenga na kumaliza, baada ya miaka mitatu minne tunaingia kwenye changamoto, miradi inakuwa ni changamoto na mingine haifanyi kazi vizuri. Tuweke utaratibu endelevu, wananchi waelimishwe ili miradi hii iwe endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Tume inapewa fedha nyingi sana na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi hii. Ushauri wangu, huko tunakokwenda tuangalie, pamoja na kwamba hii ni huduma kwa wananchi wetu, tuangalie namna ya kuijengea uwezo Tume, isikae kwa asilimia mia moja kusubiri kupewa fedha na Serikali, kuwe na namna mbalimbali za kuifanya Tume kutengeneza mapato ili mambo yake yaweze kuwa mazuri na hivyo waendelee kukarabati skimu hizi na mambo yaendelee kuwa endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana, 2023 tulizungumza na tukaenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri, tukakaa tukazungumza kuhusu ukarabati kwenye Skimu za Mombo, Mafreta na Kwemazandu. Ninamshukuru nimeiona kwenye kitabu cha hotuba. Ombi langu ni moja, kwamba Skimu ya Mombo mwaka 2021 tulikwenda na Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye akiwa Naibu Waziri, tukazungumza kuhusu Skimu ya Mombo, pembeni kuna eneo la Kwamkumbo ambapo mto ule umejaa udongo, maji yanapoteza mwelekeo yanaingia kwenye mashamba ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 tulizungumza na Mheshimiwa Waziri, tulienda ofisini kwake tukakaa na tukazungumza kuhusu ukarabati kwenye scheme za Mombo, scheme ya Mafreta, kwenye scheme ya Kwemazandu, ninakushukuru nimeiona kwenye kitabu cha hotuba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni moja, scheme ya Mombo mwaka 2021 tulikwenda na Mheshimiwa Waziri wewe ukiwa Naibu Waziri, tukazungumza kuhusu scheme ya Mombo pembeni kuna eneo la Kwamkumbo, ambao mto ule umejaa udongo, maji yanapoteza mwelekeo yanaingia kwenye mashamba ya wananchi. Sasa unapokwenda kukarabati scheme hii ya Mombo, tuhakikishe kwamba tunaweka package kwa ajili ya kutengeneza eneo la Kwamkumbo ili wananchi wetu wafanye kilimo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mheshimiwa Waziri, kama tulivyokubaliana ameweka kwenye bajeti yake kwenda kufanya upembuzi kwenye scheme za Magoma na Kwakunda. Ombi langu, tulitembea naye kule Korogwe; ukipita pale kwa Mdole kule kwa Mufti upande wa kulia mpaka unafika Magoma, ni bonde na maji, yanapotea. Pamoja na Kufanya upembuzi kwa ajili ya ukarabati katika Scheme ya Magoma, tunaomba tuweke mpango wa kujenga bwawa ili mambo ya watu wa Magoma yawe mazuri na mazao yao yasiondoke wakati wa mafuriko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka kuchangia ni kwenye eneo la zao la chai. Mheshimiwa Waziri, sina mashaka na Bodi ya Chai, wanajitahidi na wanafanya vizuri. Nilisoma kwenye website ya Wizara, taarifa ya tarehe 15 Februari, 2022, karibu nusu ya wakulima wa chai tulionao ni wakulima wadogo, lakini zao la chai linakabiliwa na changamoto kubwa mbili; changamoto ya kwanza ni bei ya chai kwamba ni ndogo na inaumiza sana wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba natambua changamoto hii ya bei ya chai inachangiwa sana na bei ya soko la dunia, naiomba sana Wizara, Bodi ya Chai na taasisi nyingine, tuweke mkazo kwenye kuongeza ubora wa chai yetu ili iweze kwenda kushindana vizuri kwenye masoko, tuweke mkazo, tuweke uwekezaji kwenye mnyororo wa thamani ili tunapozalisha chai na kuipeleka kwenye soko, iweze kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, kama nilivyosema zaidi ya nusu ya wakulima wa chai ni wakulima wadogo, lakini sehemu kubwa ya wakulima wadogo wanategemea viwanda vya wakulima wakubwa ambao wanawekeza kwenye mashamba makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ni kule Korogwe, Mheshimiwa Waziri ni shahidi. Mheshimiwa Waziri, wiki iliyopita tulizungumza na alifanya mawasiliano, nampongeza kwa juhudi alizozifanya kwenye Kampuni ya Mohammed Enterprises, jana wamefungua kiwanda na wameanza kuchakata chai ya kwao wenyewe na wanajiandaa kwenda kununua chai ya wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii changamoto imekuwa ikijirudia mara kwa mara. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, ombi na ushauri wangu, hebu Serikali ione namna ya kukaa na hao wawekezaji. Kama hakuna uwezekano na hawawezi kuendelea na kazi ya uzalishaji, tutafute namna ya kuongeza nguvu tuwape wakulima wadogo hivi viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Kenya 75% ya viwanda vilivyopo Kenya vinasimamiwa na wakulima wadogo (ni viwanda vya wakulima wadogo). Tuone namna ya kuwapa nguvu wakulima wadogo wawe na viwanda vyao na wasitegemee viwanda vya wawekezaji ili mwekezaji akiyumba mambo yao yasiyumbe na biashara ya chai iendelee kuwa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho nichangie kwenye eno la Katani (Mkonge). Nampongeza Mheshimiwa Waziri, na tunaishukuru Serikali hasa sisi watu wa Mkoa wa Tanga kwa kufufua na kurejesha zao la mkonge kwenye ramani ya mazao ya nchi yetu, mmefanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza, tumeongeza uzalishaji, tulikuwa tani na 36,000, leo tunazungumza mkonge, tuko kwenye uzalishaji wa nyuzi zaidi ya tani 56,000 sasa. Pia kuna changamoto na nimewahi kuisema na nitaendelea kuisema siku zote mpaka tutakapoelewana vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizi tani 56,000 tunazozalisha za nyuzi za mkonge, 70% tunapeleka nje. Tafsiri yake rahisi ni nini? Tunakwenda kuuza ajira za watu wetu, tunakwenda kuuza kodi za kwetu na pia tunakwenda kuishi kwa kutegemea soko la wenzetu. Zikitokea changamoto kama ilivyotokea kwenye COVID, wakulima wetu wanaingia kwenye matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, najua anaweza, aongeze nguvu kwenye kuimarisha soko la ndani la mkonge hasa kwenye kuimarisha viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema humu ndani mara nyingi, bado tuna changamoto ya nyuzi za plastic, bado tuna changamoto ya uingizaji mkubwa wa magunia ya duty, tukiweka vizuri maeneo hayo, tutafanya vizuri. Leo kwenye nchi hii, mahitaji ya gunia kwa mwaka ni zaidi ya piece milioni 15…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Naomba uhitimishe.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamepewa viwanda. Namshauri Mheshimiwa Waziri, hebu akae na watu waliopewa viwanda vya kamba na viwanda vya magunia ili tusiuze ajira za watu wetu. Tuhakikishe usalama wa soko la watu wetu kwenye eneo la Mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.