Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa juhudi. Kwa kweli anachakarika. Baada ya kusema hayo, mimi nitatoa maoni na ushauri na ninaomba Mheshimiwa Bashe, haya ninayoyasema hapa sasa hivi, leo ayaandike hapo. Namwambia hivi, mimi lazima shilingi nitaishika na anajua nakwenda kuzungumza nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na suala la hiki kilimo cha jembe la mkono. Mheshimiwa Waziri amekuja na programu kibao, mimi nikafikiria, hizi programu ni kwa ajili ya wakulima wadogo hawa wa Mdundualo au anawalenga wakulima hawa wakubwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jembe la mkono, nasema haya mambo anayoyapanga itakuwa ni ngumu. Hebu sasa tuamue, wakati CAG akija hapa akisema fedha zimeliwa nyingi, inasikitisha. Hebu tuamue hizi fedha sasa kila kijiji kipate matrekta. Kazi kubwa ya kilimo ni kulima. Ule ukulima ndiyo unaowatesa wakulima. Umefanya vizuri kwenye suala la mbolea, lakini sasa wanalima kiasi gani hawa wakulima wadogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mtu anaweza kulima ekari mbili tu amechoka, akiweza sana ekari tatu, lakini tungekuwa na matrekta kama enzi zile za Mwalimu Nyerere, wakulima hawa wangeweza kulima ekari za kutosha. Pia hata miili yao na afya zao ziwe nzuri, hebu tujielekeze huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linakwenda sambamba na mikopo wanayoitoa kwenye hizo benki za Mheshimiwa Bashe. Hivi, hiyo mikopo wanayoitoa ni mikopo kwa ajili wakulima wadogo au ni mikopo kwa wakulima wakubwa? Benki zinaweza kumkopesha mkulima huyu mdogo ambaye fedha zake wakati mwingine unakuta wanahitaji shilingi 500,000 au shilingi milioni moja, lakini benki zinawakopesha wakulima gani? Ndiyo maana wakulima wetu wanaingia kwenye hiyo mikopo ya kukausha damu kwa sababu benki zimeshindwa kuwasaidia wakulima wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nilijaribu kuwaomba waende wakapate mkopo, shilingi 500,000 sijui shilingi 200,000 kwenye benki, hawapati. Sasa hii TADB ni kwa ajili ya wakulima gani Mheshimiwa Bashe? Tuliangalie hilo. Ukulima wa jembe la mkono hauwasaidii kabisa wakulima wadogo. Hii mipango yote, umesema hapa vipaumbele mazao 20 yale ya umwagiliaji, hivi watalima wakulima wadogo kweli kwa jembe la mkono! Mheshimiwa Bashe umejitahidi ukapeleka pikipiki, ingawa hizo pikipiki nikwambie zimekaa ofisini pale Halmashauri, ukiwapigia simu wanakwambia weka mafuta. Mimi nitaweza, kwani mimi ni Mbunge, hivi mkulima yule wa Mdundualo ataweza kuweka mafuta? Kwenye wale wataalam wako, sasa nikwambie zile pikipiki haziwasaidii wakulima wadogo, zinakwenda kwa wakulima wenye uwezo tu, hawa wakulima wakubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili liangaliwe. Wapeleke power tiller na matrekta kwa wakulima vijijini. Kila kijiji kiwe na matrekta angalau mawili au matatu, tutafanikiwa kwa hilo, lakini hivi hivi tutakuwa kila siku tunasema wakulima na tunawasifia wanatulisha, lakini wanatulisha kwa mateso makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke hapo sasa niende huko kwenye zao analolipenda Mheshimiwa Bashe, alikuwa anazungumza wakati ule nilikuwa nafurahi, anawatetea wakulima sana. Sasa nije kwenye kilimo cha tumbaku. Hili zao Mheshimiwa Bashe naomba aendelee nalo kwa sababu anasema linaleta fedha za kigeni. Likileta fedha za kigeni haziwasaidii wakulima wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri kwamba, hii tumbaku aende nayo kwa wakulima wakubwa tu kama akina Mheshimiwa Cherehani, hao wanalipenda, lakini wakulima wadogo wa tumbaku wanateseka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mvua imenyesha, mabani yote yameanguka kwa sababu hawana mabani bora. Kwa hiyo wanateseka, afya zao ni mgogoro. Wakulima wa tumbaku, kama Mheshimiwa Waziri anasema lina faida, twende tuongozane, kwenye block farm, twende Namtumbo akaone makazi yao. Bado wanakaa kwenye zile nyumba tunaziita mbavu za mbwa. Afya zao, wanaumwa vifua. Hebu hili zao la tumbaku kwa wakulima wadogo tuliondoe, siyo taratibu, tuliondoe mapema sana. Kuna mazao ambayo wanaweza wakalima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Manyanya, kule kwake Nyasa mlitaka kumpelekea tumbaku. Nyasa ni Wilaya ambayo ni maskini kwa kweli, yeye akajikita kwenye kahawa na mpunga kwa umwagiliaji. Hayo ni mazao ambayo wakulima wadogo wanaweza wakayalima. Mheshimiwa Bashe angalia, leo nenda Mbinga, Magugu kule Babati, wakulima wadogo wanalima mpunga na maisha yao ni mazuri, angalia nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mbinga leo, wakulima wadogo wa kahawa watasema hili zao safi, ukienda Mbinga tena Mheshimiwa Spika angekuwepo ningemwambia, hebu mtembeze, mpeleke Mheshimiwa Spika Mbinga mkaangalie kule nyumba za wakulima wadogo, hapo ndiyo utasema zao la kahawa lina faida kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tumbaku Mheshimiwa Bashe, ahangaike na wakulima wakubwa tu, na hawa wanunuzi kwanza. Kwa tumbaku nikwambie ukweli, kwanza mkulima mdogo hawezi kupata grade one wala grade two wanapo-classify tumbaku zao. Hao wakulima wadogo kulipwa inakuwa ni balaa. Anafanya kazi miezi nane au tisa hajalipwa, wanaishia tena kukopwa. Kwa hiyo, wale wakulima wakubwa na wanunuzi wanawatumia wakulima wadogo ili wapate tumbaku na wapate pesa, lakini huyu mkulima mdogo ananyanyasika mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niliwahi kulima tumbaku wakati huo siyo Mbunge, nafanya kazi nyingine, sijawahi kupata grade one wala grade two, mpaka uzungumze na ma-classifier. Kwani hilo Mheshimiwa Bashe wewe hulijui! Hulijui hilo! Hebu tuwasaidie wakulima wadogo, ondoa zao la tumbaku kwa wakulima wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia Mheshimiwa Waziri, aende akaangalie kule, wale wakulima wa block farm ni majirani zangu, nyumba zao kwanza hazina adabu, kwa sababu wanatumia mbavu za mbwa, matundu kila mahali, watoto wanalala chumba hiki, wazazi wanalala chumba hiki, hakuna heshima kabisa. Halafu bado mnasema tumbaku inaleta foreign currencies. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, foreign currency haimsaidii mkulima mdogo. Niambie wamefaidika kwa kitu gani? Hapo nakwambia usiponiambia leo umejipangaje kuliondoa hili zao la tumbaku, nitakushangaa. Namtumbo ni Wilaya ya mwisho kabisa kule, umaskini umejaa, wanalima tumbaku hawapati chochote. Hapana, lazima tuwaonee huruma watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu hii miradi ya umwagiliaji, mmejinasibu toka mwaka 2023 naisikia. Sasa naomba kwanza Waziri atuambie, miradi mingapi ya umwagiliaji imefanikiwa mpaka sasa? Pia huko Litui kwetu kuna vijiji vinaitwa Kimbande, Lundo na Chiulu, hiyo miradi ya umwagilijai imefikia wapi? Akinijibu hayo, yeye na mimi hapo tutapatana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niendelee kusema, Mheshimiwa Waziri azungumze na wanunuzi wako wakubwa, wajielekeze kwa wanunuzi wakubwa waache kwenda kuwanyanyasa wakulima wadogo wa tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)