Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Moja ya jukumu la Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha usalama wa chakula. Hilo ni moja ya jukumu la Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu, Serikali imehamia Dodoma. Jiji la Dodoma sasa ni kioo kwa maana ya kwamba ndipo Makao Makuu ya Serikali. Idadi ya watu wameongezeka na watu wengi wameendelea kuingia katika mji huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba, Serikali ni lazima iangalie hali ya maisha ya wananchi katika Jiji la Dodoma na wilaya zinazozunguka. Nataka niseme, bado Serikali haijaonesha mkakati wa kuweka umadhubuti kwamba, pamoja na maendeleo makubwa tunayoyaona ndani ya Jiji la Dodoma, lakini ukitoka ndani ya wilaya zake, hakuna mkakati wa kilimo unaoonekana. Nnataka niliseme hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba, kwa mfano ukija Wilaya ya Bahi, tunalima mpunga na tuna scheme kubwa sana na ile scheme ilijengwa mwaka 1984, lakini haijawahi kufanyiwa ukarabati, na ni scheme kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Bahi ilipo, scheme ile inapitika na ndipo lami inapopita kutoka Singida, ipo karibu na mji lakini productivity yake iko chini kwa sababu haijakarabatiwa. Sasa huu ni mwaka wa nne Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amekuwa ananiweka kwenye upembuzi yakinifu. Pia, safari hii tena ameniweka kwenye upembuzi yakinifu. Kwa hiyo, hii ninaiona pia imetoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme, alikuja Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Chongolo na akaahidi akasema tunaanza ukarabati na wananchi walisikia. Mimi nikasema kweli kwamba sasa ukarabati unaanza, lakini hakuna ukarabati na leo niko kwenye upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nataka niseme, Serikali na kwa Mkoa wa Dodoma, bado hakuna mipango ya kuondoa umasikini kupitia kilimo. Mbegu za uwele tunazozitumia ni zile zile na productivity yake iko chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwa ruzuku kwa mwaka 2023 ni shilingi bilioni 136. Njoo Dodoma uone kama tumepata ruzuku hata shilingi milioni 300, tena kwa mkoa mzima! Sisi ruzuku hatupati. Kama hatupati ruzuku, basi hata mbegu si mtufanyie utafiti. Kwa hiyo, mbegu tunalima zilezile, hela ya ruzuku kwetu sisi hatuioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Bashe, yeye ni zao la Kanda ya Kati, hawezi kuitofautisha Nzega na Dodoma, kwani hali ya hewa ni ile ile. Hata hivyo, hakuna programu za utafiti wa mbegu na mbegu hatupati. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri hilo aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu matumizi bora ya ardhi. Nchi yetu akija mwekezaji anayetaka ekari 5,000 au 6,000 kwa Pamoja, hawezi kuzipata. Ndiyo maana hata uwekezaji kipindi kile Zimbabwe wale Wazungu walipopata shida pale, walishindwa kuja kwetu. Kidogo walibahatisha Zambia, sisi hatuna ardhi. Tuna ardhi kubwa ya maneno, lakini ardhi ya kilimo hatuna, na hatuna kwa sababu ya sera zetu kwamba hatuzidhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vijijini, kuna uholela. Mtu anakuja anaweka beacon tayari ameshategesha pale. Akija mwekezaji, ina maana yule mtu wa kawaida ametangulia kuliko Serikali. Kwa hiyo, ardhi yetu katika kilimo kumekuwa na uholela mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Bashe sisi alitupatia na akatuomba tutenge eneo kwa ajili ya BBT. Tumetenga ekari 3,500, sasa zile ekari watu wanazinyemelea kwa sababu ule mkakati hauonekani. Sisi kule tumetenga lile eneo na bahati nzuri barabara inatengenezwa, tumepeleka maji pale katika Kijiji cha Ikumbulu, tumejenga zahanati na tunawaambia kwa sababu unakuja mradi mkubwa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Bashe hilo nalo aliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Serikali katika vipaumbele vyake kwenye kupunguza kuagiza ngano na mafuta ya chakula. Tumekuwa na matamanio hayo, lakini mkakati madhubuti hauonekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye alizeti ambayo ndiyo inaleta mafuta ya chakula, bado hatujawa na strategic plan kuhusu zao la alizeti; ipo kwenye vile vipaumbele vikubwa, lakini mkakati wa alizeti hauonekani. Kutokuwa na mkakati ndiyo maana hata mbegu bora za alizeti sisi hatupati. Mmewahi kutuletea mbegu pale Bahi, ilirefuka kama mita tatu, mvua inaisha na yenyewe bado inarefuka. Kwa hiyo, tunaomba mbegu ya uhakika kwenye alizeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la ngano kama nilivyosema, nchi hii hatujaamua, tatizo lililopo ni kwamba ardhi tunayo, lakini ni uthubutu, bado tunaendelea kuagiza ngano hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka niseme kwenye suala zima la ardhi ambalo nimesema, akija mwekezaji hapa, Tanzania Investment Center wanafanya kazi kubwa sana katika maeneo mengine. Nilikuwa naomba kwenye suala la ardhi washirikisheni na mwapatie baadhi ya maeneo makubwa TIC waweze kushikilia. Wamefanya vizuri kwenye suala zima la kuleta wawekezaji kwenye viwanda, lakini kwenye suala zima la ardhi bado kuna shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka niseme kwa dhati, Taifa lolote duniani ni lazima kwanza lipate udhibiti mkubwa wa maendeleo ya kilimo na kilimo sisi tunasema kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu. Naona mawazo ya Mheshimiwa Waziri ni ya ku-transform nchi hii. Tunaomba Serikali imuunge mkono, falsafa hizi ambazo anazo za kutaka ku-transform nchi katika kilimo, basi Serikali itoe fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli fedha zinakuja nyingi, lakini njoo katika utekelezaji, haijafika zaidi ya 50%. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali iangalie, bado tunahitaji fedha katika kilimo, lakini bado kilimo chetu hakijawa na tija cha kuleta wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)