Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nami kupata fursa kuwa miongoni mwa wachangiaji katika bajeti ya Wizara ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu. Naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya ili niweze kusimama leo nikiwa na afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wenzangu ambao wamempongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya hasa katika sekta hii ya kilimo. Tunabaki na hadithi kuwa, katika nchi ambazo zina uhakika wa kujitosheleza kwa chakula ni pamoja na nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujitosheleza kwa chakula siyo kama ni jambo ambalo limekuja kama vile ni mtu unalala unaamka, linatokana na mipango thabiti ambayo imewekwa, mipango thabiti katika kuhakikisha kwamba kila mwananchi mkulima anafikiwa na mbolea. Inawezekana kwamba, kuna baadhi ya maeneo ya vijijini ambayo mbolea haikufika, lakini sisi wananchi wa Kalambo tuna kila sababu ya kusema ahsante kwa sababu mbolea hii imefika kwa walengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho. La kwanza, ni suala zima la mbolea kufika kwa wakati, lakini mbolea ambayo ndiyo hitaji la wananchi ifike. Kama wenzangu walivyokuwa wamesema, ni vizuri pia Mheshimiwa Waziri akaendelea kufikiria juu ya packaging ya mbolea. Siyo lazima wote wakanunua kilo 25 na kilo 50. Ifike wakati kwamba anayehitaji kilo tano apate, kilo 10 apate na kilo 20 apate, lakini na hao wanaohitaji kilo 25 waweze kupata na wapate kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika suala zima la ubora katika kilimo. Ili uweze kupata mahindi yaliyo bora na ili uweze kuwa competitive kwa maana ya uzalishaji unaoleta tija na kilimo kile ambacho kila mkulima akifurahie, ni pale ambapo tunakuwa na uhakika wa shamba ambalo limeandaliwa vizuri, lakini tuwe na uhakika wa mbegu zilizo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa katika mbegu ndiyo naomba nitumie muda mwingi kuelezea jinsi ambavyo tuna kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tunajitosheleza katika suala zima la uzalishaji wa mbegu. Mheshimiwa Waziri unajua, kama Taifa tumekuwa tukitumia mbegu ambazo zinatoka kwa majirani zetu. Kwa sisi ambao tuko mpakani, tunategemea mbegu kutoka Malawi na Zambia. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ametaka Taifa la Tanzania twende kwa kasi, hayo Mataifa yote ambayo nimeyataja sasa hivi, yana ukame mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Ni wakati mwafaka tuhakikishe kwamba tunazalisha mbegu za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia Watanzani na kwa ajili ya kuuza katika mataifa hayo ambayo sisi tumekuwa tukinunua kutoka kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba tukiwa na uhakika na mbegu iliyo bora ambayo inakubali, itakuwa ni chanzo cha mapato na katika mchango wa kilimo kwa kuingiza forex. Hili ni eneo mojawapo ambalo tunaweza tukafanya vizuri na tukazalisha mbegu za kutosha. Kwa uwekezaji ambao unawekwa katika bajeti ya kilimo, hatuna sababu ya kutokuzalisha mbegu za kutosha kwa ajili ya watu wetu na kwa ajili ya kuuza kwa majirani zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba niikumbushe Wizara, kuwa tunazo mbegu bora na nzuri, ni jambo moja, lakini siyo busara tukaamua kwamba kwa sababu tunazalisha hizi mbegu, basi tukasahau mbegu zetu za asili. Tusije tukafanya kosa hilo kubwa. Ukienda kwa wananchi ambao wanakuwa wanalima mahindi, wanajua mbegu zao za asili ambazo zina uvumilivu mkubwa sana katika kupambana na maradhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiwa na la kwako unajivuna. Isije ikafikia mahali kwamba lazima tutoe mbegu kwa hao ambao wametuletea, halafu tukaua kabisa mbegu zetu za asili. Hii iende kwenye mazao yote, kwa maana ya mahindi, ulezi, ngano na mtama. Ni vizuri kitengo hiki ambacho kinahakikisha kwamba tunakuwa na mbegu zetu za asili, tuzilinde kwa wivu mkubwa sana. Wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba katika hizi mbegu zetu za asili tunafanya maboresho ili ziweze kuwa zinazalisha kwa wingi na kwa ubora ambao unatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongelea habari ya kuwa na shamba lililoandaliwa vizuri na mbegu iliyo bora na mbolea ambayo inatakiwa. Hili naomba niipongeze Wizara, wameanzisha jitihada za kuhakikisha kwamba udongo unapimwa. Ukishakuwa unajua afya ya udongo, kiasi cha mbolea ambayo inatakiwa kuwekwa utakuwa unajua, kwa sababu siyo kila udongo unahitaji Urea na siyo kila udongo unahitaji DAP. Ifike mahali ambapo sisi kama Taifa tujivunie kwamba maeneo yote yamepimwa kwa maana ya kujua afya ya udongo, na pia tuwe na uhakika kiasi gani cha mbolea na aina gani ambayo inatakiwa kutumika katika ardhi yetu. Hii itakuwa tunawasaidia wakulima wetu. Siyo busara unaambiwa kwamba ekari moja utumie mifuko mitatu ya Urea. Wakati mwingine unakuwa unazidisha udongo tayari hauhitaji Urea lakini kwa sababu tumeshakariri kwamba Urea ndiyo inatakiwa, inakuwa haitusaidii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishakuwa na uhakika wa mazao yaliyo bora, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba mwananchi huyu aliye Kalambo anahakikishiwa soko la uhakika la mazao yake kama ni mahindi, ulezi na mtama. Siyo kazi yake alime halafu ahangaike kutafuta soko. Suala la kutafuta soko bado libaki mikononi mwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa kupitia kitengo chake cha NFRA, kulikuwa na kitengo kinahangaikia suala zima la kutafuta masoko na masoko twende kuyatafuta huko duniani. Serikali ndiyo mna uwezo wa kuongea kwa misuli yenu kwa mawasiliano mliyonayo na mahusiano mliyonayo kuhakikisha kwamba kama ni mahindi tunapeleka South Sudan, Congo, Kenya, Malawi na Zambia. Siyo kazi ya Mwananchi wa Kalambo kwenda kutafuta soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtusaidie ili tuwe na uhakika wa kwamba tukiwa tunalima tuna uhakika wa soko, tunapata hamu ya kwenda kulima mwaka unaofuata, lakini kama mwaka huu tunakuwa na bei nzuri halafu mwakani bei ikawa siyo nzuri, hakika kilimo hakitakuwa kivutio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo ambao tumeuanza na mwendo huu ambao Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wanaenda, wakaze buti, inawezekana ndani ya muda mfupi mchango kutoka kwenye sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya Watanzania 75% ukaonekana kwa wazi kabisa. Ifike mahali kuwe na malengo ya kwamba itafika mahali ambapo badala ya kwamba Wizara iwe inapata pesa kutoka Serikali Kuu, kilimo ndicho ambacho kiwe kinatoa pesa kupeleka Serikali Kuu na wakati mwingine hata ruzuku tusitarajie kwamba itakuwepo miaka yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala zima la mazao ya chakula kwa maana ya mafuta. Kumekuwa na notion kwamba ukitaka michikichi, maana yake ni Kigoma peke yake, la hasha! Narudia tena michikichi inakubali mwambao wote wa Ziwa Tanganyika na inakubali hata ukienda Kyela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja.