Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Alfred James Kimea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara ya Kilimo. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kuendelea kutupa nguvu, afya na uhai ambao unatuwezesha kuendelea kulitumikia Taifa la Tanzania, lakini hasa wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo kwa Mwenyezi Mungu, niruhusu nimpongeze Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa chama changu cha CCM kwa namna ambavyo anawajali wananchi wa Tanzania. Tunaona namna Serikali ambayo inaongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyoendelea kuongeza fedha kwenye sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Kilimo inaajiri Watanzania zaidi ya 85%. Kwa hiyo, namna Rais wetu anavyoongeza fedha kwenye sekta hii, inaonesha ni namna gani anavyowajali Watanzania, hasa Watanzania wanyonge ambao wengi wamejikita kwenye sekta hii ya kilimo. Kwa hiyo, nampongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyoendelea kutekeleza ilani ya chama chetu ya mwaka 2020/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, kwa kazi hii kubwa ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais, ni dhahiri kwamba, Watanzania wanamwelewa na Watanzania mwakani wako tayari kumlipa kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa hiki kipindi kifupi ambacho yuko madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wangu wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natumia fursa hii kwa kifupi sana kuwapongeza Watendaji Wakuu kwenye Wizara hii; Mheshimiwa Waziri Bashe na Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Silinde, kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kuongoza Wizara hii na ku-transform Sekta hii ya Kilimo kwa vitendo. Ndugu zetu hawa ni mahodari sana na wamekuwa na ushirikiano mkubwa na Waheshimiwa Wabunge pale tunapokuwa na changamoto zetu. Kwa hiyo, tuwashukuru sana na kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache sana leo ya kuchangia. Jambo la kwanza, nitachangia kwenye issue ya masoko na la pili ni kwenye sekta ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa kwenye sekta ya kilimo ni upatikanaji wa masoko. Tumeona wakulima wetu wengi wakikata tamaa kuendelea na sekta ya kilimo kwa ajili ya uhaba wa masoko, lakini natumia fursa hii kuipongeza Wizara kwa namna wanavyopambana kuhakikisha Wakulima wa Tanzania wanapata masoko ya mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi sana, nawapongeza NFRA ambayo inaongozwa na Ndugu yangu Dkt. Andrew Komba. Ndugu huyu namfahamu, nilifanya naye kazi kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara kipindi kilichopita kabla sijahamia Kamati nyingine. Ndugu huyu ni mchapakazi, mwadilifu na ni mtu ambaye anashirikisha sana Waheshimiwa Wabunge. Tuendelee kumwamini na kumpa ushirikiano aweze kuongoza sekta hii ili aendelee kutoa masoko kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Rais kwa anavyoendelea kuongeza fedha kwenye eneo la NFRA ili kuongeza uwezo wao wa kuhifadhi mazao. Ukiangalia kwenye hotuba ya Waziri, sekta hii, I mean NFRA, inaenda kuongezewa uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 400,000 mpaka tani 500,000, na pia Serikali ina mpango wa kuongeza mpaka zifike tani 3,000,000 Mwaka 2030. Kwa hiyo, tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Bashe, na pia tunampongeza kwa namna ambavyo anawajali Watanzania kwa kuwaongezea sehemu ya kuuza mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoiomba Serikali ni kuendelea kupunguza restrictions kwa wananchi wetu kuuza mazao yao nje. Serikali ikishanunua kiwango ambacho inahisi inakihitaji kuhifadhi, basi ziada inayobaki, wananchi waruhusiwe kwenda kuuza nje, ili wapate bei nzuri wanufaike na kilimo chao, hasa kilimo cha mahindi ambayo kule kwetu Tanga tunalima sana. Hiyo ilikuwa ni hoja yangu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ni kwenye kilimo cha umwagiliaji. Wananchi wengi wa Tanzania wanakuwa discouraged kuingia kwenye kilimo, kwa sababu hakitabiriki, kwa sababu kuna asilimia kubwa ya risk. Tulikuwa tunategemea mvua, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi hali imebadilika sana na mvua hazitabiriki au zinakuja nyingi kiasi kwamba wananchi wanapata hasara kwa sababu ya mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyoendelea kuongeza fedha kwenye Taasisi yetu ya Umwagiliaji na kila mwaka wanavyozidi kuongeza ekari ambazo wananchi watakuwa wanalima zaidi ya mara moja wakitumia umwagiliaji pasipokutegemea mvua. Haya ni mapinduzi makubwa kwenye nchi yetu ya Tanzania. Ninaamini watu wengi watakuwa wanakimbilia kilimo, lakini pia hata taasisi za kifedha sasa zitafungua mioyo yao na kukopesha wakulima kwa kuwa wana uhakika wakulima watakuwa wanaenda kuvuna kwa sababu miundombinu ya umwagiliaji ipo ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana Rais wetu kwa namna ambavyo anaendelea kuongeza fedha kwenye Tume yetu ya Umwagiliaji. Ukiangalia kwenye bajeti, zaidi ya shilingi bilioni 400 zimetengwa mwaka huu kupelekwa kwenye sekta ya umwagiliaji ambayo ni zaidi ya 30% ya bajeti nzima. Hii ni kazi kubwa ambayo Serikali yetu inaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nimpongeze kaka yangu na ndugu yangu Raymond Mndolwa kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kuisimamia Tume hii ya Umwagiliaji. Mwanzo nilihisi anapendelea tu Skimu za Tanga kwa sababu ndiko anakotokea, lakini siyo hivyo, kila Mbunge kila mahali anampongeza na kumsifu jamaa huyu kwa namna anavyosimamia skimu nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama ndugu yake ambaye tumeishi pamoja, namfahamu vizuri, natumia fursa hii kumpongeza. Pia namshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyomwamini. Naamini ataleta mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Umwagiliaji, tunamwomba Rais aendelee kumwacha pale, na tunamwomba Waziri Bashe aendelee kumwamini ndugu yetu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini nina skimu tatu kubwa za umwagiliaji, moja inaitwa Mahenge, nyingine inaitwa Kwa Mngumi, na nyingine Kwa Msisi. Mwaka 2023 tulisaini kandarasi ya kutengeneza Skimu ya Mahenge, lakini mwaka mzima hakuna kitu kilichofanyika na mkandarasi yule ameonekana hana uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru Waziri, lakini kupitia Ndugu yetu Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji walimtoa mkandarasi yule na sasa hivi skimu ile inaenda kutengenezwa kwa njia ya force account. Ninaiomba Wizara iiangalie Skimu ile ya Mahenge kwa jicho la kipekee kabisa ili ipate kukamilika kwa sababu ilikuwa ina matumaini makubwa. Wananchi waliamini msimu huu wanaenda kuingia kwenye kilimo, skimu ikiwa imekamilika, lakini mwaka mzima hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, chonde chonde ndugu yangu asimamie kwa kutumia ile force account ambayo wamepanga ili kutengeneza ile skimu ipate kukamilika. Pia nashukuru kwa skimu zangu mbili zilizobaki, Skimu ya kwa Mngumi na Skimu ya Kwa Msisi kwamba, ziko kwenye mpango wa mwaka huu na wanasema wanaenda kutangaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 walisema Skimu ya Kwa Msisi inatangazwa, lakini mpaka kufikia wakati huu hawajatangaza kusaini mkataba kwenye skimu ile. Sasa ninachoomba, Mheshimiwa Waziri mwaka huu kwa sababu wananchi wa Kata ya Kwa Msisi wamekuwa wanasumbua sana, wanahitaji mkandarasi apatikane ili waweze kutengenezewa ile skimu yao ya Kwa Msisi, kwa kuwa, ni sehemu ambayo wanaihitaji kwa ajili ya maisha yao kwa sababu hawana shughuli nyingine zaidi ya kilimo. Kwa hiyo, naomba skimu ile itangazwe ili iweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja na Mungu akubariki. (Makofi)