Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Wizara muhimu sana katika Taifa letu. Tunafahamu kabisa, bado sijaamini kama tumeacha ule msemo uliokuwa unasema, Kilimo ni Uti wa Mgongo. Ninaamini bado tunaendelea nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wenzangu, tunampongeza Mheshimiwa Waziri, kwani ni mtu unayeweza. Sasa naomba katika kuweza kwake, kuna shida kubwa sana na anafahamu mimi na yeye tunaongea mara nyingi kuhusu suala la wakulima wa chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri achukue juhudi za makusudi, kwanza kufika katika Wilaya ya Rungwe na kuonana na wakulima bila kupitia njia nyingine yoyote. Kwa nini nasema hivyo? Tunapozungumzia chai, ni zao ambalo limewapa fedha wazazi wetu miaka na miaka. Nimeona juhudi unazozizungumzia, pia tulikuwa na kikao cha wadau ambao watu waliokuwepo, na Waziri kama kiongozi wetu, alitoa tamko kwamba, kiwanda cha MO cha Rungwe kisifungwe, kwa sababu kikifungwa wale wakulima wanaolima chai watauza wapi, wakati muda waliokuwa wameutoa siyo muda ambao wale wakulima wamejiandaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwambia Mheshimiwa Waziri kwamba kiwanda kimefungwa, wafanyakazi wamesimamishwa bila taratibu za kazi tunazozijua, watu wako nyumbani wameondoka na hawajui hatima zao zikoje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu Mheshimiwa Waziri aliniambia ametuma timu yake. Bado nina mashaka na timu. Naomba yeye kama Waziri, najua Waziri ni taasisi, ana watu wake, lakini kuna maeneo kama Taifa yanayosumbua, tunaomba Mheshimiwa Bashe afike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo mwanzo, chai ni zao muhimu sana. Tuna Kiwanda cha Busokelo na Kiwanda cha Katumba. Leo hii viwanda hivi vyote havieleweki. Unafahamu kabisa Katumba imeanza kuuza baadhi ya majengo, inawapa shaka sana wakulima. Leo hii wanakwambia kwamba wanarudisha vile viwanda kwa wakulima. Mheshimiwa Waziri, wakulima hao ni akina nani? Kuna watu wanajiita AMCOS. AMCOS ni familia zinajiunga, zinajisajili na kuwaacha wakulima kwa zaidi ya 2,000 ambao ndio wenye mali na ndio wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ya umuhimu wa kuunda Tume. Natambua Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwahi kuunda tume, lakini hatukuwahi kupata majibu. Sasa basi, kwa sababu tunaingia mwaka mpya wa Serikali, naomba uunde tume iende chini ikasimamie ugawaji wa vile viwanda hasa Busokelo na Katumba virudi kwa wakulima wa Wilaya ya Rungwe ili uchumi wa Rungwe uendelee na wakulima wasiyumbishwe kabisa katika uuzaji wa chai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la parachichi limezungumzwa na wenzangu wa Njombe na sisi Rungwe tumeshasema kwamba, hii ni dhahabu ya kijani, lakini leo hii mizani inayotumika na wauzaji na madalali imekuwa ni feki na inawadhulumu wakulima haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii madalali, kwa sababu nafahamu kuna hawa Herb Africa, wananunua kwetu kwa 80%; nilikuwa naongea na yule kiongozi ambaye Waziri amemleta hapa kwenye maonesho kwamba, kwa nini msiende moja kwa moja kwa wakulima kuliko kutumia madalali? Leo hii dalali ananunua parachichi anakwambia 50% ni reject. Hiyo reject kwa macho ya nani? Kwa sababu yeye ni mnunuzi, ameshashusha chini ya mti, anasema haya maparachichi ni reject? Naomba tuwasimamie wakulima wetu. Mwisho wa siku tunataka tuwajenge Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Rais ameongeza bajeti ya kilimo. Nafahamu hizo ni jitihada kubwa sana. Basi ikawasaidie, na kama ni keki ya Taifa, wakulima wote tukapate sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu masoko. Leo hii masoko ni shida. Nafahamu yananunuliwa, sawa. Hata hivyo, kwa nini tusiweke AMCOS ambazo ni za kweli, siyo zile za kwanza nilizozisema? Kama wakulima waliopo katika vikundi, tupeleke moja kwa moja Uswisi, Dubai, na kadhalika badala ya kutegemea makampuni binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalalamika, hakuna ajira, lakini tuna uwezo wa kukusanya vijana wetu kwa kutumia ile mikopo ya asilimia 4.4.2, kwa maana ya asilimia nne wanawake, asilimia nne vijana na asilimia mbili za watu wenye ulemavu; tukawaunganisha huko, tukawasaidia kama Taifa, wakauza nje badala ya kupita katikati kama madalali hapa katikati. Mheshimiwa ninafahamu unaweza na ukiamua unaweza, ninaomba usimamie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Rungwe ndizi ni zao kubwa sana. Leo hii nchi za Jamaica zinanunua silaha kwa kuuza ndizi. Kwa nini sisi tunashindwa? Kwa nini tusihakikishe kwamba ndizi ni zao la kibiashara, wawe wanakuja watu binafsi kutoka Malawi na Zambia kununua ndizi ya Rungwe? Kwa nini tusisimamie tukaweka mkazo hapo na kusaidia vilevile kuuza huko nje? Viwanda vidogo vidogo ndilo suluhisho la mkulima wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalifahamu kabisa zao la kahawa kwamba ni zao zuri sana na wakulima wamejitahidi sana kuendeleza zao hili, lakini malipo yao yanachukua mwezi mpaka miezi mitatu mkulima hajalipwa kahawa yake. Leo hii utakuta msimu mwingine anataka kununua mbolea, pesa ziko kwenye vyama vya ushirika, hawajalipwa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri asimamie hilo. Ninajua kuna Bodi za Kahawa na Bodi za chai, naomba tusimamie wananchi wetu waweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye zana za kilimo. Rais wa Awamu ya kwanza aliweka viwanda kwa makusudi kabisa. Kule Mbeya tulikuwa tuna ZZK kwa ajili ya kusaidia vifaa hivi. Naomba sana tuwekeze na bajeti yetu ijikite zaidi kwenye zana za kilimo ili kuwasaidia wakulima. Suala la mbolea amekwenda nalo vizuri, lakini bado tunaomba nguvu iongezeke ili tuweze kufanikisha wakulima hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba kurudia tena, kwa sababu ni la muhimu sana, kwamba viwanda vinavyofungwa vizuiwe. Hakuna haja ya kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu jitihada anazozifanya tunaziona. Tukianza kugombana kwa kushika shilingi, nafikiri wakati mwingine tutamkatisha tamaa. Naomba alisimamie hilo, tusifike mahali pa kuleta hoja binafsi kwa sababu tu ya wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wawekezaji hawa wengi wanatoka nchi za jirani, isije ikawa wanafanya hivyo kwa makusudi, wanatuharibia huku Tanzania, lakini kwenye nchi zao kahawa inaendelea na chai inaendelea. Kwa sababu wengi wanatoka nchi jirani, sitaki kuitaja kwa sababu ya mambo ya kiusalama na mambo ya kiurafiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana watu wetu wa TISS na wengine wafuatilie hawa wawekezaji kwamba wanakuja kuwekeza, kutuharibia au kutusaidia! Kwa sababu anakaa miaka mitano, halafu baadaye kiwanda kinakufa, lakini kwake ana kiwanda hicho hicho na kinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, majibu ya Mheshimiwa Waziri yatatufanya tufurahi au tunyang’anyane mshahara ili kuhakikisha kwamba haki za Wanarungwe na Wanajombe wote zinakuwa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono hoja. Kipindi Mheshimiwa Waziri atakapojibu swali langu vizuri ndiyo hoja itaungwa mkono na vinginevyo haitawezekana. Ahsante. (Makofi)